Articles by "TAWIRI"
Showing posts with label TAWIRI. Show all posts

 


Ujenzi wa jengo la  ghorofa tatu (03) la Makao Makuu ya Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) unaoendelea jijini Arusha, ni hatua muhimu inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika  kuimarisha miundombinu ya utafiti, uhifadhi na usimamizi endelevu wa rasilimali za wanyamapori nchini ambapo hadi  sasa imetoa  shilingi bilioni 2.5.

Jengo hilo linakuja wakati ambapo Tanzania inazidi kuimarisha nafasi yake kama moja ya mataifa yenye utajiri mkubwa wa wanyamapori na vivutio vya utalii barani Afrika ambapo imetwaa tuzo mbalimbali za kimataifa za utalii. Ujenzi huu ni  juhudi za kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza uwezo wa TAWIRI kutekeleza  jukumu kuu la Kufanya, Kuratibu na Kusimamia tafiti za wanyamapori nchini.

Mkurugenzi Mkuu TAWIRI, Dkt. Eblate Mjingo ameishukuru Serikali kwa kuwezesha ujenzi wa jengo la makao Makuu ya Taasisi hiyo unaoendelea ambapo ndani ya  jengo  hilo kutakuwa na ofisi za watumishi, maabara za wanyamapori pamoja na kumbi za mikutano

“ Miundombinu hii  itatoa mazingira bora zaidi kwa watafiti na watumishi wote kufanya kazi na kuendelea kutoa taarifa za kisayansi ambazo ni tija katika uhifadhi wa wanyamapori hapa nchini kwa utalii endelevu” amebainisha Dkt. Mjingo

Aidha, Ujenzi wa jengo hilo ulioanza  Januari 5,2026 na unatarajiwa kukamilika 05/01/2028 utagharimu Bilioni 8.9 za Kitanzania na utachangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambapo Sayansi na Teknolojia ni miongoni mwa vichocheo vitakavyo saidia hatua madhubuti za kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia katika kukidhi mahitaji ya jamii na uchumi endelevu.

Ikumbukwe kuwa TAWIRI ni Injini katika Maendeleo ya sekta ya Uhifadhi na Utalii.





 


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii leo Agosti 18, 2026 Bungeni Jijini Dodoma, imeipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi yake ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania(TAWIRI)

Kwa namna inavyofanya jitihada za kugundua mbinu mbalimbali za kupambana na kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu.

Pongezi hizo zimetolewa wakati kamati hiyo ikipokea  na kujadili taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya utendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI). 

“ tunaona na kuthamini kazi nzuri ya Wizara kupitia TAWIRI kwa kufanya tafiti zilizosaidia kupata njia bora zinazoonesha matokeo chanya katika kudhibiti wanyama wakali na waharibifu” amesema Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Timotheo Mnzava

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ameihakikishia Kamati kuwa , Wizara hiyo itaendelea kuziwezesha taasisi zake ili ziendelee kufanya kazi kwa  ufanisi na kufikia malengo yanayotarajiwa, 

“ Wizara na wataalamu wake wapo kazini kila wakati kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuifanya Sekta ya Maliasili na Utalii kuendelea kuwa na mchango mkubwa katika ustawi wa wananchi na taifa kwa ujumla” amebainisha Dkt. Kijaji

Ikumbukwe mbali na jukumu la Kufanya, Kuratibu na Kusimamia tafiti za wanyamapori hapa nchini, TAWIRI inajukumu la kuishauri serikali juu ya masuala yote ya sayansi ya wanyamapori kwa uhifadhi endelevu, ustawi wa jamii na kukuza utalii.







 


Wanawake kikundi cha UMOJA kilichopo Wilaya ya  Mtama Mkoani Lindi wamejengewa uwezo na Mtaalam kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) juu ya ufugaji bora wa nyuki na uongezaji  thamani mazao ya nyuki ambapo wameweza kutengeneza bidhaa mbalimbali kama vile Sabuni, Mafuta ya kujipaka , mishumaa ambazo zinatokana mazao ya nyuki (asali na nta)

Bi Amina  Nandilika ambaye ni Mwenyekiti wa kikundi hicho amesema  mafunzo hayo Yana tija katika kuongeza kipato chao kwani awali walikua wakinufaika na asali pekee “ mafunzo haya yatatuwezesha kuandaa bidhaa nyingi zaidi kwa ubora wa juu” amefafanua Nandilika

Mtafiti kutoka TAWIRI  Bw. Jackson Vicent Kizeze amesema tafiti za nyuki zinazofanywa na TAWIRI kupitia Kituo cha utafiti wa wanyamapori Njiro zinalenga kupata taarifa za kisayansi zinazosaidia kuleta tija katika Sekta ya nyuki ambapo amewakaribisha wadau na jamii kuja TAWIRI ili kujifunza juu ya ufugaji bora wa nyuki na uongezaji thamani mazao ya nyuki.







 


Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) ni miongoni kwa washiriki wa  Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) Mkoani Arushs inayofanyika Mei 1, 2025, katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Aidha,  watumishi wa TAWIRI wameonesha  umahiri wao kupitia maandamano ya miguu na pia kupitia gari la maonesho, ambalo lilikuwa moja ya vivutio vikubwa katika maandamno haya,  ilikuwa ni fursa kubwa kwa  wafanyakazi wa TAWIRI kunadi mchango wa taasisi  katika uhifadhi wanyamapori nchini .

Kupitia machapisho, vipeperushi, video na sanamu za wanyamapori, TAWIRI ilidhhirisha mbele ya mgeni  rasmi na umma  wa Arusha  namna tafiti zake zinavyosaidia kuelimisha na kutatua changamoto za uhifadhi ili kuwezesha maendeleo endelevu ya sekta ya utalii, na maisha bora ya Jamie.

Kitaifa, maadhimisho ya Mei Mosi, 2025  yanafanyika mkoani Singida, ambapo Mgeni Rasmi ni Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.












 

Taasisi  ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania(TAWIRI) imegundua dawa ya kuotesha nywele au kuzuia nywele kutoka kwa binadamu kutokana na mimea inayotumika kama tiba asili ugunduzi huo ulianza  mwaka 2013 na kukamilika mwaka huu katika mimea inayotumika kwa tiba asili katika ukanda wa kaskazini mwa Tanzania katika wilaya za Ngorongoro, Mbulu na Hanang kwa watu jamii ya Masai, Hadzabe, Datoga na Iraqw.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Arusha kuhusu ugunduzi wa dawa ya kuotesha nywele au kuzuia nywele kutoka kwa kutumia mmea uitwao Mporojo, Mkurugenzi wa Utafiti kutoka TAWIRI, Dkt, Julius Keyyu amesema taasisi hiyo imefanya utafiti kwa kipindi cha miaka 12 na hatimaye imepata dawa hiyo ya watu wenye changamoto za vipara pamoja na nywele kutokuota

Dk, Keyyu alisema mmea huo kwa kiingereza unaitwa wormwood albizia, bitter false thorn, jina la kisayansi unaitwa Albiziaanthelmintica na kwa Kimasai unaitwa Ormuktan ambapo wamasai wanatumia magome na mizizi yake kutibu minyoo, malaria na maumivu ya miguu, mgongo na misuli. 

Alisema Utafiti huu ulikwenda zaidi ya matumizi haya na kugundua uwezo wa mmea huu kuotesha nywele au kuzuia nywele kutoka na tayari umepata hati miliki (Hataza) hii inaitwa ‘Composition for Hair Growth Stimulation or Hair Loss Prevention Using an Extract of Albizia anthelmintica’.

Alisema Tawiri ni taasisi ya wanyamapori lakini pia inapofanya tafiti hizo inakwenda sanjari na mimea na ndio maana wamebaini mmea huo wa Mporojo unasaidia nywele kuota na kukua zaidi kwa wale wenye changamoto za kutokuota nywele kwa wanawake na wanaume

Alisema gharama yake ni kwa shampoo ni sh, 31,000 na sh, 75,000 mafuta sawa na dola12  kwa shampoo na dola 24 kwa mafuta kwa jumla na upande wa rejareja ni sh, 76,000 kwa shampoo na sh, 152,000 kwa mafuta endapo wakipata mawakala wa ndani na nje ya nchi baada kusaini mkataba wa makubaliano kati ya TAWIRI na mawakala. 

Alisema teknolojia ya Hataza hii imetolewa (patent transfer) kwa kampuni ya Winwik Enterprise co. ltd ya Korea Kusini ambayo ni watengenezaji wa Kimataifa wa dawa na vipodozi. 

"Tayari kampuni hii imeshatengeneza dawa ya kuotesha nywele (Albizia Hair Loss Care) katika mfumo wa Shampoo (shampuu ya wanawake na wanaume), Dawa(Treatment), na Mafuta (Hair Essence Tonic),Dawa/ vipodozi hivi vitaanza kupatikana kwa bei ya jumla kwa mawakala na pia rejareja hivi karibuni."

Alisema utafiti wa jinsi ya kuotesha Mporojo (propagation) kwa ajili ya kilimo umeanza ili kuzuia mmea huu kutoweka kutokana na uvunaji wa magome kutoka mimea iliyopo porini

Alisema lengo la  utafiti huo lilikuwa kufanya ugunduzi wa dawa na vipodozi kutokana na bioanuwai ya mimea inayotumika kwa tiba asili na pia kubaini mimea inayotumika kwa tiba asili ambayo iko katika hatari ya kutoweka ili kuihifadhi katika bustani za mimea au ‘botanical garden’.

Alisema kutokana na utafiti wa bioanuwai ya mimea inayotumika kwa tiba asili, watafiti wa Tawiri  wamepata Hataza  tatu za ugunduzi wa dawa au vipodozi asili ambazo ni  dawa hiyo ya kuotesha nywele au kuzuia nywele kutoka kwa kutumia mmea uitwao Mporojo Alisema dawa ya  ya kuotesha nywele (Albizia Hair Loss Care) imetengenezwa katika mfumo wa shampoo (shampuu ya wanawake na wanaume), dawa (Treatment), na Mafuta (Hair Essence Tonic).

Alisema dawa na vipodozi hivyo vitaanza kupatikana kw bei ya jumla kwa mawakala na pia rejareja hivi karibuni kwanni dawa au vipodozi hivi vinatumika kuotesha nywele, kuboresha,  kuimarisha nywele (zisikatike, kuwa nyingi), kuzuia nywele kutoka (kuzuia kipara), au kuondoa kipara.

Aidha, kutokana na utafiti huo, taasisi hiyo pia imepata hataza  nyingine mbili kutokana na bioanuwai ya mimea inayotumika kwa tiba asili ambazo ni ugunduzi wa kipodozi cha kung’arisha ngozi na kuondoa makunyanzi kwa kutumia mmea wa Mugufe. 

Alisema Mmea huo kwa kiingereza unaitwa Evergreen shrub,blue bush cherry, na kwa jina la jina la kisayansi la mmea huu unaitwa Maerua edulis ambapo mmea huu kwa Kidatoga unaitwa Ekwida na jamii hii inatumia majani yake kutibu minyoo, tumbo na ngiri

Alisema utafiti huo ulikwenda zaidi ya matumizi haya na kugundua uwezo wa mmea huu  katika kung’arisha ngozi na kuondoa makunyanzi na kuongeza kuwa 

Teknolojia ya hataza hii bado haijanunuliwa au kupewa kampuni yoyote, hivyo bado taasisi na washirika wake wanaendelea kuitangaza ili kupata  atakayeihitaji ili kutengeneza kipodozi cha kung’arisha ngozi na kuondoa makunyanzi.

Pia wamegundua dawa nyingine ya tatu ambayo ni dawa ya kuotesha nywele au kuzuia nywele kutoka kwa kutumia mmea uitwao Chimbulei (Kigwala, Mphata na kuongeza kuwa mmea huo kwa kiingereza unaitwa Apple leat, broadlance-pod na kwa jina la kisayansi unaitwa Lonchocarpus eriocalyx. 

Alisema mmea huo kwa Kisonjo unaitwa Ekurehe ambapo Wasonjo wanatumia magome na mizizi yake kutibu kikohozi na mafua kwani utafiti huu ulikwenda zaidi ya matumizi hayo na kugundua uwezo wa mmea huu kuotesha nywele au kuzuia nywele kutoka. 

Kwamujibu wa Dk, Keyyu alisema teknolojia  hiyo bado haijapewa kampuni yoyote, hivyo bado taasisi na washirika wake wanaendelea kuitangaza ili kupata atakayeihitaji ili kutengeneza dawa ya kuotesha nywele au kuzuia nywele kutoka.

Wakati huo huo, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri, Rogastian Msafiri alisisitiza utafiti huo ni nyota njema kwa nchi ya Tanzania katika kuhakikisha ataza mbalimbali zinalindwa ili kuhakikisha mimea asil8 inatunzwa na watafiti kufanya tafiti mbalimbali na kuja na matumaini mengine kwa jamii na wanyamapori. 







 


Wataalam sekta za Wanyamapori na Misitu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Wizara ya Maliasili na Utalii  na Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakutana Jijini Arusha, kujadili utekelezaji wa mashirikiano baina ya pande mbili kwa ustawi wa uhifadhi na kukuza utalii nchini.

Wakizungumza wakati wa kikao hicho viongozi wa pande zote mbili, Bi. Kay Kagaruki, Mkurugenzi Msaidizi Matumizi Endelevu ya Wanyamapori , Kutoka Wizara ya Malisili na Utalii, Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Bw. Said Juma Ali Mkurugenzi wa Misitu, Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar wamesema  mashirikiano hayo yameleta tija katika sekta ya uhifadhi wa wanyamapori, Misitu na Utalii.

Aidha, Miongoni mwa mada zilizojadiliwa katika kikao  kazi hicho ambacho kimefanyika makao Makuu ya TAWIRI, ni pamoja na utekelezaji wa Mikataba ya Kikanda na Kimataifa, udhibiti wa ujangili, utoroshwaji wa nyara, usimamizi wa rasilimali za misitu, nyuki na wanyamapori, utafiti na biashara katika sekta za misitu, nyuki na wanyamapori na uendelezaji Utalii.








 


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana(Mb) amekagua maabara ya  ithibati (Acreditation)ya mazao ya nyuki inayosimamiwa na  Taasisi  ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kupitia kituo chake cha utafiti wa Wanyamapori Njiro ambacho kimejikita kwenye utafiti wa nyuki na mazao yake.

Akikagua Maabara hiyo ya  kuchakata mazao ya nyuki  kwa  viwango vya kimataifa leo Novemba 14,2024. Mhe. Chana ametoa wito kukamilisha maabara hiyo  ambayo itaongeza pato la taifa kwa nchi kupata fedha za kigeni kupitia soko la kimataifa la mazao ya nyuki ikiwemo asali pamoja na uchumi wa moja kwa moja kwa wananchi.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi Shupavu wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inahakikisha wananchi wananufaika na fursa zilizopo kwenye maliasili ikiwemo sekta ya nyuki“ amesema Mhe.Chana.

Naye, Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Wanyamapori Njiro, Dkt. Alfred Mariale amesema maabara ya ithibati itakamilika mwanzoni mwa mwaka 2025 na itasaidia kuharakisha biashara ya mazao ya nyuki katika soko la Kimataifa ambapo awali Serikali ilikuwa inatumia gharama kubwa kupeleka sampuli  nje ya nchi  kuthibitisha viwango vya ubora “Sample zilikuwa zinachukua miezi 6 kupata majibu  na kusababisha kupoteza soko kupotea” ameeleza Dkt.Marriale

 


Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu  ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kwa shughuli za utafiti wa Wanyamapori ambazo zina tija katika  sekta ya uhifadhi na utalii  ambayo inachangia asilimia 17% ya pato la Taifa.

Akizungumza  jijini Arusha wakati wa kikao na Menejimenti ya TAWIRI, Bw. Mchechu  amesema Ofisi ya msajili wa Hazina  itaendelea kushauri vyema katika kuimarisha Mashirika ya Umma yaweze kujiendesha kwa tija.

“nawapongeza kwa utendaji mzuri, nitoe wito kuendelea kuwa wabunifu kutumia  rasimali mlizo nazo kujiendesha kwa ufanisi” amehimiza  Bw.Mchechu

Naye, Mkurugenzi Mkuu TAWIRI Dkt, Eblate Mjingo amesema TAWIRI ni taasisi ya kimkakati  ambayo mbali na kutokuonekana  ikizalisha  fedha moja kwa moja ina mchango  mkubwa katika mapato yatokanayo na utalii nchini ambapo takwimu na taarifa za tafiti ndizo zinazonadi utalii na kuimarisha uhifadhi

 

Shirika la Hifadhi ya Taifa TANAPA wameanza mpango wa kudhibiti wanyamapori, wakiwemo tembo wasivamie maeneo ambayo ni makazi ya watu kwa kwa kuwavalisha mikanda ya  kielektroniki yenye kutoa ishara ya utambuzi walipo hasa kama wameondoka katika hifadhi.

Taarifa ya kutekelezwa kwa mpango huo imetolewa na Mkuu wa Uhifadhi kanda ya Mashariki Kamishna msaidizi mwandamizi John  Nyamuhanga wakati mwa utekelezaji wa zoezi la kuwaweka mikanda ya mawasiliano makundi mbalimbali ya wanyama waharibifu.

Nyamuhanga amesema zoezi hilo ni mikakati ya makusudi inayofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori, TAWIRI, katika kupunguza muingiliano baina ya wanyamapori na wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi za Taifa.

Alisema matumizi ya teknolojia za kisayansi ya kuwavalisha Wanyamapori wakali na waharibifu mikanda yenye mfumo wa mawasiliano ili kutambua na kudhibiti mienendo yao itasaidia kupata taarifa za mienendo ya wanyama hao  mapema  na hivyo kuwazuia au kuwarejesha hifadhinikabla ya kusababisha madhara kwa jamii.
 
Awali akizungumzia teknolojia hiyo, Mtafiti kutoka TAWIRI, Dk Justin Shamanche amesema kifaa hicho kinauwezo wa kutoa ishara pindi mnyama akitoka nje ya mipaka hifadhi hivyo kutoa fursa kwa wananchi kujipanga kwa njia nyingine kuweza kurudisha ndani ya hifadhi.

Naye Ofisa Uhifadhi mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa Saadani, Prisca Elisia amesema pamoja na kusaidia wanyama hao wasilete vurugu katika maeneo jirani na hifadhi pia inasaidia sekta ya utalii kwa kutambulisha wanyama wapo wapi hivyo kuwa rahisi kwa watalii kufika walipo na kuwaona.

" Teknologia hiyo itasaidia sekta ya utalii kwa wageni kuweza kumuona mnyama wanaemtaka kwa wakati badala ya kumtafuta mnyama kiholela" alisema Prisca.

Naye mwakilishi kutoka kiwanda cha sukari cha Bagamoyo, Jeremia Mponji alielezea kufurahishwa na kuingizwa kwa teknolojia hiyo kwani wamekuwa wakipata hasara sana katika shamba lao la miwa.

Alisema mashamba yao yamekuwa yakivamiwa sana na tembo hivyo kuja kwa teknolojia hiyo anaamini itawasaidia maofisa uhifadhi kuwaswaga kuwarejesha  hifadhini kirahisi.



 Wakazi wa jiji la Dar es Salaam wametakiwa kuchukua taadhari kutokana na kuwepo kwa uwezekano wa Mamba na Viboko kuzagaa kwenye maeneo ya makazi baada ya kusombwa na maji yaliyotokea kwenye mito kuelekea Baharini baada ya kunyesha kwa mvua kubwa zilizosababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali nchini.


Tahadhari hiyo imetolewa na Mhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA, Kanda maalum ya Dar es Salaam, Zawadi Malunda Mei 11,2024 wilayani Kigamboni Mkoani Dar es Salaam wakati akitoa elimu kwa Wananchi kuhusu uwepo wa wanyamapori hao.

Amesema, wanyamapori hao wanaweza kuwa wamebaki katika mito, madimbwi ya mitaani na kwenye makazi ya watu, hivyo kusababisha athari kwa jamii kwani husombwa na maji ya mito inapofurika kuelekea baharini kupitia mito, vijito na maji yaliyotuama jirani na makazi ya watu, hivyo kuweza kusababisha athari kwa jamii.

Malunda amewataka wananchi kutoendesha shughuli zao ndani ya Madimbwi, Mito, Mabwawa bila tahadhari ikiwa na kuzingatia kilimo cha umbali wa zaidi ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji.

Kwa upande wake Mhifadhi toka TAWA, Sanjo Mafuru amesema tabia ya baadhi ya wananchi wanaoharibu kingo za mito, vyanzo vya maji na wanaofanya shughuli za uvuvi haramu wa kutumia sumu pamoja na shughuli za kilimo ni chanzo cha mamba na viboko kulazimika kuyahama makazi yao ya asili na kukimbilia kwenye maficho yaliyo jirani na makazi ya watu.

Amesema, mahali penye vitendo vya uharibifu wa mazingira panakuwa ni vichocheo vya mabadiliko ya tabia nchi ikiwa ni pamoja na uwepo kwa mvua nyingi zinazosababisha mafuriko au kiangazi kikavu kinachosababisha wanyamapori kutoka eneo moja kwenda jingine ikiwemo kwenye makazi ya watu.



Timu ya Wataalamu kutoka Wizara  ya Maliasili  na  Utalii  imewasili katika Wilaya Mbarali, Mkoani Mbeya kuratibu zoezi  maalumu  la kuwaondoa tembo kwenye makazi ya watu katika  kata tano za Igava, Mawindi, Miyobweni, Imalilosongwe na Rujewa ambapo zoezi litaanza katika  vijiji vya Kata ya Igava ambavyo  vimeathiriwa zaidi na uvamizi wa tembo.  

Akizungumzia zoezi  hilo , Mwakilishi  wa  Wizara  ya  Maliasili  na  Utalii  Antonia Raphael amesema  zoezi hilo litafanyika kwa  muda wa siku mbili kuanzia tarehe  08 hadi 09 Mei, 2024 ambapo teknolojia  ya  helikopta  itatumika kuwaswaga tembo hifadhini sambamba na kuwafunga  mikanda maalum ya mawasiliano  (GPS satellite Collars) tembo viongozi wa makundi ili kufuatilia mienendo yao.

Vilevile,  Anthonia amesema kuwa zoezi hilo litaongozwa na Mheshimiwa  waziri  wa Maliasili  na Utalii.

Naye, Dkt. Emmanuel  Masenga  ambaye  ni  Mtafiti  Mkuu kutoka Taasisi  ya Utafiti  wa  Wanyamapori  Tanzania  (TAWIRI) amebainisha kuwa maandalizi  ya zoezi hilo  yamekamilika ambapo timu ya wataalamu kutoka Wizara  ya Maliasili  na Utalii  na taasisi  zake za TAWIRI, TANAPA, TAWA  pamoja  na timu kutoka Wilaya ya Mbarali  zipo uwandani kuhakikisha zoezi la kuwaondoa tembo kwenye  makazi  ya watu linaanza kesho kwa ufanisi.

Dkt.Masenga  amesema teknolojia  ya helikopta  imekuwa  na manufaa katika kuwaondoa tembo kwenye makazi ya watu kwa haraka zaidi.

Naye, mwakilishi  wa  Mkuu wa Wilaya  ya  Mbarali, Donald Mwigombe ambaye pia ni Afisa Tarafa ya Rujewa, ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari  wakati wa zoezi la kuwaswaga tembo kutoka kwenye makazi ya watu  ambapo amewataka wananchi kutokusogea karibu na tembo, wakati  zoezi linaendelea ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na tembo pindi wanaposwagwa kwa helikopta.