Wakazi wa jiji la Dar es Salaam wametakiwa kuchukua taadhari kutokana na kuwepo kwa uwezekano wa Mamba na Viboko kuzagaa kwenye maeneo ya makazi baada ya kusombwa na maji yaliyotokea kwenye mito kuelekea Baharini baada ya kunyesha kwa mvua kubwa zilizosababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali nchini.


Tahadhari hiyo imetolewa na Mhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA, Kanda maalum ya Dar es Salaam, Zawadi Malunda Mei 11,2024 wilayani Kigamboni Mkoani Dar es Salaam wakati akitoa elimu kwa Wananchi kuhusu uwepo wa wanyamapori hao.

Amesema, wanyamapori hao wanaweza kuwa wamebaki katika mito, madimbwi ya mitaani na kwenye makazi ya watu, hivyo kusababisha athari kwa jamii kwani husombwa na maji ya mito inapofurika kuelekea baharini kupitia mito, vijito na maji yaliyotuama jirani na makazi ya watu, hivyo kuweza kusababisha athari kwa jamii.

Malunda amewataka wananchi kutoendesha shughuli zao ndani ya Madimbwi, Mito, Mabwawa bila tahadhari ikiwa na kuzingatia kilimo cha umbali wa zaidi ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji.

Kwa upande wake Mhifadhi toka TAWA, Sanjo Mafuru amesema tabia ya baadhi ya wananchi wanaoharibu kingo za mito, vyanzo vya maji na wanaofanya shughuli za uvuvi haramu wa kutumia sumu pamoja na shughuli za kilimo ni chanzo cha mamba na viboko kulazimika kuyahama makazi yao ya asili na kukimbilia kwenye maficho yaliyo jirani na makazi ya watu.

Amesema, mahali penye vitendo vya uharibifu wa mazingira panakuwa ni vichocheo vya mabadiliko ya tabia nchi ikiwa ni pamoja na uwepo kwa mvua nyingi zinazosababisha mafuriko au kiangazi kikavu kinachosababisha wanyamapori kutoka eneo moja kwenda jingine ikiwemo kwenye makazi ya watu.

Share To:

Post A Comment: