Saturday, 21 July 2018

Zahanati yateketea kwa moto, watano wadakwa akiwemo mtendaji

Watu watano akiwamo ofisa mtendaji wa kijiji cha Ulaya, wilayani Igunga mkoani Tabora,  Zablon Hussin wanashikiliwa polisi kwa mahojiano wakihusishwa na tukio la jengo la zahanati ya kijiji hicho kuungua moto.

Jengo hilo liliungua moto usiku wa Julai 14, 2018 na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh85 milioni.

Akizungumza na wanahabari leo Jumamosi Julai 21, 2018  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley amesema majina ya watuhumiwa wengine wanaoshikiliwa yanahifadhiwa kuepuka kuharibu upelelezi.

"Wakati moto huo unazuka, zahanati ile haikuwa na mlinzi na tayari tumetoa maelekezo kwa viongozi wa Serikali za mitaani kuhakikisha maeneo yote ya umma yanakuwa na ulinzi," amesema Kamanda Nley.

Kaimu Mganga Mkuu wilaya ya Igunga, Dk Bonaventura Kalumbete amesema moto huo pia umeteketeza dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya Sh25 milioni.

Dk Kalumbete amesema juhudi zinaendelea kutafuta jengo jingine ili litumike kwa ajili ya huduma wakati mchakato wa ukarabati zahanati iliyoungua ukiendelea.
TUNATEST MITAMBO HAI

Leo Jumamosi 21/07/2018 tunatarajia kuanza Mchakato wa Kutafuta vipaji vya Michezo katika Wilaya ya Hai , Mkoani Kilimanjarokwa kuzindua Michuano ya Mpira wa Miguu kwa Kata ya Masama Rundugai itakayoshirikisha Timu nane na moja Timu moja mwalikwa kutoka Wilaya ya jirani ya Simanjiro.

Tunaanza na kata ya Masama Rundugai kama kata ya kufanyia UTAFITI tafiti wa tutakachokwenda kufanya kwa kata zote 17 za jimbo la HAI kwa ajili ya Kujipanga kuanza Michuano ya Mpira wa Miguu Kwa Wilaya ya Hai kabla ya Kumaliza mwaka 2018.

Nawashukuru Wadau wa Michezo Wilaya ya Hai, Marafiki zangu kwa kunipa support ya Baadhi ya Vifaa, na nawashukuru wana Hai kwa kukubali Kuungana Nami katika Safari ya kuwafikia vijana wengi wenye vipaji vya Michezo na sanaa.

Nawatakia Mapumziko Mema ya Wiki, na kribuni tujenge Msingi wa Hatma ya Maendeleo ya Vijana wetu Wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro.

 Jerry Muro

Kheri James Azindua kampeni kwa kishindo Arusha kata zote 77 kuchukuliwa na ccm

Mwenyekiti wa Uvccm Taifa na MCC Ndg. Kheri James Leo amezindua kampeni katika kata ya Daraja Mbili Mkoani Arusha ambapo amesema chama cha Mapinduzi kitashinda kata zote 77 nchini zinazofanya uchaguzi wa marudio.

Akimnadi mgombea wa kata hiyo kwa tiketi ya Ccm Ndg. Prosper Msofe Ndg. kheri james amesema ushindi huu unatokana na muamko wa wananchi juu ya utendaji na kasi ya Rais  John Pombe Magufuli dhidi ya kutatua kero  na matatizo yanayowakabili wananchi.

Miongoni mwa  kero mbalimbali zilizotatuliwa kwa kipindi kifupi ni maji,miundombinu ya barabara  Elimu bure na sasa serikali inaendelea kutatua changamoto ya umeme katika mradi wa Rea  awamu ya tatu sambamba na treni ya umeme.

Akimnadi mgombea huyo amewataka wananchi wa eneo hilo  kumchagua diwani wa kata hiyo kwa kuwa ni Mtendaji na alikuwa akikwamishwa wakati akiwa upinzani kutoka na na chama alichokuwepo kupinga ilani ya CCM.

Ameongeza kuwa kwa sasa itakuwa rahisi kwa yeye kutetea shida za wananchi kutoka na na hakuna wa kumkwamisha.

Kwa upande wake mgombea udiwani Prosper Msofe ameahidi kuendeleza Yale mazuri aliyekuwa akijaribu kuyafanya awali ikiwemo kuhakikisha kina mama na Vijana wanapata mikopo, kero ya ukosefu wa ofisi katika baadhi ya Shule inatatuliwa, Pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya Barabara katika kata hiyo.

Matukio mbalimbali katika picha.
Afisa Habari wa Yanga Dismas Ten akanusha kujihuzulu yanga
Na Magdalena Kashindye
Afisa Habari wa Yanga Dismas Ten amekanusha taarifa zinazosambaa kuwa amejiuzulu nafasi yake.

Ten ambaye alikuwa nje ya ofisi kwa wiki kadhaa kutokana na kuugua maradhi yaliyosababisha akalazwa, amesema yeye bado ni mwajiriwa wa Yanga.

"Bado tupo mapambano yanaendelea "-Ten ameandika kwenye akaunti yake ya instagram

Baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuwa Ten amejiuzulu nafasi yake baada ya kuenea taarifa za kujiuzulu kwa Katibu Mkuu, Charles Mkwassa.

Taarifa hizo zimebainisha kuwa Ten amejiondoa Yanga sababu kuu ikielezwa kukosa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya viongozi wa mabingwa hao wa Kihistoria Tanzania Bara.

Friday, 20 July 2018

Polepole Azindua Kampeni na Kumnadai Mgombea wa CCM Moshi
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amewasihi wakazi wa kata ya Mawenzi mjini Moshi, kumchagua mgombea udiwani wa CCM, Apaikunda Naburi kwa maelezo kuwa atakuwa kiunganishi sahihi kati yao na Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli.

Polepole ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Julai 20, 2018 katika viwanja vya kituo kikuu cha mabasi mjini Moshi, wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata hiyo, ambayo awali diwani wake, Hawa Mushi alikuwa akitokana na Chadema.

Hawa aliyechaguliwa kuwa diwani mwaka 2015 alifariki dunia mwezi uliopita na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo, sambamba na kata zingine 76 nchi nzima.

Polepole amesema maendeleo yanayoonekana katika mji wa Moshi yanatokana na sera nzuri za Serikali ya CCM, ambayo ndio imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa asilimia 80.

Katibu huyo amesema kitakwimu, halmashauri ya manisapaa ya Moshi ina uwezo wa kukusanya mapato ya ndani yanayofikia zaidi ya Sh5 bilioni wakati bajeti kwa mwaka mzima ni Sh46bilioni.

"Hawa wenzetu (Chadema) wanasema wao ndio wameleta haya maendeleo mnayoyaona hapa Moshi. Nataka niwaambie leo, halmashauri mapato yake ni Sh5bilioni kwa mwaka lakini bajeti nzima ni Sh46 bilioni. Mwenye macho haambiwi tazama,"amesema Polepole.

Polepole aliwaomba wakazi wa kata hiyo kumchagua Naburi akisema ndio chaguo sahihi la kuwaletea maendeleo wananchi wa Moshi, ikiwamo kuboresha huduma katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi.

Mbunge wa Siha (CCM), Dk Godwin Mollel amesema ni upotoshaji mkubwa kudai  Rais Magufuli hapendi vyama vya upinzani wakati anaendelea kutoa ruzuku ya kila mwezi kwa Chadema ambacho kinajinasibu kuwa chama kikuu cha upinzani nchini.

Dk Mollel alikuwa mbunge wa Siha kwa tiketi ya Chadema kati ya Novemba 2015 hadi Desemba 2017, kabla ya kujiuzulu na baadae kuteuliwa na CCM kugombea ubunge jimbo hilo hilo na kushinda.

Kwa mujibu wa Dk Mollel, Chadema imekuwa ikipatiwa ruzuku ya Sh337 milioni kwa mwezi kwa fedha za Serikali ya CCM hivyo si sahihi kudai Rais Magufuli hapendi upinzani.

Dk Mollel amedai pamoja na chama hicho kupokea mamilioni hayo ya fedha kwa mwezi, kimeshindwa kuzitumia kwa maendeleo ya chama hicho na ndio maana hadi leo hakina ofisi yake ya kujenga.

Katika mkutano huo, CCM kiliwatumia makada wa zamani wa Chadema waliohamia CCM, kuwashawishi wakazi wa kata ya Mawenzi, kumchagua mgombea wa CCM.
Tanzania na Zambia kutumia kituo kimoja cha forodha mjini Tunduma
Tanzania na Zambia zimekubaliana kutumia kituo kimoja cha forodha kilichojengwa mjini Tunduma.

Lengo na ushirikiano huo ni kupunguza na kudhibiti msongamano wa magari  na uingizwaji wa mizigo kwa njia za magendo.

Makubaliano hayo yamefanyika jana Ijumaa Julai 20, 2018  baina ya naibu kamishna wa forodha  wa mamlaka ya mapato  Tanzania (TRA),  Qamdiyay  Akonaay na kamishina wa forodha  wa mamlaka ya mapato Zambia (ZRA),  Sydney Chibbabbuka  baada ya kukagua miundombinu ya majengo katika mpaka wa  Tunduma na Nakonde.

Akizungumzia na waandishi wa habari mjini Tunduma, Akonaay amesema wamefikia makubaliano hayo  kwa  lengo la kupunguza msongano wa magari na usimamizi wa usafirishaji wa mizigo ili kuongeza mapato  na kuthibiti njia za magendo  za kupitisha bidhaa katika mipaka ya nchi hizo.

"Kituo cha pamoja cha forodha kitaanza kufanya kazi Julai 26 mwaka huu. Wafanyakazi wa ZRA na TRA watafanya kazi katika ofisi moja. Ushirikiano huu utakuwa  chachu ya kukuza uchumi wa mapato  hususani kwa upande wa Tanzania," amesema.

Naye  Chibbabbuka amesema ushirikiano huo utakuwa na faida nyingi katika usafirishaji wa mizigo na kupunguza msongamano uliokuwepo.

Amesema nchini Zamziba tayari wamepata eneo la maegesho ya magari kutoka Tanzania, wanatarajia kuanza ujenzi wa uzio katika eneo hilo mwakani.
Lugola Azungumzia Suti Zake
Baada  ya suti za Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, kuwa gumzo kwenye mitandao mbalimbali, mwenyewe amefunguka na kufafanua juu ya suala hilo.
 
Kwa muda sasa, tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo, Lugola amekuwa akivaa suti zenye bendera ya Tanzania kwenye mifuko hali ambayo imesababisha mijadala kwenye mitandao ya kijamii.

Akizungumza na Michuzi, Lugola alisema anazo suti nyingi za aina hiyo na ni yeye mwenyewe aliyeamua zifanane kwa mwonekano.

Baadhi ya wachangiaji kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakihoji iweje Waziri avae suti moja muda mrefu wakidhani kuwa amekuwa akiirudia.

Lakini mwenyewe jana alijibu na kueleza kuwa suti hizo ambazo ameziita kuwa ni za aina yake, anazo nyingi lakini ameamua zote zifanane.

“Hata ninapobadilisha suti hizi hakuna anayeweza kujua kwa sababu zote zimefanana,” alisema.

Mwonekano wa suti hizo umefanya watu wengine kuzishangaa kutokana na mifuko ya shati kutengenezwa kwa bendera ya taifa.
Waziri Kigwangalla Awataka Wavamizi Maeneo Yaliyohifadhiwa Kuondoka
Na Pamela Mollel,Arusha
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla amewataka wananchi waliovamia maeneo ya hifadhi nchini, kujiandaa kuondoka ndani ya miezi mitatu kabla ya operesheni kuanza.

Akizungumza na waandishi wa habari,Julai 19  katika eneo la  hifadhi ya Jamii ya wanyamapori(WMA) ya makao, wilayani Meatu, Dk Kigwangalla alisema wavamizi wa maeneo ya hifadhi wengi wamekuwa wakijihusisha na matukio ya ujangili.

“Utakula kijiji kina ardhi kubwa, lakini wengine wanajenga hadi katika ndani ya eneo la mita 500 kutoka mpaka wa hifadhi na hao mara nyingi ndio wanaingiza mifugo hifadhini usiku na kufanya ujangili”alisema

Alisema maeneo mengi ya hifadhi na mapori ya akiba nchini yamevamia na wananchi jambo ambalo serikali haiwezi kukubali yaharibiwe ama kutumika kwa ujangili.

Waziri huyo, pia alitembelea kambi ya kitalii ya TGTS na hoteli ya  Mwiba   na kushuhudia vikosi vya kupambana na ujangili katika maeneo hayo ambavyo vipo yapo chini ya taasisi  Friedkin Conservation Fund na kueleza kuridhishwa na uwekezaji wa taasisi hiyo.

Mkurugenzi wa Mwiba Holding, Abdukaril Mohamed, alisema katika eneo la Mwiba wamewekeza sh 2.2 bilion na hivi sasa wanaendelea na shughuli za uhifadhi na utalii.

“Mheshimiwa Waziri katika eneo hili, kampuni yetu inafanya utalii wa picha na kuna hoteli,tunafanyakazi kwa amani na utulivu na vijijini vinavyotuzunguka”alisema

Mwenyekiti wa kijiji cha makao, Anthony Philip, alimweleza Waziri Dk Kigwangalla kuwa, katika eneo hilo kuna mahusiano mazuri baina ya vijiji na wawekezaji na vijiji vinapata mgao wa fedha.

Alisema kijiji cha makao kimekuwa kikipata zaidi ya sh 147 milioni kwa mwaka kutoka kwa mwekezaji na vijiji vingine sita vimekuwa vikipata zaidi ya milioni 80,000 kila mwaka”alisema.

Akiwa katika pori la akiba la Maswa,Meneja wa pori hilo, Lusato Masinde alisema pia wanauhusiano mzuri na wawekezaji ambao licha ya kulipia ada za vitalu pia wamekuwa wakitoa msaada wa huduma mbali mbali ikiwepo maji.

Hata hivyo, alisema katika pori hilo changamoto kubwa ni uvamizi wa mifugo, uchache wa watumishi na upungufu wa vitendea kazi.
Mazishi ya Baba Mkwe Wa Kikwete Yawakutanisha Viongozi MbaliMbali Wa Vyama Tofauti
Viongozi wa ngazi mbalimbali Serikalini , viongozi wastaafu pamoja na mamia ya wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wameshiriki katika mazishi ya mzee Rashid Mkwachu ambaye ni baba yake mzazi Mke wa Rais mstafu Jakaya Kikwete, Mama Salma Kikwete.

Mwili wa mzee Mkwachu umezikwa jana katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

Mzee Mkwachu alifikwa na umauti Julai 19 mwaka huu  na chanzo cha kifo chake kimeelezwa na Msemaji wa familia ya Kikwete,Ridhawani Kikwete kuwa mzee huyo amefariki kutokana na magonjwa ya utu uzima kwani umri wake ulikuwa zaidi ya miaka 100.

Kabla ya mwili kufikishwa makaburi ya Kisuti ibada na dua kumuombea marehemu mzee Mkwachu zilifanyika nyumbani kwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete Msasani jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya viongozi walioshiriki kwenye maziko hayo ni Rais Mstaafu Al haji Ali Hassan Mwinyi,  Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa.

Akizungumza kwenye msiba huo Sheikh Mkuu wa Tanzania Muft Abuubakary Zubeiry amesema maisha ya binadamu ya kuishi kwenye ulimwengu ni mafupi sana na kwa kawaida ni kati ya miaka 63 na ikitoa zaidi ya hapo ni zawadi tu.

Amesema kuwa viumbe vyote ni vinamuda wake wa kuondoa kwenye huu ulimwengu na hakuna ambaye ataishi milele na kufafanua na kufa si kutoweka moja kwa moja bali ni utaratibu wa maisha ya kutoka kwenye ulimwengu na kwenda akhera.

Kwa upande wake Mjuukuu wa Marehemu Mzee Mkwachu ambaye pia ni Msemaji wa Familia Ridhwan Kikwete alieleza kilichokuwa kikimsumbua babu yake ni magonjwa ya utu uzima.

Ametumia nafasi hiyo kuwashukuru woye ambao wamepata nafasi kwa namna moja a nyingine kuungana nao katiki kipindi hiki ambacho cha majonzi wako.
Polepole Aipukutisha CHADEMA Jimbo la Mbowe
Viongozi wote wa Chadema Kata ya Muungano, wakiongozwa na Godliving Emmanuel Kimaro ( Baba Diana) Mwenyekiti wa Kata ya Muungano na Ibrahimu Hamis Mkindi (Mparee) Mwenezi wa Chadema Kata Muungano kutoka Wilaya ya Hai wamejivua uanachama wa Chadema na kujiunga na CCM.

Viongozi hao wamepokelewa na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Taifa Kamaradi Humphrey Polepole kwenye Mkutano wa hadhara Moshi Mjini Kata ya Mawenzi wakati akimnadi Mgombea wa Udiwani wa CCM Kata ya Mawenzi Ndg. Apaikunda Ayo Naburi.