Kamishna msaidizi wa Ardhi mkoa wa Arusha Geofrey Mwamsojo leo, Alhamisi Aprili 25.2024 amemrejeshea kiwanja na kumkabidhi hati mama mjane aliyetambulika kwa jina la Arafa Mohammed mkazi wa...., jijini Arusha ambaye takribani miaka 15 amekuwa akifuatilia haki yake baada ya kudhulumiwa na mtu mmoja aliyemtaja kwa jina la Alex Mtinange naye akiwa ni mkazi wa jijini humo

Akizungumza na wanahabari wakati wa kukabidhi hati hiyo Kamishna Mwamsojo amesema mama huyo ambaye marehemu mume wake alikuwa raia wa kigeni alifikisha malalamiko hayo mbele ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi Jerry Silaa alipoendesha kliniki ya ardhi jijini Arusha hivi karibuni ambapo alieleza kuwa marehemu mume wake alijenga nyumba kwenye kiwanja hicho na walikuwa wakiishi wote kama familia lakini baada ya muda mume wake alianza kuugua, na katika harakati za kupigania uhai wake alimpeleka kumuuguza kwenye nchi mbalimbali huku nyumbani akimuacha binti yake

Hata hivyo baada ya mume wake aliyekuwa raia wa... kufariki, mwaka 2012 mama huyo ambaye kiasili ni mzaliwa wa Tanga alifika kwenye nyumba hiyo lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida alimkuta mtu tofauti akiishi, na alipofuatilia ndipo alipoelezwa kuwa nyumba hiyo kwa sasa inamilikiwa na Alex Mtinange ambaye inatajwa kuwa alikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na binti yake

Inaelezwa kuwa awali wawili hao (binti wa mama huyo mjane na mpenzi wake Alex Mtinange) walikuwa wakiishi wote kwenye nyumba hiyo lakini baadaye waliingia kwenye mgogoro uliopelekea binti huyo kukimbilia nchini Kenya na ndipo Mtinange alipotumia nafasi hiyo kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa serikali ya mtaa kujimilikisha kinyume cha sheria

Jitihada mbalimbali ambazo zilichukuliwa na mama huyo ili kurejesha nyumba yake ziligonga mwamba, hadi hivi karibuni jambo hilo lilipotua kwenye meza ya Waziri Silaa aliyetoa maelekezo kwa Kamishna msaidizi wa Ardhi mkoa wa Arusha kufuatilia na kuhakikisha mama huyo anapata haki yake, jambo ambalo limefanikiwa, ingawa nyumba iliyokuwa imejengwa ilikuwa imebomolewa na hivyo kubaki kiwanja pekee

Akizungumza baada ya kukabidhiwa hati hiyo mama huyo ametoa shukrani kwa serikali kupitia Waziri Silaa na Kamishna Mwamsojo kwa kumpigania kuhakikisha anapata haki yake, hata hivyo ametoa wito kwa viongozi na watendaji mbalimbali wa serikali nchini kuiga mfano wa viongozi hao wa kuhakikisha mara zote wanasimamia haki za wananchi ambao wengi wao wamekuwa wakizihangaikia kwa muda mrefu bila mafanikio 

Katika hatua nyingine Kamishna msaidizi wa Ardhi mkoa wa Arusha Geofrey Mwamsojo amesema atahakikisha anamaliza migogoro yote ya ardhi iliyoko mkoani humo, na kwamba ndani ya siku 90 alizopewa na Mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda kuhakikisha anamaliza migogoro hiyo anaamini atafanikisha, kwa kuwa kinachofanywa na ofisi hiyo kwa sasa si kuzalisha migogoro mipya bali kushughulikia migogoro ya zamani jambo ambalo linaendelea kwa kasi.


Share To:

Post A Comment: