Na Oscar Assenga,TANGA
WAZIRI Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Mizengo Pinda amehimiza viongozi waliopewa dhamana ya mamlaka ya kusimamia mchakato wa uteuzi wa wagombea kuhakikisha wanatenda haki kwa wale wote waliojitokeza kwenye kinyang’anyiro hicho .
Pinda aliyasema hayo leo mara baada ya kutembelea ukarabati wa ofisi ya Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga ambao umefikia asilimia 99 uliofanywa ikiwa ni ndoto za Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo Rajab Abduhaman kuona jengo hilo linakuwa na muonekana mzuri kwa ajili ya kuwahudumia wana CCM.
Akiwa katika eneo hilo mara baada ya kutembelea ukarabati wa jingo hilo aliupongeza uongozi wa CCM kutokana na kazi nzuri walioifanya ya kukarabati jengo hilo na hivyo kuwa na muonekana mpya.
Alisema wakati nchi ikielekea kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu Octoba mwaka huu tayari maandalizi yameshaanza na waliochukua fomu Udiwani na Ubunge wameshafanya na kazi ya chama ni kuhimiza viongozi waliopewa dhamana ya mamlaka ya kusimamia mchakato watende haki.
“ Bahati nzuri kamati yenu mlisimamie kikamilifu ili mtu asipate sababu ya kupiga kelele wakati hakuna sababu ya kufanya hivyo kwa wananchi tunaomba wakati wa kupiga kura tumieni haki yenu tena kwa uhuru wenu wenyewe”Alisema
Aidha alisema pia kupitia utaratibu uliowekwa kabla ya kutoka kwenda kupambana na vyama vyengine lazima wampate mgombea wa chama atakayekwenda kupambana na vyama vyengine vya siasa tumieni haki yenu vizuri mtupe mgombea ambaye mnaamini anaweza kutuvusha kwa haraka zaidi.
Hata hivyo Waziri Mkuu Mstaafu Pinda alisema kwamba wanaendelea kumshukuru Rais Dkt Samia Suluhu na kumpongeza kwa kazi nzuri anayoifanya nchi ipo kwenye utulivu na amani na mambo yanasonga mbele.
“Tanga kuna maneno nimesikia Rais hana deni na sisi na octoba tunatiki niombeni wana Tanga na wana CCM hilo jambo lipo mbele yenu na Tanga mlikuwa wapambanaji sana lazima jitihada kuhakikisha mnaongoza kwenye kura za Rais na Ubunge kwenye chaguzi zijazo”Alisema
Pinda aliwataka viongozi wa mkoa huo kuendelea kuchapa kazi pamoja na mshikamano kwa kuhakikisha wanaendelea kudumisha amani na ulitulivu ambao wanao mpaka sasa kutokana na kwamba haukudondoka tu angani bali umejengwa hivyo waendelee kumuomba mwenyezi Mungu aendelee kuisimamia.
Awali akizungumza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Rajabu Abdurhaman amesema ukarabati wa ofisi hiyo ni maelekezo ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho Dkt Samia Suluhu kuhakikisha mali za chama yakiwemo majengo ya chama ya ofisi na menginevyo wanayalinda na kuyafanyia ukarabati mkubwa ili yaendelee kutumika miaka mingi kadri inavyowezekana.
Aidha alisema kwamba alifanya ziara kwenye mkoa wa Tanga na katikati pita pita yake aliona jengo lao namna lilivyokuwa na kutoa maelekezo kuhakikisha jengo hilo linafanyiwa ukarabati mkubwa na hayo ni matunda ya Mwenyekiti wa Taifa na maelekeo yake.
“Tulipopata maelekezo hayo tukasema lazima tufanye kwa sababu haki na heshima ya CCM kwenye nchi na mkoa wa Tanga ni kubwa haiwezekani viongozi wa CCM wanaovyoonekana uzuri lakini mahali wanapofanyia kazi hapafanani na nasi tukasema hapana lazima watii maelekezo hayo na tunashukuru wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa na Kamisaa wao kwa umoja na mshikamano wao ndio umewezesha kutekeleza maelekezo hayo ya Rais”Alisema
Naye kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi ,Dkt Batilda Burian amesema wa wamefarijika uwepo wa Waziri Mkuu huyo na wanamshukru Mwenyekiti Taifa kwa kazi kubwa aliyoifanya wakati wa ziara yake na wana Tanga wanaendelea kumshukuru kwa mambo mengi makubwa ya kimaendeleo aliyofanya kwa mkoa huo.
“Kutokanana na hilo tunasema kwamba Mama Hana deni na Octoba tunatiki na kura zitajaa na kumwagika kutokana na kasi kubwa ya maendeleo aliyoyafanya katika mkoa wa Tanga na hivyo kuufungua kiuchumi”Alisema
Hata hivyo,Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga Mfaume Kizigo alisema chama hicho kimepata kiongozi wa kwelikweli na kinachoonekana hapo ni sehemu ya maendeleo makubwa yaliyofanywa na Mwenyekiti huyo kutokana na kila wilaya amejenga byumba za watumishi kuanzia chama na Jumuiya zake zote na amefanya hivyo kila alipokwenda kuishauri kamati ya siasa.
Mwisho.