Katika mwendelezo wa kampeni ya kitaifa ya TUWAAMBIE KABLA HAWAJAHARIBIWA, Sajenti Emmanuel kutoka Jeshi la Polisi, kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto, ametembelea Shule ya Sekondari Robanda iliyopo Kijiji cha Robanda, Kata ya Ikoma, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, na kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na wanafunzi wa kidato cha tano.
Akiwa shuleni hapo, Sajenti Emmanuel amewahimiza wanafunzi hao kujitambua na kuelekeza nguvu zao katika masomo ili kufikia malengo yao ya kitaaluma na maisha kwa ujumla, amesisitiza umuhimu wa kuepuka mahusiano ya kimapenzi wakiwa bado shuleni, akieleza kuwa vitendo hivyo vimekuwa chanzo kikuu cha kukatisha ndoto za wanafunzi wengi nchini.
Aidha, amewataka wanafunzi kuwa mstari wa mbele katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kutoa taarifa mapema kwa mamlaka husika, amebainisha kuwa taarifa zinaweza kutolewa katika ofisi ya Dawati la Jinsia na Watoto iliyo katika kituo cha polisi, kwa Afisa wa Ustawi wa Jamii, au kwa viongozi wa serikali ya kijiji na kata.
Kampeni hiyo inalenga kuwafikia vijana walioko mashuleni na katika jamii kwa ujumla, ikiwa ni jitihada za pamoja kati ya serikali, vyombo vya dola, na wadau wa maendeleo katika kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia na kusaidia vijana kufikia ndoto zao kwa usalama.
Post A Comment: