Articles by "ARDHI"
Showing posts with label ARDHI. Show all posts


Na Munir Shemweta 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Lucy Kabyemera, ameahidi kuwa Wizara yake itayafanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wadau wa sekta ya ardhi, huku akiwataka kuimarisha ushirikiano na kuachana na tabia ya kunyoosheana vidole.

Bi. Kabyemera ametoa ahadi hiyo Novemba 24, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akifunga kikao kazi kati ya Wizara ya Ardhi na kampuni zinazojihusisha na mipango miji, upimaji wa ardhi na uendelezaji wa milki.

Amesema, Wizara ya Ardhi natambua mchango mkubwa wa wadau hao katika maendeleo ya sekta ya ardhi na makazi, hivyo itaendelea kushirikiana nao katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazokabili sekta hiyo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Ameeleza kuwa, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeipa sekta ya ardhi nafasi muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo ni muhimu kwa Serikali na wadau kuunganisha nguvu katika kuhakikisha utekelezaji wake unafanikiwa.

Bi. Kabyemera amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ipo tayari kuunga mkono juhudi za wadau katika kuendeleza sekta hiyo.

“Malengo ya Rais ni kuhakikisha vikwazo katika maeneo mbalimbali, ikiwemo sekta ya ardhi, vinaondolewa ili kuwezesha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kufanyika kwa ufanisi,” amesema.

Amehakikishia washiriki wa kikao kazi hicho kuwa, maoni na mapendekezo yote yaliyowasilishwa yatafanyiwa kazi kwa kina, akibainisha kuwa Wizara inazifahamu changamoto zinazokabili sekta hiyo na tayari imeanza kuzishughulikia.

“Tutafanyia kazi maoni ya wadau mpaka mwisho na tayari tumeanza kuzifanyia kazi baadhi ya changamoto mbalimbali na tunazifahamu,” amesema.

Aidha, amesema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa katika kuboresha usimamizi wa sekta ya ardhi ni kurejeshwa kwa watumishi wa sekta hiyo chini ya Wizara, hatua ambayo amesema imeonesha matokeo chanya katika usimamizi na maendeleo ya sekta hiyo.

Hata hivyo, amewataka wadau kuachana na tabia ya kunyoosheana vidole na badala yake kujenga utamaduni wa kushirikiana katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Amesema, kulaumiana hakusaidii kutatua changamoto zilizopo, bali kunatoa taswira isiyofaa kwa sekta hiyo, hivyo ni muhimu kwa Wizara na wadau kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuimarisha huduma na kuendeleza sekta ya ardhi nchini.

Amesisitiza kuwa, ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuhakikisha sekta ya ardhi inachangia ipasavyo maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania.

Kikao hicho cha siku mbili kimewakutanisha wataalamu na kutoka kampuni za Mipangomiji, upangaji, upimani pamoja na wale wa uendelezaji milki.

 




WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Leonardo Akwilapo, amesema sekta binafsi ni nguzo muhimu katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika usimamizi wa ardhi, uendelezaji wa miji ya kisasa, makazi bora na ukuaji wa uchumi.

Akizungumza Novemba 11, 2026, jijini Dar es Salaam, katika kikao kazi na kampuni za upangaji, upimaji na uendelezaji wa milki, Waziri huyo amesema ardhi ni rasilimali muhimu inayobeba shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo, viwanda, ujenzi wa nyumba, ofisi na uwekezaji wa biashara.

Amesema Dira ya Taifa ya 2050 imeipa sekta ya ardhi nafasi muhimu kutokana na uwezo wake wa kuchochea maendeleo ya wananchi na kufikia malengo ya uchumi, hivyo ni lazima kuweka mifumo imara ya usimamizi na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi.

Waziri amesema serikali haiwezi kutekeleza Dira ya 2050 peke yake, kwa kuwa sekta binafsi imepewa nafasi kubwa katika kuchochea shughuli za kiuchumi, hivyo ni muhimu kushirikiana katika ubunifu wa miji ya kisasa, ujenzi wa makazi ya gharama nafuu, kuboresha makazi yaliyopo na kuimarisha usalama wa milki.

Amesema ushirikiano huo unapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kitaaluma, huku akisisitiza kuwa serikali na sekta binafsi ni washirika wanaojenga nyumba moja na wanapaswa kuzungumza kwa uwazi, kukosoana na kutatua changamoto kwa lengo la kuleta maendeleo.

Katika hatua nyingine, Waziri amesema serikali ipo katika maandalizi ya kuanzisha Mamlaka ya kusimamia sekta ya milki nchini, ambayo itakuwa na nguvu za kisheria za kuratibu na kusimamia shughuli za sekta hiyo, akieleza kuwa muswada wake unatarajiwa kuwasilishwa Bungeni katika nusu ya pili ya mwaka 2027 baada ya kukamilisha hatua za mashauriano na wadau.

Amesema kuanzishwa kwa mamlaka hiyo kutasaidia kuimarisha usimamizi wa sekta ya milki, kudhibiti ukiukwaji wa maadili ya kitaaluma, udanganyifu na migogoro ya ardhi, pamoja na kuweka mfumo wa pamoja wa utendaji kwa wadau wanaohusika.

Aidha, amesema serikali inaendelea na programu ya urasimishaji wa makazi yaliyopangwa kiholela na kuzuia uanzishwaji wa makazi mapya yasiyozingatia mipango miji, akibainisha kuwa changamoto ya makazi yasiyopangwa imeendelea kuathiri mandhari ya miji, upatikanaji wa huduma na maendeleo endelevu.

Waziri ametoa rai kwa sekta binafsi kushirikiana na serikali katika kuboresha makazi chakavu na kuhuisha maeneo ya mijini yenye thamani kubwa, bila kuathiri haki za wananchi katika maeneo yao, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia mipango miji na matumizi sahihi ya ardhi.

Ameongeza kuwa serikali pia inafuatilia changamoto za ukusanyaji wa kodi ya pango la ardhi, baada ya kubainika kuwa baadhi ya wananchi wanaotaka kulipa wanakabiliwa na vikwazo vya kupata namba za malipo, akielekeza uchunguzi kubaini kama tatizo linatokana na mifumo ya kiteknolojia, watendaji au sababu nyingine.

Waziri amesema sekta ya milki ina mchango wa takribani asilimia 4.4 katika Pato la Taifa, hivyo kuna haja ya kuimarisha usimamizi wake ili kuongeza mapato ya serikali, kuvutia uwekezaji na kukuza uchumi, huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na mazingira bora ya kufanya kazi.

Pia amesema kwamba Serikali inathamini mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya ardhi, milki na makazi nchini, na kwamba ushirikiano wa karibu, uwazi, uwajibikaji na kuzingatia taaluma ni muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa.

 



SERIKALI ya Tanzania imeunga mkono maazimio sita ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), yanayolenga kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maafa katika ukanda huo, hususan kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.

Msimamo huo umetolewa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.Kaspar Mmuya, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi ambapo aliwasilisha msimamo wa Tanzania katika Mkutano wa Saba wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya Usimamizi wa Maafa katika nchi wanachama wa SADC, uliofanyika kwa njia ya mtandao Leo, Novemba 12, 2026, jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Mmuya amesema Tanzania inatambua na kupongeza jitihada zinazofanywa na nchi wanachama pamoja na Sekretarieti ya SADC katika kujiandaa kukabiliana na maafa yanayoweza kujitokeza kutokana na El Niño, ikiwemo kuandaa mipango ya dharura ya kitaifa na kikanda kwa lengo la kupunguza madhara.

Amesema jitihada hizo ni pamoja na kuratibu mazoezi ya utayari wa kukabiliana na vimbunga na mafuriko kupitia Timu ya Kikanda ya Utayari wa Kukabiliana na Dharura, yaliyofanyika Nacala, Msumbiji, pamoja na maandalizi ya taarifa ya kikanda kuhusu hali ya usalama wa chakula na lishe kwa mwaka 2026.

“Tanzania inaunga mkono na kuridhia maazimio yote kuanzia Uamuzi Na. 1 hadi Na. 6 kama yalivyopendekezwa na Sekretarieti,” amesema.

Ameongeza kuwa Sekretarieti imeendelea kuratibu usambazaji wa taarifa za utabiri wa hali ya hewa na tahadhari za mapema, kuandaa mkakati wa kikanda wa kuhifadhi vifaa vya akiba kwa ajili ya misaada ya kibinadamu na mwongozo wa utekelezaji wa hatua za mapema za kupunguza athari za vihatarishi mbalimbali kwa kipindi cha mwaka 2026 hadi 2030.

Akisisitiza maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele, Mmuya amesema ni muhimu nchi wanachama kuimarisha usalama wa chakula na lishe kwa kuhakikisha taarifa zinazohusu eneo hilo zinaandaliwa na kuwasilishwa kwa wakati.

Amesema upatikanaji wa chakula cha kutosha, salama na chenye virutubisho muhimu ni sehemu muhimu ya usimamizi wa maafa kwa kuwa unasaidia kulinda maisha ya wananchi, kupunguza athari za majanga na kuimarisha ustahimilivu wa jamii.

"Sekretarieti ya SADC kushirikiana na washirika wa maendeleo kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali fedha na utaalamu utakaowezesha kuimarisha utayari wa kikanda, kutekeleza hatua za mapema na kutoa misaada ya kibinadamu kwa haraka wakati wa maafa,"amesema

Pia, amesisitiza umuhimu wa utaratibu wa kikanda wa kuhifadhi vifaa vya dharura kuzingatia vihatarishi vya majanga, haki na usawa, uendelevu wa kifedha, uwazi na kuimarisha mifumo ya kitaifa iliyopo.

Kwa upande mwingine, Mmuya ameipongeza Sekretarieti ya SADC kwa kuendelea kutekeleza ajenda ya kuimarisha Kituo cha Huduma za Kibinadamu na Operesheni za Dharura (SHOC), ikiwemo kuimarisha timu ya utayari wa kukabiliana na dharura kupitia mafunzo, mazoezi na upatikanaji wa vifaa.

Amesema hatua hizo ni muhimu katika kuimarisha uwezo wa nchi wanachama kukabiliana na maafa, kupunguza madhara kwa wananchi na kulinda maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika ukanda wa SADC. 


Na Munir Shemweta, WANMM

Tanzania inatarajiwa kuwa na miji ya kisasa, yenye makazi bora na nafuu, miundombinu imara, huduma za kijamii zinazopatikana kwa urahisi pamoja na mazingira salama na rafiki kwa wananchi.

Hayo ni miongoni mwa matarajio yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo mwaka 2050, inayolenga kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia upangaji na maendeleo endelevu ya miji.

Hayo yamebainishwa Novemba 8, 2026 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Deogratias Kalimenze wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mipangomiji Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka Novemba 8 na mwaka huu siku hiyo inatimiza miaka 77 ya Mipangomiji Duniani.

Amesema, Dira ya Tiafa ya Maendeleo 2050 inaweka msisitizo katika kujenga miji janja (Smart Cities), itakayotumia teknolojia kurahisisha utoaji huduma, kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi na kuboresha usimamizi wa rasilimali za mijini.

Kwa mujibu wa Bw. Kalimenze, Tanzania ya 2050 inatarajiwa kuwa na miji yenye makazi bora na yanayomudu gharama za wananchi, maeneo ya kijani yanayolinda mazingira, mifumo bora ya usafiri na usafirishaji pamoja na makazi jumuishi na salama yanayozingatia mahitaji ya makundi yote ya jamii.

Ameeleza kuwa, katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Serikali pia inalenga kujenga miji inayostahimili majanga ya kimazingira, ikiwemo mafuriko na changamoto nyingine zinazoweza kuathiri maisha na shughuli za wananchi.

Akielezea hatua zinazochukuliwa kuelekea mwaka 2050 amesema, Ili kufanikisha maono hayo, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu na huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, shule, masoko, maeneo ya maegesho na majosho.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa Idara ya Maendeleo ya Makazi Wizaya ya Ardhi, hatua nyingine ni kuweka sera zinazowezesha sekta binafsi kushiriki ujenzi wa nyumba, pamoja na kuimarisha upangaji na upimaji wa ardhi ili kuongeza upatikanaji wa viwanja vilivyopangwa na kupatiwa huduma muhimu.

Vilevile, ameweka wazi kuwa, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanaendelea kuboreshwa katika sekta mbalimbali za Serikali kwa lengo la kurahisisha upatikanaji huduma kwa wananchi na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa miji.

Hata hivyo, Bw. Kalimenze amesema pamoja na jitihada hizo, ukuaji wa makazi yasiyopangwa bado ni changamoto inayokabili miji mingi nchini.

Pia, uhaba wa viwanja vilivyopimwa na kupatiwa huduma muhimu unachangia wananchi kutafuta maeneo ambayo taratibu za upatikanaji wa ardhi ni rahisi zaidi, hata kama hayajapangwa.

Ameitaja sababu nyingine kuwa ni baadhi ya wananchi kuendeleza maeneo bila kufuata taratibu za kisheria, ikiwemo kujenga bila vibali vya uendelezaji ardhi na vibali vya ujenzi.

Bw. Kalimenze amesema, hali hiyo inaonesha kuwa kufikia miji inayotarajiwa mwaka 2050 hakutategemea mipango iliyowekwa pekee, bali pia utekelezaji wake, usimamizi wa matumizi ya ardhi na ushiriki wa wananchi katika kufuata taratibu za mipango miji.

Akizungumzia kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mipangomiji Duniani, amesema kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo yam waka 2050 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Awamu ya Nne wa mwaka 2026/2027 hadi 2030/2031 serikali itaendelea kuweka mikakati ya kuboresha sekta mbalimbali nchini.

Katika maadhimisho hayo, Wataalamu wa Mipangomiji wametakiwa kuendelea kuzingatia misingi ya taaluma yao katika usanifu na uendelezaji wa miji ili kuhakikisha ukuaji wa makazi unazingatia mipango iliyopo na mahitaji ya wananchi.

Kwa ujumla, sura ya Tanzania ya mwaka 2050 itategemea namna maono ya kuwa na miji janja, salama, jumuishi na endelevu yatakavyotekelezwa kuanzia sasa.

 


Na Munir Shemweta, WANMM KASULU

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, ameendelea na ukaguzi wa maeneo ya uwekezaji ambapo ametembelea eneo la mradi wa kilimo cha miwa na uzalishaji sukari la Kasulu Sugar, wilayani Kasulu mkoani Kigoma na kusisitiza umuhimu wa ardhi iliyotolewa kwa uwekezaji kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa. 

Amesema, Serikali inataka kuona maeneo yote yaliyotolewa kwa wawekezaji yakiendelezwa na kuleta tija kwa mujibu wa makubaliano na mipango iliyowekwa.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ndiyo mwenye dhamana ya kuunda Kamati ya Kitaifa ya Kugawa Ardhi ya uwekezaji ambapo mbali na jukumu hilo pia kamati inamshauri Kamishna wa Ardhi katika kushughulikia maombi ya umilikishaji ardhi.

Dkt. Akwilapo amefanya ziara hiyo mwishoni mwa wiki katika eneo la mradi huo linalomilikiwa na kampuni ya Mufindi Papers Mills Co. Limited, maarufu kama Kasulu Sugar, lenye ukubwa wa hekta 37,662. 

Katika ziara hiyo, Dkt Akwilapo alijionea shughuli za uwekezaji zinazofanyika na kutoa msisitizo kwa uongozi wa kampuni kuhakikisha ardhi hiyo inaendelezwa na kutumika kwa shughuli za kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari.

"Wizara haitarajii kuona ardhi inayotolewa kwa ajili ya uwekezaji ikiendelea kubaki bila kuendelezwa".amesema Mhe Dkt Akwilapo.

Ameupongeza uongozi wa Kasulu Sugar kwa uwekezaji uliofanyika na kuutaka kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili uweze kuchangia uzalishaji wa sukari nchini. 

"Kuendelezwa kwa eneo hili kutasaidia kuongeza uzalishaji miwa na sukari, kupanua upatikanaji wa bidhaa hiyo sokoni na kuwa na mchango katika kupunguza changamoto ya bei ya sukari nchini". Ameeleza.

Ziara hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii iliyotaka maeneo yaliyotolewa kwa shughuli za uwekezaji kukaguliwa kwa lengo la kubaini maeneo yasiyoendelezwa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Mufindi Papers Mills Co. Limited Bw. Satya Narayana amemueleza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa, mradi unaotekelezwa na kampuni yake unatumia teknolojia ya hali ya juu na ya kisasa katika uzalishaji sukari. 

"Mradi wa kilimo cha miwa na uzalishaji sukari katika kiwanda hiki unagharimu dola 320 milioni na unatarajia kuchangia uchumi wa Tanzania na jamii kwa ujumla". Amesma.

Eneo la mradi wa Kasulu Sugar wilayani Kasulu mkoa wa Kigoma linahusisha vijiji saba vya Nyarugusu, Kiyungwe, Kitanga, Kamtundu, Nyamidaho, Kigadye na Heru Ushingo, vilivyotoa ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa mradi huo.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaendelea na jitihada za kufuatilia matumizi ya ardhi kwenye maeneo ya uwekezaji kwa lengo la kuhakikisha rasilimali hiyo inatumika kwa tija, kwa kuzingatia mipango ya matumizi ya ardhi na masharti yaliyowekwa. 

Hatua hiyo inalenga kuimarisha usimamizi wa ardhi, kuhakikisha wawekezaji wanatimiza wajibu wao na kuongeza mchango wa uwekezaji katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananch

 


Na Munir Shemweta, WANMM KOROGWE

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo amezindua rasmi mpango wa kupanga, kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) katika eneo la Shamba la Mwakinyumbi lililopo Kata ya Hale, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga huku akiwataka wananchi wanaoishi eneo hilo kushirikiana na wataalamu ili zoezi hilo likamilike ndani ya muda uliopangwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo katika uwanja wa Mwenge, Hale Korogwe leo Sept 21, 2026 mkoani Tanga Mhe. Dkt Akwilapo amesema, hatua hiyo inalenga kuwatambua wananchi wanaostahili, kupangiwa na kupimiwa ardhi hiyo, na hatimaye kuwamilikisha viwanja vilivyopimwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria.

Mpango wa uendelezaji wa ardhi katika eneo hilo unahusisha ekari 5000 zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kilimo, makazi na huduma za jamii, miundombinu, ardhi ya akiba, ardhi ya uwekezaji na uchimbaji madini, hifadhi ya mlima na hifadhi ya vyanzo vya maji. Aidha ekari 4,220 zimetengwa kwa vijiji vya Mwanyumbi Station na Miembeni na kufanya jumla ya ekari 9220 kuwa katika mpango huo wa uendelezajI.

Aidha, Dkt Akwilapo aliweka wazi kuwa, kabla ya kuanza kwa zoezi hilo la upangaji na upimaji, wananchi watapatiwa elimu kuhusu taratibu zitakazotumika, vigezo vya utambuzi, ukubwa wa maeneo watakayopangiwa pamoja na masuala mengine ya kisheria na kitaalamu.

" Niwaombe wananchi wa Mwakinyumbi kushiriki kikamilifu katika hatua hiyo ili kupata ufafanuzi na kuelewa namna zoezi litakavyotekelezwa". Amesema

Mbunge wa jimbo la Korogwe Vijijini Mhe. Timotheo Mzava amemuomba Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhakikisha wananchi Mwakinyumbi katika kata ya Hale Korogwe wanapewa kipaumbele kwa kuwapatia viwanja kwa gharama nafuu.

Aidha, ametaka pasiwe na utaratibu wa kuwaondoa wanachi walioingia katika shamba la Mwakinyumbi na kufanya maendelezo kwa kuwa tayari wamefanya uwekezaji mkubwa.

" Pasiwe na utaratibu wa kuwaondoa wananchi wa Mwakinyumbi walifanya maendelezo na badala yake warasimishiwe maeneo yao kwa utaratibu ili waendelee kuishi". Amesema Mhe Mzava

Mkuu wa wilaya ya Korogwe kwa upande wake amesema kila mtu ahakikishe anajaza fomu kulingana na maelekezo wasifanye magumashi ili kila mtu apate haki yake.

Eneo la mradi lilikuwa likimilikiwa na Kampuni ya M/S Mwakinyumbi iliyopewa ardhi hiyo mwaka 1989 kwa ajili ya uwekezaji katika kilimo cha mkonge. Hata hivyo, kampuni hiyo ilishindwa kutekeleza masharti ya umilikishwaji, ikiwemo kuliendeleza eneo hilo, hali iliyosababisha milki hiyo kubatilishwa mwaka 2023 na ardhi kurejea serikalini.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo amewaonya wananchi dhidi ya kuendelea kuuza au kununua ardhi kiholela katika eneo la Shamba la Mwakinyumbi wakati zoezi la upangaji na upimaji likiendelea.

Dkt Akwilapo amewataka wananchi wa eneo hilo kutoendeleza uvamizi wa ardhi au kufanya mauziano yasiyo rasmi, huku akianisha kuwa serikali tayari imeanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya baadhi ya watu wanaodaiwa kuuza ardhi kwa njia za ulaghai.



Na Munir Shemweta, WANMM

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amewaagiza Makamishna wa Ardhi Wasaidizi katika mikoa yote nchini kufanya ukaguzi wa maeneo ya uwekezaji yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali kwa lengo la kubaini maeneo yasiyoendelezwa na kutoa taarifa ili hatua stahiki zichukuliwe

Dkt. Akwilapo ametoa agizo hilo Septemba 18, 2026, mara baada ya kuhitimisha ziara yake katika maeneo ya uwekezaji ya Kongani ya Viwanda ya KAMAKA pamoja na kiwanda cha Nondo cha Gain Company Limited kilichopo Mlandizi, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.

Amesema Wizara ya Ardhi, imebaini kuwepo kwa maeneo ambayo yalipewa wawekezaji kwa ahadi ya kuanzisha viwanda au shughuli nyingine za uzalishaji, lakini hayajaendelezwa kwa muda uliokubaliwa.

“Tuna taarifa kuna waliochukua maeneo wakasema watatengeneza viwanda lakini bado hawajafanya hivyo. Natoa maelekezo makamishna kufanya ukaguzi na kuwasilisha taarifa ili hatua stahiki zichukuliwe kwa maeneo yasiyoendelezwa kadri ya mikataba waliyoingia,” amesema Dkt. Akwilapo.

Aidha, Waziri huyo amewataka wamiliki wote wa ardhi ambao hawazingatii masharti ya uendelezaji maeneo waliyopewa kuhakikisha wanayaendeleza kwa wakati, vinginevyo wizara itachukua hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

Amesisitiza kuwa, hatua hizo zitawahusu wawekezaji wazawa na wa kigeni, akieleza kuwa kwa wawekezaji wazawa hatua inaweza kujumuisha kubadilisha milki za ardhi walizopewa, huku kwa wawekezaji wa kigeni wizara ikishirikiana na taasisi husika, ikiwemo TISEZA, katika kushughulikia masuala ya umiliki na uwekezaji.

Dkt. Akwilapo amesema, hatua hiyo inalenga pia kujibu malalamiko kutoka kwa wananchi ambao maeneo yao yalichukuliwa kwa ajili ya uwekezaji, lakini baadaye hayakuendelezwa.

Ameeleza kuwa, hali hiyo imekuwa ikisababisha wananchi kuhoji sababu za maeneo kutolewa kwa wawekezaji ambao hawajaanza shughuli za maendeleo kwa muda mrefu.

Awali Mhe Dkt Akwilapo alielezwa kuwa eneo la Kongani ya Viwanda Mlandizi wilayani Kibaha mkoa wa Pwani linakabiliwa na changamoto kadhaa kama vile upatikanaji wa maji na ubovu wa barabara hali waliyoieleza kuwa inayosababisha kero katika usafirishaji bidhaa na malighafi.

Hata hivyo, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) wameeleza kuanza  kuchukua hatua za dharura kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi wa muda mfupi na mrefu

Ziara ya Dkt. Akwilapo katika Mkoa wa Pwani imelenga kujionea kwa karibu shughuli za uwekezaji na matumizi ya ardhi katika maeneo hayo, pamoja na kutathmini namna bora ya kuendeleza maeneo ya uwekezaji kwa kuzingatia mipango ya matumizi ya ardhi na maendeleo endelevu.

Aidha, ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi za kutambua fursa na changamoto zinazohusiana na ardhi na uwekezaji, kwa lengo la kuimarisha matumizi bora ya ardhi, kuvutia uwekezaji na kuchochea maendeleo ya wananchi





Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amewaonya wananchi wanaovamia maeneo kwa nguvu na kuunda vikosi vya ulinzi kwa ajili ya kulinda maeneo hayo, akisema Serikali haitavumilia vitendo hivyo na kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa.

Dkt. Akwilapo ametoa onyo hilo leo Sept 17, 2026 wakati akizungumza na wananchi katika Kliniki ya Ardhi iliyofanyika Kata ya Zingiziwa, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Amesema, wananchi hawapaswi kujichukulia sheria mkononi kwa kuvamia maeneo yanayomilikiwa na watu wengine na kuanzisha vikosi vya ulinzi kwa lengo la kuyadhibiti kwa nguvu.

“Serikali haitavumilia vitendo vya watu kujichukulia sheria kwa kuvamia maeneo ya wananchi wengine na kuunda vikosi vya ulinzi kwa lengo la kulinda maeneo hayo kwa nguvu,” amesema Dkt. Akwilapo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Bw. Elihuruma Mabelya, amesema hadi sasa jumla ya hati miliki 545 zimetolewa kwa wananchi kupitia Kliniki hiyo ya Ardhi.

Mabelya ameeleza kuwa, timu ya wataalamu itaendelea kuwepo katika eneo hilo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za ardhi kwa urahisi na kwa wakati, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Wizara.

Baadhi ya wananchi, kupitia Diwani wa Kata hiyo, wameipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kusogeza huduma za ardhi karibu na maeneo yao.

Wameielezea hatua hiyo kuwa  imewapunguzia adha ya kusafiri umbali mrefu pamoja na gharama kubwa walizokuwa wakitumia ili kufuata huduma hizo



 


Na Munir Shemweta, MOROGORO

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mzava, ameitaka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuongeza nguvu katika kuboresha na kupanua Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) ili kuongeza uwezo wa kuzalisha wataalamu wengi zaidi katika sekta ya ardhi.

Aidha, Mhe. Mzava ameitaka Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Upangaji) katika kuweka utaratibu wa kutumia wataalamu wanaozalishwa na vyuo vya ardhi kusaidia wananchi kutatua changamoto za ardhi na hivyo kupunguza migogoro inayojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini.

Mhe. Mzava ametoa kauli hiyo, Agosti 30, 2026, wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii katika Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO), mkoani Morogoro.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Mzava amekipongeza Chuo cha Ardhi Morogoro kwa kazi kinayoifanya ya kuwaandaa vijana kitaaluma licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali.

“Nikipongeze Chuo cha Ardhi Morogoro. Pamoja na changamoto zake, kinafanya kazi nzuri ya kuwaandaa vijana ili watumikie Taifa lao.”

Amesema, chuo hicho ni taasisi muhimu katika uzalishaji wa wataalamu wa sekta ya ardhi na kwamba ni muhimu kuendelea kuboresha mipango yake ya maendeleo, ikiwemo kutekeleza mpango kabambe wa chuo.

Amebainisha kuwa, anatamani kuona mabadiliko makubwa katika vyuo vya Ardhi vya Morogoro na Tabora, ikiwa ni pamoja na kuboreshwa kwa miundombinu, mazingira ya kujifunzia na uwezo wa vyuo hivyo kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko.

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa kutembelea Chuo cha ARIMO na kujionea shughuli zinazofanyika katika chuo hicho.

Waziri Akwilapo ameihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge kuwa Wizara yake itakiangalia kwa karibu Chuo cha Ardhi Morogoro ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kusomea na kujifunzia.

Nao wajumbe wa Kamati wamekipongeza Chuo cha Ardhi Morogoro na Wizara kwa ujumla kwa kazi nzuri inayofanyika katika kuendeleza elimu ya ardhi nchini.

Hata hivyo, wamependekeza chuo kuangalia uwezekano wa kuongeza na kuanzisha kozi mbalimbali tofauti na zile zinazotolewa kwa sasa, ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kuongeza fursa kwa vijana.

Wajumbe hao pia wamekishauri chuo kuanza mapema kutafuta maeneo ya ardhi kwa ajili ya upanuzi wa shughuli zake katika miaka ijayo, wakieleza kuwa si jambo baya kwa chuo kutafuta eneo katika mikoa mingine, ikiwemo Iringa, kwa ajili ya shughuli za kitaaluma na maendeleo ya chuo.

Vile vile wamesisitiza umuhimu wa upatikanaji wa vifaa vya kisasa kwa lengo la kusaidia wanafunzi kupata mafunzo yanayozingatia teknolojia za kisasa na kuwawezesha kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Katika ziara yake ya siku moja katika Chuo cha Ardhi Morogoro Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ilipata taarifa maendeleo ya chuo Pamoja na kukagua mradi wa ujenzi wa madarasa Pamoja mpango wa uendelezaji chuo katika eneo la Mlimakola mkoani Morogoro.

 


Na Munir Shemweta, Tanga

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amesema Wizara yake iko tayari kutoa hati miliki za ardhi kwa maeneo yatakayotumika katika shughuli za utafiti, elimu ya ujuzi na ubunifu nchini.

Dkt. Akwilapo ameyasema hayo leo, Agosti 18, 2026, wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu kwa mwaka 2026, inayoendelea viwanja vya Usagara jijini Tanga.

Amesema, Wizara ya Ardhi iko tayari kushirikiana na taasisi za elimu na utafiti kwa kuhakikisha maeneo yanayotumika katika shughuli hizo yanapatiwa hati miliki ili kuwezesha utekelezaji wa tafiti na ubunifu kwa ufanisi.

“Nichukue fursa hii kuipongeza Wizara ya Elimu, sambamba na kuwashukuru wahadhiri na wakufunzi wote kwa kazi nzuri ya kuandaa vijana katika kazi za ujuzi na ubunifu. Wizara yangu iko tayari kutoa hati miliki katika maeneo ya utafiti,” amesema Dkt. Akwilapo.

Akizungumzia Maonesho ya wiki ya kitaifa ya elimu, ujuzi na ubunifu nchini, Dkt. Akwilapo amepongeza kazi inayofanywa na taasisi za elimu, akisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia na ubunifu.

“Nipongeze ubunifu pamoja na maonesho. Kwa kweli yamefana sana, na ubunifu mliouonesha ni wa hali ya juu. Nawapongeza kwa yote mnayoyafanya katika taasisi zenu,” amesema.

Dkt. Akwilapo, ambaye aliwahi kuwa katika Wizara ya Elimu, ameeleza kuwa, mabadiliko yaliyofanyika katika sekta hiyo yanaonesha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa, hususan katika mabadiliko ya mitaala na kuibua vipaji vya vijana.

“Mimi nilikuwa Wizara ya Elimu na nilivyoiacha siyo ilivyo sasa. Mmepiga hatua kubwa, mmebadilisha. Tulivyoiacha siyo ilivyo leo. Mmerekebisha mtaala wa Amali na Sera, na matokeo yake tunayoyaona sasa, ambapo vijana wa kidato cha kwanza na cha pili wanaonesha uwezo wao,” amesema.

Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu kwa mwaka 2026 imezinduliwa rasmi na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, ikiwa na lengo la kuendeleza ujuzi, ubunifu na matumizi ya teknolojia miongoni mwa vijana na jamii kwa ujumla.

Kaulimbiu ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu mwaka 2026 ni: “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya 2050.”



Na Munir Shemweta, Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imekutana leo tarehe 12 Agosti 2026 Bungeni jijini Dodoma kupokea na kujadili taarifa kuhusu utendaji wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, ikiwa ni sehemu ya jukumu la Bunge la kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Serikali katika sekta ya ardhi.

Katika kikao hicho, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeieleza Kamati hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kuboresha utendaji wa Mabaraza hayo, ambayo yako chini ya Wizara hiyo.

Miongoni mwa hatua zilizobainishwa ni kuongezeka kwa idadi ya Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, kupungua kwa mashauri na malalamiko, kuimarishwa kwa matumizi ya mifumo ya kidijiti pamoja na kuboreshwa kwa mfumo wa uendeshaji wa shughuli za madalali.

Pamoja na mafanikio hayo, Kamati imeelezwa kuwa bado zipo changamoto kadhaa zinazoathiri utendaji wa Mabaraza hayo na kwamba Wizara inaendelea kuzifanyia kazi ili kuongeza ufanisi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amewaeleza wajumbe wa Kamati kuwa, Serikali inaendelea kushughulikia changamoto zinazoyakabili Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, akieleza kuwa kutatuliwa kwa changamoto hizo kutasaidia kuyafanya Mabaraza kuwa bora zaidi na yenye manufaa makubwa kwa wananchi.

 

Awali, wajumbe wa Kamati wameitaka Wizara kuweka mkazo zaidi katika matumizi ya usuluhishi wakati wa kushughulikia migogoro ya ardhi badala ya kila shauri kulenga kupata mshindi na mshindwa.

Wamesema, usuluhishi unaweza kusaidia kupunguza migogoro, kuharakisha utatuzi wa mashauri na kujenga mahusiano mazuri miongoni mwa wananchi.

Wajumbe hao wameeleza kuwa, pamoja na mafanikio yanayoonekana katika utendaji wa Mabaraza, bado ipo haja ya Wizara kuchukua hatua za haraka kukabiliana na changamoto zilizopo ili Mabaraza hayo yaweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuendelea kujenga imani ya wananchi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Timotheo Mzava, amesisitiza umuhimu wa Wizara kuongeza idadi ya wenyeviti wa Mabaraza, kupanua upatikanaji wa Mabaraza katika wilaya mbalimbali pamoja na kukamilisha mfumo wa kidijiti ili kuongeza ufanisi na kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.

“Sisi kama Kamati tunaona umuhimu wa kuwa na Mabaraza kila Wilaya pamoja na kukamilika kwa mfumo wa kidijiti, kwa kuwa mtakapoboresha, kelele kuhusu Mabaraza zitapungua,” amesema Mhe. Mzava.

Kikao hicho kilichoongozwa na Mhe. Mzava pia kimehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga, Naibu Katibu Mkuu Bi. Lucy Kabyemera, pamoja na viongozi na watendaji wengine wa Wizara.







Na Munir Shemweta, Bariadi, Simiyu

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amesema Wizara yake iko tayari kushirikiana na mikoa inayounda Kanda ya Ziwa Mashariki pamoja na Wizara ya Kilimo na wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuandaa ramani ya uwanja ikiwemo mpangilio kulingana na mahitaji ya eneo la Viwanja vya Maonesho Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu.

Mikoa inayounda kanda ya Ziwa Mashariki katika maonesho ya Wakulima (Nanenane) ni mkoa wa Simiyu, Mara Pamoja na Shinyanga.

Dkt. Akwilapo ameyasema hayo Agosti 8, 2026 wakati akifunga Maonesho na Sherehe za Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) Kanda ya Ziwa Mashariki, yaliyofanyika katika Viwanja vya Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu.

Amesema, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pia itasaidia kutoa muongozo wa umiliki wa eneo la uwanja na kuandaa mpango endelevu wa matumizi yake

Kwa mujibu wa Waziri huyo wa ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, upangaji mzuri wa eneo ni msingi muhimu katika kuhakikisha shughuli na miundombinu inayotekelezwa katika viwanja hivyo inakuwa ya kudumu, inatumika kwa ufanisi na inaepusha migongano ya matumizi ya ardhi hapo baadaye.

“Wizara yetu iko tayari kushirikiana na mikoa inayounda Kanda ya Ziwa Mashariki, Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kutayarisha ramani na mpangilio wa matumizi ya eneo hili kulingana na mahitaji yaliyopo na yajayo,” amesema Dkt. Akwilapo.

Akigeukia upande wa Maonesho ya Wakulima (Nane nane) katika kanda ya Ziwa Mashariki aliyoyafunga rasmi, Dkt Akwilapo ambaye alikuwa mgeni rasmi ametoa wito maonesho hayo kufanyika kuanzia ngazi za Vijiji, Kata, Mitaa na Halmashauri alizozieleza kuwa huko ndiko wananchi wanakoishi.

‘’Kufanyika kwa maonesho kuanzia ngazi hizo itasaidia kuwawezesha waliokusudia kuona na kujifunza teknolojia mbalimbali katika maeneo yao huko waliko’’. Amesema.

Amezishauri mamlaka za serikali za mitaa kuratibu ili maonesho hayo yaweze kufanyika katika ngazi za vijiji, kata, mitaa na wilaya kwa lengo la kuleta mapinduzi katika kilimo, mifugo na uvuvi.

Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha amesema maonesho na sherehe za wakulima (Nane nane) katika mkoa wake yalilenga kutoa fursa kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kujifunza, kubadilishana uzoefu, kujenga ushirikiano na kutangaza bidhaa wanazozalisha katika maeneo yao.

Amewashukuru washiriki wa maonesho hayo kwa kuonesha mbinu mbalimbali alizozieleza kuwa zimesaidia wananchi kujifunza teknolojia bora katika mnyonyoro wa thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Akwilapo alitembelea Banda la Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Simiyu ambapo alipata fursa ya kukabidhi hati miliki za ardhi kwa baadhi ya wananchi wa Bariadi mkoani Simiyu waliokamilisha taratibu za kumilikishwa maeneo yao.

Akizungumza baada ya kukabidhi hati hizo, Dkt. Akwilapo aliwataka wananchi waliopokea hati hizo kuhakikisha wanazingatia masharti yote yanayoambatana na umiliki wa ardhi zao.

Maonesho na Sherehe za Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) Kanda ya Ziwa Mashariki, yamefungwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo kwenye Viwanja vya Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu

 

 



Serikali imetangaza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameridhia utoaji wa kiasi cha shilingi bilioni 38 kwa ajili ya kufanikisha mpango wa kupima vijiji vyote nchini ili kumaliza migogoro ya ardhi.

Hayo yameelezwa leo Julai 1, 2026 katika viwanja vya Sokoni Mugumu Wilaya ya Serengeti mkoani Mara na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya alipokuwa akizungumza mbele ya Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tano mkoani humo.

Katika hatua ya haraka ya kusogeza huduma kwa wananchi, Mhe. Mmuya amemuagiza Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mara pamoja na timu yake, kuhakikisha wanaratibu na kuanzisha kliniki za ardhi katika kila kata.

"Hakikisheni mnaratibu uwepo wa kliniki za ardhi katika kila kata ili muwasikilize wananchi hawa na msione kila changamoto mpewazo ni ya mazoea. Hapana, amekuja kwako kwa sababu ana jambo la kusikilizwa na litatuliwe," alisema Naibu Waziri Mmuya.


Mhe. Mmuya alieleza kuwa wizara ya Ardhi iliwasilisha mpango na maombi ya fedha bungeni kufuatia maelekezo ya awali ya Waziri Mkuu, na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akaidhinisha shilingi bilioni 38 kwa ajili ya kupima jumla ya vijiji 12,333 vya Tanzania.


"Mpaka hivi ninavyoongea, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake kifupi tu ameweza kupima vijiji 4,873. Na ametupatia maelekezo kuwa ndani ya kipindi chake, vijiji vyote vilivyobakia tuvipime." Aliongeza Naibu Waziri Kaspar Mmuya 



Katika hatua nyingine Mhe. Mmuya amesema Wizara ya Ardhi itashirikiana bega kwa bega na Ofisi ya Rais - TAMISEMI ili kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa kikamilifu katika vijiji vyote vilivyosalia nchini.


Aidha, Mhe. Mmuya alieleza kuwa Wilaya ya Serengeti ina kata 30 na vijiji 78. Ameuhakikishia uongozi wa wilaya hiyo kuwa vijiji vyote 78 vimeshaingizwa kwenye mpango wa upimaji ndani ya kipindi cha miaka mitano ya Rais Samia Suluhu Hassan.


"Kupima vijiji hivi ndiyo dawa kubwa ya kutatua changamoto ya mipaka kati ya kijiji na kijiji. Lakini ni dawa kubwa ya kutatua changamoto ya kugombania matumizi ya ardhi ya mtu mmoja mmoja, taasisi na taasisi, au serikali na wananchi," alisema Naibu Waziri Kaspar Mmuya.

 Na Munir Shemweta, Itilima


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo ameitaka mikoa na wilaya nchini kuhakikisha zinatenga na kuandaa maeneo maalumu yatakayotumika kwa ajili ya kuanzisha kongani za viwanda.

Amesema upangaji mzuri wa matumizi ya ardhi ni muhimu katika kuvutia wawekezaji kwa kuwa mwekezaji anahitaji eneo lililotengwa na kutambuliwa kwa matumizi husika kabla ya kuanzisha shughuli zake.

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati alikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa shule ya awali na msingi katika Kitongoji cha Mwankola, Kata ya Lagangabilili pamoja na kusikiliza kero za wananchi katika Kijiji cha Simiyu kata ya Migato wilayani itilima mkoa wa Simiyu tarehe 7 Agosti 2026 Dkt.  Akwilapo amesema hatua hiyo pia inalenga kuzuia migogoro ya matumizi ya ardhi kati ya makazi, shughuli za kilimo, viwanda na matumizi mengine yanayohitaji maeneo maalumu.

Aidha, Waziri huyo wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameeleza kuwa,  Wizara yake   imejipanga kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maeneo yao yanasimamiwa kwa kuzingatia sheria.

Amewataka wananchi wa Itilima kufuata sheria, kanuni na taratibu zinazohusu umiliki na matumizi ya ardhi ili kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na migogoro ya ardhi.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha ameeleza kuwa, mkoa wa Simiyu hususan wilaya ya Itilima wanatambua umuhimu wa ardhi hasa katika kumilikisha wananchi, taasisi na vijiji lengo likiwa kuepuka migogoro ya ardhi.

Wakiwasilisha kero yao mbele ya Waziri wa Ardhi, wananchi wa Itilima wameiomba serikali kuwawekea uzio utakaowasaidia kuepukana na uvamizi wa mara kwa mara wa tembo wanaotoka hifadhini kwenda katika maeneo yao.

‘’Tunashukuru kwa ahadi ya kuwekewa uzio wa umeme kwa ajili ya kuzuia tembo kuvamia maeneo yetu ila tunaomba ahadi hiyo iwe ya kweli’. Amesema mkazi wa Itilima’

Hata hivyo, Mkuu wa mkoa wa Simiyu amewaambia wananchi hao kuwa serikali tayari imejipanga kuhakikisha inajenga uzio wa umeme kwa ajili ya kuzuia tembo kuingia katika maeneo ya wananchi.

‘’Niwaase wananchi kutoenda katika maeneo ya hifadhi kwa ajili ya kufanya uharibifu na mtoe ushirikiano wa kulinda uzio wa umeme pale utakaojengwa’’. Amesema

Mkuu wa wilaya ya Itilima Bi. Anna Gidarya amesema halmashauri ya wilaya ya Itilima ina lengo la kuandaa hati milki za viwanja vyote 1,604 vilivyopangwa ambapo hadi kufikia juni 2026 jumla ya hati milki 506 zimeandaliwa na kusajiliwa.

‘’Hati za viwanja vilivyosalia havijamilkishwa kwa vile wamiliki hawajalipia gharama za uandaaji wa milki hizo’’. Amesema Bi. Gidarya.

Katika hatua nyingine, Dkt. Akwilapo amewataka wananchi wa Wilaya ya Itilima kuendelea kulinda amani na utulivu uliopo nchini kwa kuwa ndiyo msingi wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.

Amesema, hakuna uwekezaji unaoweza kufanyika kwa ufanisi katika mazingira yasiyo na amani, hivyo ni jukumu la wananchi kuendelea kuthamini na kulinda utulivu uliopo Tanzania.

Ameeleza kuwa maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu, viwanda, biashara na miundombinu, yanahitaji mazingira tulivu yanayowawezesha wananchi na wawekezaji kufanya shughuli zao bila hofu.

“Uwekezaji wowote unategemea amani na utulivu na maendeleo yatakayopatikana yatatokana na amani. Hivyo amani inaiweka nchi katika nafasi nzuri ya kupokea wawekezaji,” amesema Dkt. Akwilapo.

Amesema uwepo wa amani unaifanya nchi kuwa na mazingira yanayovutia miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo baadaye inaweza kutoa ajira, kuongeza mapato na kuboresha maisha ya wananchi.

Ziara ya Dkt Akwilapo wilayani Simiyu ni sehemu ya mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuwapeleka mawaziri katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyoahidiwa kwa wananchi wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokuwa akiomba kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akilakiwa na wananchi wa Itilima alipowasili Kijiji cha Simiyu kata ya Migato wilayani itilima mkoa wa Simiyu kusikiliza kero za wananchi wakati wa ziara yake mkoani humo.Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akikabidhiwa Zawadi ya kuku na wananchi wa Kijiji cha Simiyu kata ya Migato mara baada ya kuzungumza nao wilayani Itilima mkoa wa Simiyu tarehe 7 Agosti 2026. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akipata maelezo ya mradi wa ujenzi wa Daraja katika Kijiji cha Simiyu kata ya Migato wilaya ya Itilima mara baada ya kusikiliza kero za wananchi tarehe 7 Agosti 2026. Kulia kwa Dkt Akwilapo ni Mkuu wa mkoa wa Simiyu mhe. Anamringi Macha na kushoto kwake ni mkuu wa wilaya ya Itilima Bi. Anna Gidarya.

Sehemu ya wananchi wa Itilima waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo uliofanyika katika Kijiji cha Simiyu kata ya Migato wilayani Itilima mkoa wa Simiyu tarehe 7 Agosti 2026.
Muonekano wa Daraja lililopo Kijiji cha Simiyu kata ya Migato wilaya ya Itilima.(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)