Makamu Mkuu wa chuo kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha akipokea mfano wa funguo za majengo ya Kampasi ya Tanga kutoka kwa Mkandarasi aliyemaliza kazi yake

************

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha,amesema Chuo kinatarajia kuanza kudahili wanafunzi katika Tawi la Tanga lililopo Wilaya ya Mkinga, kwa mwaka wa masomo 2027/2028, huku kikikusudia kufikia wanafunzi 10,000

Kauli hiyo ameitoa Novemba 26, 2026, wakati wa makabidhiano ya majengo ya kampasi hiyo uliofanywa na Mkandarasi Dimetoclasa Realhope Ltd, chini ya usimamizi wa Mshauri Elekezi Mekon Arch Consultant Ltd.

Prof. Mwegoha ameishukuru Serikali, viongozi wa mkoa wa Tanga na wadau mbalimbali kwa ushirikiano wao uliofanikisha utekelezaji wa mradi huo, akibainisha kuwa chuo kiliweza kupata eneo lenye ukubwa wa ekari 300 kwa ajili ya maendeleo ya taasisi hiyo katika kijiji cha Gombero wilayani Mkinga

Kwa upande wake, Mshauri Elekezi wa mradi huo kutoka Kampuni ya Mekon Arch Consultant Ltd, Dkt. Moses Mkony, amesema kuwa licha ya changamoto za miundombinu ya eneo la mradi zilizosababisha kuongezeka kwa muda wa utekelezaji kutoka miezi 18 iliyopangwa awali, wamefanikiwa kufikisha ujenzi katika hatua ya makabidhiano.

Ameeleza kuwa mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 12 unajumuisha majengo ya kitaaluma pamoja na kituo cha afya, ambacho awali kilipangwa kuwa zahanati, lakini baada ya tathmini chuo kikuu Mzumbe kiliridhia kujengwa katika hadhi ya kituo cha afya ili kupanua wigo wa huduma kwa jamii inayozunguka Chuo.

Mkurugenzi wa huduma za afya wa Chuo kikuu Mzumbe Dkt. Rajab Nyagara, ameeleza kuwa kituo hicho cha afya kinatarajiwa kuanza kutoa huduma kwa wananchi hivi karibuni, hata kabla ya kuanza kwa shughuli za kitaaluma za Chuo na kuongeza kuwa miongoni mwa huduma zitakazotolewa zitajumuisha huduma za matibabu na upasuaji, hatua inayotarajiwa kupunguza changamoto za wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo za afya.

Uwepo wa Chuo Kikuu Mzumbe katika eneo hilo unatarajiwa kuongeza fursa za elimu ya juu, ajira, biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa jamii inayokizunguka.
Makamu Mkuu wa chuo kikuu Mzumbe akipokea cheti cha ukamilisho wa kazi ya Mkandarasi kutoka kwa Mshauri elekezi.
Moja ya jengo la hosteli za Wanafunzi.
Timu ya Menejimenti ya chuo kikuu Mzumbe na Wadau wakitembelea majengo kabla ya makabidhiano
Makamu Mkuu wa chuo kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha akizungumza wakati wa makabidhiano
Moja ya nyumba za watumishi katika kampasi ya Tanga
Makamu Mkuu wa chuo kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha akikabidhi ufunguo huo kwa Naibu Makamu Mkuu wa chuo kikuu Mzumbe anaeshughulikia Mipango, fedha na utawala Prof. Allen Mushi
Naibu Makamu Mkuu wa chuo kikuu Mzumbe anaeshughulikia mipango, fedha na utawala Prof. Allen Mushi akikabidhi ufunguo huo kwa Kaimu Rasi wa ndaki ya Tanga Prof. Malipula.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Gombero Mje. Zuberi Magoha akizungumza na wadau waliohudhuria hafla ya makabidhiano ya majengo ya chuo kikuu Mzumbe Kampasi ya Tanga

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: