Na Munir Shemweta, Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imekutana leo tarehe 12 Agosti 2026 Bungeni jijini Dodoma kupokea na kujadili taarifa kuhusu utendaji wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, ikiwa ni sehemu ya jukumu la Bunge la kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Serikali katika sekta ya ardhi.

Katika kikao hicho, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeieleza Kamati hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kuboresha utendaji wa Mabaraza hayo, ambayo yako chini ya Wizara hiyo.

Miongoni mwa hatua zilizobainishwa ni kuongezeka kwa idadi ya Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, kupungua kwa mashauri na malalamiko, kuimarishwa kwa matumizi ya mifumo ya kidijiti pamoja na kuboreshwa kwa mfumo wa uendeshaji wa shughuli za madalali.

Pamoja na mafanikio hayo, Kamati imeelezwa kuwa bado zipo changamoto kadhaa zinazoathiri utendaji wa Mabaraza hayo na kwamba Wizara inaendelea kuzifanyia kazi ili kuongeza ufanisi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amewaeleza wajumbe wa Kamati kuwa, Serikali inaendelea kushughulikia changamoto zinazoyakabili Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, akieleza kuwa kutatuliwa kwa changamoto hizo kutasaidia kuyafanya Mabaraza kuwa bora zaidi na yenye manufaa makubwa kwa wananchi.

 

Awali, wajumbe wa Kamati wameitaka Wizara kuweka mkazo zaidi katika matumizi ya usuluhishi wakati wa kushughulikia migogoro ya ardhi badala ya kila shauri kulenga kupata mshindi na mshindwa.

Wamesema, usuluhishi unaweza kusaidia kupunguza migogoro, kuharakisha utatuzi wa mashauri na kujenga mahusiano mazuri miongoni mwa wananchi.

Wajumbe hao wameeleza kuwa, pamoja na mafanikio yanayoonekana katika utendaji wa Mabaraza, bado ipo haja ya Wizara kuchukua hatua za haraka kukabiliana na changamoto zilizopo ili Mabaraza hayo yaweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuendelea kujenga imani ya wananchi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Timotheo Mzava, amesisitiza umuhimu wa Wizara kuongeza idadi ya wenyeviti wa Mabaraza, kupanua upatikanaji wa Mabaraza katika wilaya mbalimbali pamoja na kukamilisha mfumo wa kidijiti ili kuongeza ufanisi na kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.

“Sisi kama Kamati tunaona umuhimu wa kuwa na Mabaraza kila Wilaya pamoja na kukamilika kwa mfumo wa kidijiti, kwa kuwa mtakapoboresha, kelele kuhusu Mabaraza zitapungua,” amesema Mhe. Mzava.

Kikao hicho kilichoongozwa na Mhe. Mzava pia kimehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga, Naibu Katibu Mkuu Bi. Lucy Kabyemera, pamoja na viongozi na watendaji wengine wa Wizara.





Share To:

Post A Comment: