Na Munir Shemweta
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Lucy Kabyemera, ameahidi kuwa Wizara yake itayafanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wadau wa sekta ya ardhi, huku akiwataka kuimarisha ushirikiano na kuachana na tabia ya kunyoosheana vidole.
Bi. Kabyemera ametoa ahadi hiyo Novemba 24, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akifunga kikao kazi kati ya Wizara ya Ardhi na kampuni zinazojihusisha na mipango miji, upimaji wa ardhi na uendelezaji wa milki.
Amesema, Wizara ya Ardhi natambua mchango mkubwa wa wadau hao katika maendeleo ya sekta ya ardhi na makazi, hivyo itaendelea kushirikiana nao katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazokabili sekta hiyo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ameeleza kuwa, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeipa sekta ya ardhi nafasi muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo ni muhimu kwa Serikali na wadau kuunganisha nguvu katika kuhakikisha utekelezaji wake unafanikiwa.
Bi. Kabyemera amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ipo tayari kuunga mkono juhudi za wadau katika kuendeleza sekta hiyo.
“Malengo ya Rais ni kuhakikisha vikwazo katika maeneo mbalimbali, ikiwemo sekta ya ardhi, vinaondolewa ili kuwezesha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kufanyika kwa ufanisi,” amesema.
Amehakikishia washiriki wa kikao kazi hicho kuwa, maoni na mapendekezo yote yaliyowasilishwa yatafanyiwa kazi kwa kina, akibainisha kuwa Wizara inazifahamu changamoto zinazokabili sekta hiyo na tayari imeanza kuzishughulikia.
“Tutafanyia kazi maoni ya wadau mpaka mwisho na tayari tumeanza kuzifanyia kazi baadhi ya changamoto mbalimbali na tunazifahamu,” amesema.
Aidha, amesema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa katika kuboresha usimamizi wa sekta ya ardhi ni kurejeshwa kwa watumishi wa sekta hiyo chini ya Wizara, hatua ambayo amesema imeonesha matokeo chanya katika usimamizi na maendeleo ya sekta hiyo.
Hata hivyo, amewataka wadau kuachana na tabia ya kunyoosheana vidole na badala yake kujenga utamaduni wa kushirikiana katika kutatua changamoto zinazowakabili.
Amesema, kulaumiana hakusaidii kutatua changamoto zilizopo, bali kunatoa taswira isiyofaa kwa sekta hiyo, hivyo ni muhimu kwa Wizara na wadau kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuimarisha huduma na kuendeleza sekta ya ardhi nchini.
Amesisitiza kuwa, ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuhakikisha sekta ya ardhi inachangia ipasavyo maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania.
Kikao hicho cha siku mbili kimewakutanisha wataalamu na kutoka kampuni za Mipangomiji, upangaji, upimani pamoja na wale wa uendelezaji milki.

Post A Comment: