Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amezitaka halmashauri nchini kuongeza uwekezaji katika afua za lishe na kuimarisha ushirikiano wa sekta mbalimbali, akisisitiza kuwa lishe bora ni msingi wa afya ya wananchi na maendeleo ya taifa.

Akizungumza katika Mkutano wa 10 wa Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa mwaka wa fedha 2025/2026 jijini Dodoma, Prof. Shemdoe amezitaka halmashauri ambazo hazijafikia viwango vilivyotarajiwa kuongeza juhudi, huku zilizofanya vizuri zikiendelea kuboresha utendaji. Amesema mapambano dhidi ya changamoto za lishe yanahitaji ushirikiano wa sekta za afya, kilimo, mifugo, uvuvi, elimu, maji na hifadhi ya jamii.

Amesema tathmini imeonesha kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, lengo lilikuwa kukusanya na kuelekeza Shilingi Bilioni 207.2 katika afua za lishe, lakini halmashauri zimefanikiwa kufikisha Shilingi Bilioni 70.8. Kutokana na hali hiyo, amewataka viongozi kuimarisha usimamizi wa rasilimali fedha na kuhakikisha zinatumika kulingana na mipango iliyowekwa.

 Pia amezihimiza halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya tafiti za kiutendaji ili kubaini changamoto za lishe na kuweka mikakati inayozingatia mahitaji ya wananchi, akitolea mfano wa tafiti zilizoanza katika mikoa ya Mtwara, Njombe na Iringa.

Katika mafanikio mengine, Prof. Shemdoe amebainisha kuimarika kwa matumizi ya mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji mapato katika halmashauri, ambapo kiwango cha mifumo iliyofungwa kimeongezeka kutoka asilimia nane mwaka uliopita hadi asilimia 92 katika mwaka wa tathmini. 

Amesema hatua hiyo imechangia kuongeza makusanyo kutoka chini ya Shilingi Bilioni Moja kwa wiki hadi kati ya Shilingi Bilioni 3.2 na 3.6 kwa wiki, akiwataka halmashauri zilizobaki kukamilisha zoezi hilo na kuhakikisha mifumo iliyofungwa inatumika ipasavyo. 

Aidha, amesisitiza kuendelea kuimarisha upatikanaji wa vyakula vilivyoongezwa virutubisho, hususan katika shule, pamoja na usimamizi wa huduma za afya ya mama na mtoto.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI, Florent Kyombo, amezitaka halmashauri kuongeza bajeti ya lishe katika maandalizi ya bajeti ya mwaka 2027, akisisitiza kuwa kiwango cha Shilingi 1,000 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano kinachotajwa katika mwongozo wa bajeti ni kiwango cha chini, hivyo halmashauri zinapaswa kutenga fedha zaidi kulingana na mahitaji na uwezo wao. Amesema uwekezaji huo ni muhimu katika kupunguza utapiamlo na kuboresha afya na ukuaji wa watoto.

Kyombo amesema halmashauri zinapaswa kujipima na kuona uwezekano wa kuongeza kiwango hicho hadi Shilingi 1,200, 1,500 au 2,000 kwa kila mtoto, badala ya kuishia kwenye kiwango cha chini kilichowekwa. Ameongeza kuwa Kamati ya Bunge itaendelea kushirikiana na Wizara katika kusimamia na kuishauri Serikali kuhusu maboresho ya huduma za lishe, akieleza kuwa mikutano ya tathmini ni fursa muhimu ya kutambua mafanikio, kubaini mapungufu na kuweka mikakati mipya ya utekelezaji.

Prof. Shemdoe amehitimisha kwa kuwataka wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi na watendaji wengine kuendelea kusimamia kwa karibu afua za lishe na kusikiliza changamoto za wananchi. 

Amesema Mkataba wa Lishe ulioanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, umeimarisha mifumo ya usimamizi wa lishe nchini, hivyo ni muhimu kuendeleza dhamira na uwajibikaji katika kuhakikisha kila mtoto anapata lishe bora na jamii inakuwa na afya imara.












Share To:

Post A Comment: