SERIKALI imeweka mikakati ya kuhakikisha tiba asili inajumuishwa katika mfumo rasmi wa huduma za afya nchini ifikapo mwaka 2030, hatua inayolenga kuongeza usalama kwa watumiaji, kuimarisha tafiti za kisayansi na kukuza uzalishaji wa dawa zinazotokana na malighafi zinazopatikana nchini.

Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imeandaa Dhifa ya Uwekezaji katika Dawa za Tiba Asili (Asili Investment Gala 2027), inayotarajiwa kukutanisha washiriki zaidi ya 1,000 kutoka sekta binafsi, taasisi za fedha, jumuiya ya kidiplomasia, washirika wa maendeleo, taasisi za utafiti na wadau wa tiba asili.

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya dhifa hiyo inayotarajiwa kufanyika Aprili 2027.

Alisema dhifa hiyo inalenga kuhamasisha uwekezaji na ushirikiano katika tafiti, ubunifu, uzalishaji wa dawa za tiba asili na kujenga uwezo wa rasilimali watu ili kuwezesha ujumuishaji wa tiba hiyo katika mfumo rasmi wa huduma za afya nchini.

Alisema Serikali inataka tiba asili itambuliwe na kuingizwa katika mifumo ya afya kuanzia ngazi ya msingi hadi taasisi za kitaifa, huku dawa zinazotumika kwa binadamu zikihakikiwa na kuthibitishwa kisayansi kuhusu usalama, ubora na ufanisi wake.

“Moja ya harakati kubwa ambazo tunaendelea nazo sasa ni pamoja na kuijumuisha pia katika Bima ya Afya kwa Wote, lakini kuhakikisha kwamba mifumo yetu yote ya afya inatambua tiba asili,” alisema Mchengerwa.

Alisema tafiti zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wanatumia tiba asili, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuweka utaratibu rasmi wa kusimamia sekta hiyo ili wananchi wapate huduma na dawa salama.

Alibainisha kuwa zipo dawa za tiba asili zilizosajiliwa, lakini nyingine bado hazijapitia taratibu rasmi za Serikali, hivyo kuhitajika ushirikiano kati ya wataalamu, wadau na taasisi za udhibiti.

“Tunataka kuwashawishi Watanzania na wale wote ambao ni wadau wetu katika mnyororo mzima wa tiba asili kurasimisha dawa zao ili Serikali iweze kuzipitia na kujiridhisha kutokana na ushahidi wa kisayansi na kitafiti,” alisema.

Alisema baadhi ya dawa zinazotumika hazijafanyiwa tafiti za kisayansi wala kuthibitishwa, hali inayoweza kusababisha madhara kwa watumiaji, ikiwemo kuathiri viungo vya mwili.

Alisema kupitia mfumo unaokusudiwa kujengwa, Serikali itashirikiana na wadau wa tiba asili kufanya tafiti, kupata ushahidi wa kisayansi na kuthibitisha dawa zinazofaa kutumiwa na binadamu.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, dhifa hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na washiriki zaidi ya 1,000 kutoka ndani na nje ya nchi.

Alisema kaulimbiu ya dhifa hiyo ni 'Wekeza katika dawa zetu za ndani za tiba asili', inayolenga kuhamasisha uwekezaji katika rasilimali za tiba asili zilizopo nchini kwa kuzitambua, kuzithamini na kuzitathmini ili kukuza tafiti, ubunifu na uzalishaji wa viwandani.

Alisema uwekezaji huo utachangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa bidhaa za afya, sambamba na Mpango Mkakati wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa Tiba Asili wa mwaka 2025–2034 unaosisitiza ujumuishaji wa tiba asili zenye ushahidi wa kisayansi, ufanisi, usalama na ubora katika mifumo ya afya.

Alieleza kuwa matokeo yanayotarajiwa ni pamoja na kupatikana kwa dawa za tiba asili za kutibu magonjwa ya kipaumbele zenye ushahidi wa kisayansi, kuimarika kwa uwezo wa kitaifa wa kufanya tafiti na kujengwa kwa viwanda vya dawa vitakavyotumia malighafi zinazopatikana nchini.

Aidha, mpango huo utajumuisha mafunzo kwa watoa huduma za afya ili kuwawezesha kuelewa na kutumia ipasavyo mfumo wa tiba asili utakaotambuliwa rasmi, hatua itakayosaidia kuongeza usalama kwa wagonjwa.

Katika hatua nyingine, Mchengerwa alisema uwekezaji katika sekta hiyo utapanua fursa za kiuchumi kupitia mnyororo wa uzalishaji wa dawa za tiba asili, ikiwemo kilimo cha mimea tiba na uchakataji wa kisasa wa malighafi.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza ajira kwa vijana, kukuza uzalishaji wa ndani na kuongeza pato la Taifa.

Aliwataka wafanyabiashara, wamiliki wa migodi, kampuni binafsi, taasisi za kifedha, mashirika ya Serikali na wadau wengine kujitokeza kushiriki katika dhifa hiyo kwa kutoa michango na kuwekeza katika sekta ya tiba asili.

“Ushirikiano wenu ni muhimu katika kufanikisha azma ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa bidhaa za afya barani Afrika,” alisema.

Alisisitiza kuwa Wizara ya Afya itasimamia ukusanyaji na matumizi ya michango kwa kuzingatia taratibu za Serikali, huku fedha zitakazopokelewa zikipitia akaunti rasmi za Serikali na kutumika katika shughuli zilizoidhinishwa.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: