Zaidi ya wadau 400 kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga wamekutana jijini Arusha katika kikao cha kujadili na kuimarisha utekelezaji wa Mpango wa Shule Salama, unaolenga kuhakikisha wanafunzi wanakamilisha masomo yao katika mazingira salama na kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji.

Akizungumza katika kikao hicho akiwa mgeni rasmi, Dr. Theresa Kuiwite amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mikakati ya ulinzi wa wanafunzi ili kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya elimu katika mazingira salama, kuanzia nyumbani hadi shuleni.

Akifafanua kuhusu utekelezaji wa mpango huo, Juma Kizija, ambaye ni Mkufunzi Mkuu wa Chuo cha Ualimu Mpwapwa na Mwezeshaji wa Kitaifa wa Mpango wa Shule Salama, amesema mpango huo una mikakati mbalimbali ya kuhakikisha mwanafunzi analindwa dhidi ya changamoto zinazoweza kumkatisha masomo.

Amesema mikakati hiyo inahusisha kuimarisha mahusiano kati ya wazazi, walimu na wanafunzi, uwepo wa walimu wa unasihi wa kike na wa kiume pamoja na masanduku ya malalamiko shuleni yatakayowezesha wanafunzi kuripoti changamoto zinazowakabili na kupata ufumbuzi.

Aidha, mpango huo unahusisha mabaraza ya watoto, wakiwemo wenye mahitaji maalum, ili kuwajengea uwezo wa kutambua na kuripoti vitendo vya ukatili, ikiwemo ukatili wa mtandaoni. Pia, vikundi vya waendesha bodaboda vinashirikishwa katika kuhakikisha usalama wa wanafunzi wanapokuwa safarini kwenda na kurudi shuleni.

Katika hatua nyingine, umuhimu wa kuifikisha elimu ya Shule Salama kwa wanafunzi, walimu, wazazi na jamii umeendelea kusisitizwa kupitia semina zinazofanyika katika maeneo mbalimbali.

Akizungumza katika semina ya Shule Salama iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Ruchya, Mwalimu John Masawe kutoka Wilaya ya Mkinga, Mkoa wa Tanga, amesema elimu hiyo inalenga kuwajengea wadau uelewa kuhusu wajibu wao katika kulinda haki za mtoto na kuhakikisha wanafunzi wanakamilisha masomo yao hadi kidato cha nne na kuendelea na ngazi nyingine za elimu.

Amesema semina hizo zimewakutanisha wanafunzi, walimu, wajumbe wa bodi za shule na viongozi wa jamii, ambao wamepatiwa elimu na nyenzo za kutambua, kuzuia na kutoa taarifa kuhusu vitendo vinavyohatarisha usalama wa wanafunzi.

Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya shule, wazazi na jamii ni muhimu katika kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kusoma, kutimiza ndoto zake na kufikia malengo yake ya kielimu bila kukumbwa na ukatili na unyanyasaji.















Share To:

Post A Comment: