Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imesema imeweka mikakati ya kuongeza uwekezaji katika kilimo himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia mifumo ya kisasa ya tathmini ya vihatarishi vya tabianchi, dhamana za mikopo na ushirikiano na taasisi za kifedha ili kuwawezesha wakulima wadogo kupata mitaji.
Akizungumza katika jukwaa la pembeni la Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), lililofanyika katika Banda la Tanzania (Tanzania Pavilion), Antalya nchini Uturuki, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB amesema kilimo kimekuwa kikichukuliwa kuwa sekta yenye hatari kubwa ya uwekezaji kutokana na uelewa mdogo kuhusu namna sahihi ya kutoa mikopo inayozingatia misimu na mabadiliko ya mnyororo wa thamani wa mazao.
Amesema TADB imefanikiwa kuonesha kuwa kilimo kinaweza kuwa eneo lenye fursa nzuri za uwekezaji kupitia mfumo wake wa Ufadhili Jumuishi wa Mnyororo wa Thamani (Integrated Value Chain Financing Model - IVCF), unaowezesha kutoa fedha kuanzia uzalishaji, ukusanyaji wa mazao, uongezaji thamani hadi mauzo ya nje, hatua inayosaidia kuongeza tija na kuhakikisha mikopo inarejeshwa.
Aidha, amesema benki hiyo imeanzisha mfumo wa kidijitali wenye taarifa za kiakili kuhusu vihatarishi vya tabianchi (Climate Risk Intelligence), unaosaidia kutambua kiwango cha athari za mabadiliko ya tabianchi kwa wateja wake na kutoa mwongozo wa uwekezaji unaozingatia kilimo himilivu na kupunguza hatari za kifedha.
Katika hatua nyingine, amesema TADB imefanikiwa kuchochea upatikanaji wa zaidi ya dola za Marekani milioni 300 kwa ajili ya sekta ya kilimo kupitia Mpango wa Dhamana ya Mikopo kwa Wakulima Wadogo (Smallholder Credit Guarantee Scheme), wenye mtaji wa takribani dola milioni 50, tangu kuanza kwake miaka minane iliyopita.
Ameeleza kuwa mpango huo unaotekelezwa kupitia taasisi 22 za kifedha umewezesha zaidi ya wakulima wadogo 680,000, wakiwemo wanawake na vijana, kupata huduma za kifedha kwa kupunguza changamoto ya dhamana ya mikopo ambayo imekuwa kikwazo kwa makundi hayo.
Ameongeza kuwa TADB inaendelea kutoa mafunzo na msaada wa kitaalamu kwa taasisi za kifedha, wakulima na wafanyabiashara wadogo wa kilimo kuhusu namna bora ya kutoa mikopo ya kilimo na kuandaa mifumo ya ufadhili unaozingatia mabadiliko ya tabianchi, huku ikitumia pia mfumo wa ufadhili wa pamoja na taasisi nyingine kuongeza uwekezaji binafsi katika sekta hiyo.
Akizungumzia hatua zitakazochukuliwa ndani ya miezi 12 ijayo, amesema TADB itaendelea kutekeleza mpango mkakati wa kufadhili kilimo cha kijani na kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, kupanua matumizi ya mfumo wake wa kidijitali wa tathmini ya vihatarishi na kuimarisha ushirikiano na wadau wa maendeleo ili kuongeza upatikanaji wa fedha za tabianchi kwa wakulima wadogo.
Amesisitiza kuwa kufanikisha malengo ya taifa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kunahitaji mfumo wa ufadhili mseto unaohusisha Serikali, taasisi za maendeleo na sekta binafsi ili kuhakikisha mitaji inawafikia wakulima na biashara za kilimo.






Post A Comment: