Na Denis Chambi, Tanga.
Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Bw. Philemon Mwita Magesa amewapatia vitendea kazi Watendaji wa mitaa 181 ya Jiji la Tanga kwa ajili ya kukusanya taarifa za wafanyabiashara katika mitaa yao ili kuliwezesha Jiji la Tanga kuwa na kanzidata moja ya biashara zote zinazofanywa ndani ya Jiji.
Mkurugenzi Magesa amewapatia vitendea kazi hivyo baada ya kumalizika kwa kikao kazi alichokiitisha kilichowahusisha Watendaji hao wa Mitaa, Kata, Maafisa Tarafa na Maafisa Afya kwa lengo la kufahamiana na kuwapa mwelekeo wa kiutendaji na vipaumbele vyake katika kuwahudumia wananchi.
Magesa amesema kanzidata ndio msingi wa kila kitu katika kufikia maendeleo, kwani bila kuwa na takwimu huwezi kufanya makisio ya mapato wala kuwa na kipimo kizuri cha utendaji, na kwamba sasa kila mtaa na kata utapimwa katika ukusanyaji wa mapato kutokana na taarifa zitakazo kusanywa kila mtaa.
Mwanzoni mwa wiki hii, Mkurugenzi Magesa aliagiza pia kupatiwa vishikwambi kumi na viunganishi vya Internet kwa timu tano za mapato zinazofanya kazi kwa kanda, ili kurahisisha utoaji wa huduma karibu na wananchi na kuondoa usumbufu wa kufuata huduma makao makuu ya Halmashauri.







Post A Comment: