NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kupitia Ndaki ya Sayansi za Jamii, kimeandaa mkutano wa kitaaluma wa siku mbili kujadili nafasi, changamoto na fursa za kizazi cha Gen Z katika jamii, uchumi na mabadiliko ya teknolojia duniani.
Mkutano huo unalenga kuelewa mienendo ya kizazi hicho, ambacho kimekuwa kikijitokeza katika maeneo mbalimbali duniani kikieleza mitazamo yake, mahitaji na nafasi yake katika jamii, huku ukitoa fursa kwa watafiti na wadau kujadili namna bora ya kukabiliana na mabadiliko hayo.
Akizungumza leo na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayeshughulikia Utafiti, Prof. Nelson Boniface, amesema vyuo vikuu vina wajibu wa kufanya tafiti zenye ushahidi zitakazosaidia jamii kuelewa mabadiliko yanayoletwa na kizazi hicho na kutoa mwongozo kwa watunga sera.
Amesema mkutano huo umewakutanisha wataalamu na maprofesa kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujadili harakati za Gen Z duniani na kutafuta namna bora ya kuwasaidia vijana hao kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya uchumi.
Prof. Boniface amesema mijadala hiyo pia inalenga kujenga uelewa wa pamoja kati ya kizazi cha sasa na vizazi vilivyotangulia ili kila upande uweze kuelewa mitazamo na matarajio ya mwenzake.
Kwa upande wake, Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii ya UDSM, Prof. Christine Noe, amesema mjadala huo unaangazia masuala ya Gen Z kwa mtazamo mpana wa kimataifa, kwa kuwa mabadiliko yanayohusiana na kizazi hicho yanagusa nyanja za kijamii, kiuchumi na kiteknolojia.
Amesema mkutano huo pia unachunguza namna maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri maisha ya vijana, yakiwamo fursa na changamoto zinazojitokeza.
Aidha, amesema ni muhimu kwa jamii kuelewa mabadiliko ya vijana na kutafuta namna bora ya kuwaongoza, huku serikali na watunga sera wakihakikisha kuwa vijana wanapata huduma stahiki na kushirikishwa katika mipango ya maendeleo ya sasa na ya baadaye.
Ameongeza kuwa matokeo ya tafiti yatasaidia kutoa uelewa mpana kuhusu mahitaji ya vijana na namna ya kuweka sera zinazotambua mchango wao katika maendeleo ya taifa.

Post A Comment: