Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amesisitiza kuwa mchakato wa kutoa ufadhili kupitia Samia Scholarship unapaswa kuwa huru na usio na upendeleo wowote, huku akiwataka wadau kuzungumza suala hilo kwa umakini ili kuepuka tafsiri potofu.

Wanu aliyasema hayo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST). Alisema ni muhimu kuhakikisha haki inatendeka na nafasi zinawafikia wale wanaostahili kwa vigezo vilivyowekwa.

"Ninaomba sana suala hili mlizungumzie kwa namna ambayo halitaleta tafsiri ya upendeleo. Tuhakikishe kuwa hakuna upendeleo katika mchakato huu wa Samia Scholarship, bali wanaopata nafasi ni wale wanaostahili," alisema.

Kuhusu wanafunzi wanaonufaika na programu hiyo, Naibu Waziri alisema ni vijana wanaojitambua na wenye uwezo mkubwa, hivyo hapaswi kudharauliwa. Alieleza kuwa alipata fursa ya kuzungumza nao wakati wa boot camp alipokuja kwa ajili ya uhakiki wa taarifa na kubaini kuwa ni vijana wenye uelewa mpana wa mazingira yao.

"Kwa hiyo, ninawaomba mnapokuwa nao msidharau uwezo wao. Wapewe nafasi ya kuishi na kujifunza kutokana na malezi na maelekezo mnayowapa, lakini pia waaminiwe. Ni vizuri pia kuwapa nafasi ya kuzungumza kwa Kiingereza ili kuimarisha uwezo wao wa kuwasiliana na kuwajengea Ujasiri"Alisisitiza Naibu Waziri 

Alisema Rais Samia Suluhu Hassan ana imani kubwa na timu inayotekeleza programu hiyo, na mara nyingi amekuwa akisisitiza kwa Waziri wa Elimu kuwa ni jukumu la pamoja kuhakikisha ndoto hiyo inatimia. "Mheshimiwa Rais amekuwa akimwambia Mheshimiwa Waziri, 'Tupambane, hili ni jukumu langu na lako'. Nimepokea pongezi kwa niaba ya Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri," alisema huku akiwapongeza watendaji wote na kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati kwa usimamizi mzuri wa mipango na shughuli za kamati.

Nae Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye ni Mbunge wa Kyela, Mhe. Baraka Mwambengo,mara baada ya  wa ziara ya kamati katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), alisema kamati imeshuhudia uwekezaji mkubwa unaofanyika katika sayansi na teknolojia kupitia ufadhili huo, ambao ni matunda ya maono ya Rais Samia.

 Mwambengo aliwaasa wanafunzi watakaokwenda kusoma nje ya nchi kupitia ufadhili huo kutanguliza uzalendo, maadili na utamaduni wa Kitanzania.

“Mnapokwenda nje mtakutana na mambo mengi tofauti na maadili yetu. Jitambueni,kumbukeni mmetumwa na kijiji kikubwa zaidi, ambacho ni Taifa la Tanzania, Nendeni mkaiwakilishe nchi vizuri,” alisisitiza.

Mwambengo alibainisha kuwa licha ya uwekezaji mkubwa wa vifaa na teknolojia za kisasa chuoni hapo, baadhi yake bado havijaanza kutumika kibiashara.

“Hatutaki kuona chuo hiki kinabaki kuwa sehemu ya kufundishia na kufanya tafiti pekee bali tunataka kiwe kitovu cha kuzalisha bunifu na suluhisho zinazotumika kiuchumi. Teknolojia hizo zipelekwe sokoni wananchi wanufaike,” alisema.

Kamati pia ilipongeza wanafunzi wa Shahada ya Uzamili wanaofanya tafiti za Akili Unde (Artificial Intelligence - AI), na kuishauri Serikali kuendelea kuwekeza katika eneo hilo ili wataalamu wa Kitanzania wasiachwe nyuma na kasi ya dunia.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Profesa Maulilio Kipanyula alisema kuwa Programu ya Samia Scholarship Extended katika Sayansi ya Data, Akili Unde na Sayansi Shirikishi (SSE DS/AI+) ina lengo kuu la kujenga uwezo wa nchi katika masuala ya Sayansi ya Data, Akili Unde na Sayansi Shirikishi ili kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali kwa kuzalisha rasilimali watu mahiri.

Aidha alisema kuwa malengo mahususi pia ni kuwaandaa wahitimu wa Kidato cha Sita wenye ufaulu wa juu kitaaluma, kiteknolojia na kiuongozi kupitia kambi ya mafunzo ya miezi kumi, ikiwemo maandalizi ya mitihani ya kimataifa ya lugha na ya Hisabati, kuwezesha maombi maalum ya kujiunga na vyuo vya nje ya nchi.

"Programu hii inakabiliwa na changamoto ya gharama kubwa za masomo nje ya nchi na upatikanaji wa ufadhili, ambapo Wizara imeweka kipaumbele kwa nafasi zenye ufadhili kamili na punguzo kubwa la ada, huku ikiendelea kufuatilia ufadhili wa asilimia 100 kupitia wadau wa elimu," alisisitiza Profesa Kipanyula.









Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: