Articles by "WIZARA YA ELIMU"
Showing posts with label WIZARA YA ELIMU. Show all posts




Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefanya marekebisho ya ratiba ya upimaji na mitihani ya Taifa kwa mwaka 2026, kwa lengo la kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na uwezekano wa mvua kubwa za El Nino zinazotarajiwa katika baadhi ya maeneo nchini.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Septemba 25, 2026, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya Serikali kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa na kutathmini athari zinazoweza kujitokeza katika uendeshaji wa upimaji na mitihani ya Taifa.

Amesema kwa mujibu wa utabiri rasmi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, kuna uwezekano wa kutokea kwa El Nino yenye nguvu, huku mvua zikitarajiwa kuanza katika baadhi ya maeneo mwezi Oktoba 2026 na kuwa nyingi zaidi mwezi Novemba 2026, hali ambayo inaweza kuathiri usafiri na kufikika kwa baadhi ya vituo vya mitihani.

Ameeleza kuwa kwa kuzingatia jiografia ya nchi na uwezekano wa baadhi ya maeneo kukumbwa na mafuriko, changamoto za usafiri na athari nyingine zinazoweza kusababishwa na hali ya hewa, Wizara kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani la Tanzania imefanya marekebisho ya ratiba ya upimaji na mitihani ya Taifa.

Kwa mujibu wa ratiba iliyorekebishwa, Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili Ngazi ya Shule utafanyika Oktoba 7 hadi 8, 2026, wakati Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne utafanyika Oktoba 5 hadi 6, 2026.

Aidha, Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili utafanyika Oktoba 12 hadi 23, 2026, huku Mitihani ya Kidato cha Nne ikifanyika kuanzia Oktoba 19 hadi Novemba 6, 2026.

Amesema marekebisho hayo yanalenga kuhakikisha usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi, maafisa na wadau wengine wanaohusika na uendeshaji wa mitihani, pamoja na kulinda mitihani, vifaa na nyaraka muhimu.

Ameongeza kuwa iwapo ratiba ya awali ingeendelea na mvua kubwa zikajitokeza mwezi Novemba 2026, changamoto zingeweza kujitokeza katika usafirishaji na ufikishaji wa mitihani, vifaa na nyaraka muhimu katika vituo, huku wanafunzi na wasimamizi wakikabiliwa na ugumu wa kufika kwa wakati kutokana na mafuriko na uharibifu wa barabara.

Wizara imeendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa hali ya hewa na kuchukua hatua stahiki kwa kushirikiana na mamlaka na taasisi husika, ili kuhakikisha upimaji na mitihani ya Taifa inafanyika kwa utaratibu unaofaa, huku usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi na wadau wengine ukipewa kipaumbele.








 


Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha sekta ya elimu kwa kuongeza miaka ya elimu ya lazima, kupanua fursa za elimu ya sekondari na kuimarisha mafunzo ya ufundi ili kuwapa vijana uwezo wa kushiriki kikamilifu katika soko la ajira.

Akizungumza Septemba 02, 2026 jijini Dodoma na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema maandalizi ya utekelezaji wa miaka 10 ya elimu ya lazima kuanzia mwaka 2028 yanaendelea, hatua itakayohitaji miundombinu, walimu na nafasi za kutosha katika shule za sekondari.  

Prof. Mkenda amebainisha kuwa mpango huo utasababisha ongezeko kubwa la wanafunzi watakaoingia sekondari, hivyo Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha wanafunzi wote wanaostahili wanapata nafasi ya kuendelea na masomo.  

Aidha, ameongeza kuwa  Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa elimu wenye mikondo ya elimu ya jumla na elimu ya amali, ili wanafunzi wapate maarifa na stadi zinazowawezesha kuajirika au kujiajiri.  

Katika mazungumzo hayo, Prof. Mkenda ameeleza kuwa Serikali inajenga vyuo vya ufundi katika maeneo mbalimbali na kuimarisha mafunzo ya ufundi ili kukidhi mahitaji ya vijana na uchumi wa Taifa.  

Prof. Mkenda ameongeza kuwa Serikali inawekeza katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati pamoja na teknolojia mpya kama akili bandia (AI), ujifunzaji wa mashine na usalama wa mtandao, ili kuandaa wataalamu wa kisasa.  

Amesisitiza  umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi katika kupanua fursa za elimu, hususan katika ujenzi wa miundombinu na utoaji wa elimu ya amali.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa Serikali inatazama uwezekano wa kuboresha vivutio vya kisera vitakavyoongeza uwekezaji wa sekta binafsi katika elimu.  

Naye Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Mhe. Marianne Young, amepongeza juhudi za Tanzania na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika elimu na na mafunzo ya  ufundi, ikiwemo kuunganisha taasisi za Tanzania na vyuo vikuu vya Uingereza katika maeneo ya teknolojia ya kisasa na mazingira.

 


Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo,akizungumza wakati akiongoza kikao cha tafakuri cha uongozi na watumishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kilicholenga kutathmini utekelezaji wa majukumu yaliyokabidhiwa kwa wizara.

Na.Mwandishi Wetu

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amewapongeza watumishi wa wizara hiyo kwa kazi kubwa na mafanikio waliyoyapata katika mwaka wa fedha uliopita, huku akiwataka kuendelea kuyasema kwa ujasiri mafanikio hayo yaliyoiwezesha sekta ya elimu kung’aa kitaifa na kimataifa.

Prof. Nombo amesema mafanikio hayo yametokana na uongozi imara wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, na Naibu Waziri, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, pamoja na ushirikiano wa Wakurugenzi, Wakuu wa Idara na watumishi wote.

Prof. Nombo amesema hayo Septemba 1, 2026 jijini Dodoma wakati alipoongoza kikao cha tafakuri cha uongozi na watumishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kilicholenga kutathmini utekelezaji wa majukumu yaliyokabidhiwa kwa wizara. Amewashukuru watumishi kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yao na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano katika kufikia malengo ya wizara.

Aidha, Prof. Nombo amesema mabadiliko makubwa yanayoendelea katika sekta ya elimu yanatokana na utekelezaji wa sera mpya ya elimu, ambayo inalenga kuandaa wahitimu wenye ujuzi, kuboresha matokeo ya kujifunza na kuimarisha mfumo mzima wa elimu nchini. Amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu kupitia ujenzi wa miundombinu, ajira za walimu, mafunzo ya watumishi na fursa mbalimbali za kitaaluma.

Katika kikao hicho, Katibu Mkuu amekumbusha wajibu mkubwa wa Wizara katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akieleza kuwa takribani asilimia 40 ya masuala yaliyomo kwenye dira hiyo yanahusu sekta ya elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu. Ameongeza kuwa utekelezaji wa elimu ya lazima kwa miaka 10 na maandalizi ya kupokea kundi la wanafunzi la double cohort mwaka 2028 ni miongoni mwa majukumu makubwa yanayohitaji maandalizi ya mapema na ushirikiano wa pamoja.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, amewataka watumishi kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano, weledi, nidhamu na uadilifu, akisema misingi hiyo ni muhimu katika kuimarisha utendaji kazini. Prof. Mushi amesema hayo Septemba 1, 2026 jijini Dodoma wakati akifunga kikao cha tafakuri cha watumishi wa wizara hiyo.

Amesema mafanikio ya wizara yanatokana na mchango wa kila mtumishi, hivyo kuna umuhimu wa kuongeza ubunifu katika utendaji huku sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma ikizingatiwa. Pia amesisitiza umuhimu wa kuzingatia usalama wa taarifa za Serikali na kuhakikisha wananchi wanahudumiwa kwa furaha, ufanisi na weledi, huku akiwataka watumishi kutumia mafunzo waliyopata kuongeza tija na kuhamasisha utamaduni wa kuendelea kujifunza katika kila ngazi ya utumishi.

Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Edith Rwiza, amesema kikao cha uongozi na watumishi kimetoa fursa ya kutafakari kwa pamoja, kujenga mshikamano na kubadilishana uzoefu kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi.

Amesema kikao hicho pia kililenga kutafakari mafanikio, changamoto na mafunzo yaliyopatikana katika utekelezaji wa mipango na majukumu ya wizara katika mwaka uliopita.

Dkt. Rwiza amesema kikao hicho kimewapa watumishi nafasi ya kujitathmini kwa kuzingatia uhalisia wa utendaji kazi na kujadili namna bora ya kuhakikisha malengo ya wizara yanafikiwa kwa ufanisi.

Ameongeza kuwa washiriki wamepata fursa ya kutazama kwa pamoja changamoto za rasilimali na kubaini namna ya kuongeza ufanisi ili kupata matokeov makubwa zaidi kwa kutumia rasilimali zilizopo, huku wakielekezwa kuimarisha mshikamano na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao.



Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo,akizungumza wakati akiongoza kikao cha tafakuri cha uongozi na watumishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kilicholenga kutathmini utekelezaji wa majukumu yaliyokabidhiwa kwa wizara.

  

Sehemu ya Watumishi wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo (hayupo pichani) wakati akiongoza kikao cha tafakuri cha uongozi na watumishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kilicholenga kutathmini utekelezaji wa majukumu yaliyokabidhiwa kwa wizara.

 

Sehemu ya Watumishi wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo (hayupo pichani) wakati akiongoza kikao cha tafakuri cha uongozi na watumishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kilicholenga kutathmini utekelezaji wa majukumu yaliyokabidhiwa kwa wizara.

  

Sehemu ya Watumishi wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo (hayupo pichani) wakati akiongoza kikao cha tafakuri cha uongozi na watumishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kilicholenga kutathmini utekelezaji wa majukumu yaliyokabidhiwa kwa wizara.

 

Sehemu ya Watumishi wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo (hayupo pichani) wakati akiongoza kikao cha tafakuri cha uongozi na watumishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kilicholenga kutathmini utekelezaji wa majukumu yaliyokabidhiwa kwa wizara.        

 



Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) inaendelea kushiriki katika Maonesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika katika Viwanja vya Usagara jijini Tanga, ikitumia jukwaa hilo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya mionzi na fursa zinazotokana na teknolojia ya nyuklia katika kuchochea maendeleo ya Taifa.

Maonesho hayo, yanayoratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, yanawakutanisha taasisi za Serikali, taasisi za elimu na utafiti, wabunifu, wanafunzi, wataalamu pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu, sayansi na teknolojia.

Katika banda la TAEC, wananchi, wanafunzi na wadau mbalimbali wanaendelea kupata elimu kuhusu jukumu la Tume la kusimamia na kudhibiti matumizi salama ya mionzi nchini, pamoja na mchango wa teknolojia ya nyuklia katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, kilimo, mifugo, maji, viwanda, migodi, utafiti na nishati.

Ushiriki wa TAEC katika maonesho hayo pia unatoa fursa kwa wanafunzi na vijana kufahamu taaluma mbalimbali zinazohusiana na teknolojia ya nyuklia na umuhimu wa kujikita katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM) ili kujenga kizazi cha wataalamu kitakachosaidia Taifa kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Akifungua rasmi maonesho hayo Agosti 18, 2026, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alisisitiza umuhimu wa elimu, ujuzi, sayansi, teknolojia na ubunifu katika kujenga uchumi wa kisasa na kuongeza uwezo wa Taifa kutumia maarifa na teknolojia katika kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo.

Katika muktadha huo, ushiriki wa TAEC unaunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha sayansi na teknolojia zinatumika moja kwa moja katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Teknolojia ya nyuklia ina matumizi mapana yenye manufaa kwa wananchi, ikiwemo katika uchunguzi na tiba ya magonjwa, kuongeza tija katika kilimo na mifugo, usimamizi wa rasilimali za maji, shughuli za viwandani na migodini, utafiti wa kisayansi pamoja na sekta ya nishati.

Wananchi wanaotembelea banda la TAEC pia wanapata nafasi ya kuzungumza moja kwa moja na wataalamu, kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu usalama wa mionzi, udhibiti wa vyanzo vya mionzi na matumizi ya teknolojia ya nyuklia kwa madhumuni ya amani na maendeleo.

TAEC itaendelea kutoa elimu na kuhamasisha matumizi salama ya mionzi na teknolojia ya nyuklia kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

“Mionzi kwa Matumizi Salama na Teknolojia ya Nyuklia kwa Maendeleo ya Taifa.”






 

Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) Profesa Haruni Mapesa akisaini Kitabu wakati alipotembelea Banda la TIA katika Wiki ya Elimu Kitaifa ,Ujuzi na Ubunifu inayoendelea katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara,Jijini Tanga.
Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) Profesa Haruni Mapesa akipata maelezo kutoka Mkuu wa Sehemu - Ukuzaji na Uendelezaji wa wanafunzi kitaaluma na kitaalam wa TIA Imani  Matonya  kuhusiana na bunifu mbalimbali wa wanafunzi na wahitimu was TIA  walizoleta katika Maonesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu ,Ujuzi na Ubunifu  Kwakati Mkuu wa Chuo hicho  alipotembelea Banda la TIA katika Wiki ya Elimu Kitaifa ,Ujuzi na Ubunifu inayoendelea katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara,Jijini Tanga.
Baadhi ya Wahitimu na Wanafunzi wa TIA  ambao wenye bunifu ambazo zimesimamiwa TIA kwenye maonesho ya Wiki ya Elimu Kitaifa ,Ujuzi na Ubunifu inayoendelea katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara,Jijini Tanga.

 




Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) Profesa Haruni Mapesa, amesema maonyesho ya elimu, ujuzi na ubunifu ni jukwaa muhimu kwa taasisi za elimu kuonyesha kazi zinazofanywa na wanafunzi pamoja na kuwafungulia vijana fursa mbalimbali za kujifunza na kuendeleza vipaji vyao.

Profesa Mapesa ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kuhusu ushiriki wa chuo hicho katika maonyesho ya elimu, ujuzi na ubunifu yanayoendelea mkoani Tanga, akimpongeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, pamoja na Wizara hiyo kwa kuendelea kusimamia maonyesho hayo na kuwa na mafanikio.

Amesema maonyesho hayo yamekuwa na umuhimu kwa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kuwa yanatoa nafasi ya kuonyesha programu zinazotolewa na chuoni ikiwemo mafunzo yanayohusiana na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), pamoja na kazi za ubunifu zinazofanywa na wanafunzi.

“Tunajivunia kupata fursa ya kuonyesha kazi za vijana wetu, ubunifu wao katika sayansi, teknolojia na maeneo mbalimbali. Ubunifu huu umekuwa na mguso mkubwa na tunaamini siku zijazo utakuwa na matokeo makubwa zaidi,” amesema Profesa Mapesa.

Amesema chuo kina mpango wa kuendeleza ubunifu wa wanafunzi kwa kuunganisha kazi hizo na watumiaji na wadau wakubwa ili zitumike zaidi katika shughuli za uzalishaji na kuchangia maendeleo ya uchumi.

Profesa Mapesa amesema maonyesho hayo pia yamekuwa fursa kwa vijana wanaotaka kujiunga na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kupata taarifa kuhusu programu mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho, huku baadhi yao wakipata huduma za usajili na maelekezo ya kujiunga na programu hizo moja kwa moja katika banda la chuo.

Ameeleza kuwa chuo kinatoa programu za umahiri, shahada ya kwanza, pamoja na diploma, huku akiwataka wananchi wa Tanga kutembelea maonyesho hayo, hususan banda la Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, ili kupata fursa ya kujifunza zaidi kuhusu huduma na programu zinazotolewa na taasisi hiyo.

Aidha, amesema chuo hicho kina nafasi ya kipekee katika kuhifadhi na kutangaza historia ya Muasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kupitia machapisho, kumbukumbu na hotuba zake ambazo, amesema, zimekuwa na mchango mkubwa katika historia ya Tanzania na Afrika.

Profesa Mapesa amewashukuru waandaaji wa maonyesho hayo pamoja na vyombo vya habari kwa kuendelea kuhabarisha umma kuhusu shughuli za maonyesho na kazi zinazofanywa na taasisi za elimu. Pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusisitiza umuhimu wa elimu, ujuzi na ubunifu katika maendeleo ya taifa.

Amesema uwekezaji unaoendelea katika elimu, ujuzi na ubunifu ni muhimu katika kujenga Taifa lenye vijana wenye uwezo wa kutumia maarifa na teknolojia kutatua changamoto na kuchangia maendeleo ya Tanzania.

 


Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeandaa mtaala maalum wa kozi fupi za recycling kwa lengo la kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika sekta ya taka na kuongeza thamani ya taka zinazoweza kurejelewa.

Hayo yameelezwa Agosti 15, 2026 jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Mohammed Omari, wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo katika Chuo cha VETA wilaya ya Bahi.

Amesema hatua hiyo imekuja baada ya tafiti kubaini kuwa baadhi ya vijana wanaojihusisha na shughuli za taka wanakabiliwa na changamoto za kiafya na kiusalama, hivyo kuhitajika kwa mtaala mahsusi utakaowawezesha kukabiliana na mazingira ya kazi.

Dkt. Omari amesema mtaala huo umeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya wadau katika mnyororo wa thamani wa taka, kuanzia ukusanyaji hadi uchakataji, kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais, sekta binafsi, vyuo vya walimu na waajiri.

Aidha, amesema VETA inaendelea kushirikiana na wataalamu wa sekta mbalimbali kuunganisha ujuzi wa vitendo na mafunzo ya vyuoni. Ametolea mfano ushirikiano na mtaalamu wa samani, Edo Sama, anayerejeleza zaidi ya asilimia 50 ya mbao zilizokuwa zikitupwa na kuzitumia kutengeneza samani, hivyo kuongeza thamani ya taka na kupunguza upotevu wa rasilimali.

Ameongeza kuwa VETA inaendelea kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, ikiwemo kampuni ya Hans Paul ya Arusha inayotengeneza magari ya utalii, ili kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi wa vitendo. Amesema hatua hiyo inaendana na msisitizo wa Serikali wa kushirikisha sekta binafsi katika kukuza ujuzi na ajira kwa vijana.

 


Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Jumla ya wanafunzi 10 waliomaliza kidato cha sita na kupata alama za juu katika tahasusi za PCM, PGM na PMC, wamepata ufadhili wa kwenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Urusi (RUDN University) kilichopo jijini Moscow, nchini Urusi.

Ufadhili huo umepatikana kufuatia ziara rasmi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya  nchini humo mnamo mwezi Juni, 2026 ambapo chuo hicho ndicho kilichomtunuku Shahada ya Uzamivu ya Heshima ya Udaktari (Honoris Causa).

Akizungumza na Waandishi wa Habari Agosti 13, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa wanafunzi hao wamepata ufadhili huo kupitia utaratibu wa Samia Scholarship Extended.

"Wanafunzi hao wanatarajiwa kufanya kambi ya mafunzo nchini Urusi kwa takriban miezi 10, Serikali ya Urusi itagharamia mafunzo hayo kwa asilimia 80 na Serikali ya Tanzania itagharamia asilimia 20, watakapoanza mafunzo ya chuo kikuu mnamo Septemba 2027, Serikali ya Urusi itagharamia kwa asilimia 100", amesema Prof. Mkenda.

Akifafanua juu ya upatikanaji wa wanafunzi hao, Mhe. Prof. Mkenda amesema kuwa wamechukua wale waliofaulu vizuri baada ya wale 50 wa mwanzo, hivyo wamechukua kuanzia mwanafunzi wa 51 hadi 60 ambapo kati yake, wanafunzi nane wametoka katika shule za serikali na wanafunzi wawili wametoka katika shule za binafsi.

Akizungumza kuhusu wanafunzi 50 waliochaguliwa hivi karibuni, amesema kuwa wote wamekubali kupokea ufadhili huo wa kusoma nje ya nchi na wanatarajia kuanza kambi ya mafunzo mnamo Septemba 14, 2026 kwa muda usiozidi miezi 10 katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela - Arusha (NM-AIST) kabla ya kwenda katika vyuo hivyo vya nje ya nchi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkenda ametoa rai kwa wanafunzi wanaopata ufadhili wa kusoma nje ya nchi kufanya vizuri kwenye masomo yao ili kuongeza ushawishi kwa nchi hizo kutoa ufadhili kwa wanafunzi wengine zaidi hali itakayosaidia mikopo ya elimu ya juu inayotolewa kwa wanafunzi nchini kuwafikia wanafunzi wengi zaidi.

 


Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Haruni  Mapesa amewataka viongozi wapya wa Serikali ya Wanafunzi (MASO) kutambua kuwa Uongozi ni utumishi wa kuwatumikia watu na si kutumikiwa, kwani kazi ya kiongozi ni kuwa tayari muda wote kutatua changamoto mbalimbali.

Mapesa ameyasema hayo wakati wa hafla fupi ya kuwapisha viongozi wapya wa Serikali ya Wanafunzi (MASO) kwa mwaka 2026/27 pamoja na mambo mengine amepongeza Uongozi wa Serikali  iliyomaliza muda wake iliyokuwa ikiongozwa na Magashi Magina  kuwa walizingatia Weledi wa hali ya Juu.

Mkuu huyo wa Taasisi ameitaka Serikali mpya kuzingatia misingi ya Uongozi, na kuwa na namna bora ya kutatua changamoto ikiwa ni pamoja na kushirikiana vyema na Serikali ya Wanafunzi ambayo imemaliza muda wake, huku akiwaahidi ushirikiano wa dhati kutoka kwa Uongozi wa Chuo.

Kwa upande wake, Rais aliyemaliza muda wake Magashi Magina ameishukuru Menejimenti ya chuo kwa ushirikiano alioupata katika kipindi chote cha uongozi wake, ameeleza kuwa mafanikio yote yaliyopatikana yalitokana na uwazi na utayari wa Menejimenti kusikiliza na kutatua Changamoto mbalimbali za Wanafunzi jambo lililorahisisha utendaji kazi wa serikali yake.

Nao, Viongozi wapya walioapishwa kuiongoza Serikali ya Wanafunzi , Rais ni Samir Naseer na Makamu wa Rais  Julieth Mandia  wametoa shukrani za dhati kwa Wanafunzi wote kwa kuonyesha imani kwao na kuwachagua kuongoza Serikali ya wanafunzi ambapo wameahidi kuongozi kwa Uadilifu, Amani, mshikamano kwa  kushirikiana na Menejimenti ya Chuo pamoja na Serikali ya Wanafunzi iliyomaliza muda wake.

 

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano na Masoko

CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE

28.05.2026

 


Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Haruni Mapesa amewataka Wafanyakazi wa MNMA kuendelea kufanya kazi kwa furaha, Uadilif na kuweka maslahi ya Taasisi mbele kwa kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa Wanafunzi na Watumishi kwa moyo na kufanya hivyo ni utumishi kama ilivyo utumishi wa Mungu, kwani kila kazi unayoifanya kwa ajili ya watu basi hiyo ni kazi ya Mungu.

Prof.Mapesa ameyasema hayo leo wakati wa kuwapongeza Watumishi hodari katika uwajibikaji wa utumishi wa umma kwa mwaka 2025/2026 kwa wale wote waliopata fursa ya kuwa Wafanyakazi bora, na kusisisitiza kuwa Watumishi waendelee kufanya kazi kwa kuzingatia Misingi ya utumishi wa umma na huo ndiyo uwe utamaduni wa kila siku.

Kwa upande wake Naibu Mkuu wa Chuo anaesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaaluma Prof. Richard Kangalawe amesema Ushindi ni heshima huku akiwataka watumishi wengine kuendeela kuwajibika katika nafasi zao kwa lengo la kutimiza malengo ya Taasisi.



Naye Naibu Mkuu wa Chuo anaesimamia Mipango, Fedha na Utawala Prof.Evaristo Haulle alisema mchakato wa kupata Mfanyakazi bora ulikuwa ni wa huru na haki ambapo vigezo mbalimbali vilizingatiwa ikiwemo Nidhamu ya mtumishi , Utendaji kazi wa mtumishi,(PEPMIS) na Mienendo mbalimbali, hivyo dosari zote zilizojitokeza zilishughulikiwa ipasavyo.

Nao viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Debora Donati wa THTU na kwa upande wa  RAAWU  Hashimu Mtongola  kwa pamoja wameipongeza Menejimenti kwa hafla hiyo fupi ambayo inatoa motisha na kuongeza morali ya kazi kwa Wafanyakazi na pia wameomba uongozi ufikirie kujumuisha Wafanyakazi wote kwa hafla ya namna hiyo wakati mwingine.



Wafanyakazi bora wa Taasisi kwa mwaka huu Filbert Nyakasi upande wa Wanataaluma  na Amedeus Mchau upande wa Waendeshaji wameshukuru uongozi kwa kutambua jitihada zao na mchango wao katika kutimiza majukumu ya kila siku na wameahidi kuendelea kufanya kazi kwa Uadilifu, Nidhamu kwa  kushirikiana na Wafanyakazi wengine.


Wafanyakazi wote hodari wamentunukiwa vyeti vya kutambuliwa na zawadi ya fedha, ambapo zoezi limejumuisha Wafanyakazi wote bora wa Kampasi ya Kivukoni, Karume na Pemba.


Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano na Masoko

ChUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE

25.05.2026

 


Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Prof. Haruni Mapesa amewataka wanataaluma kuacha tabia ya kuchapisha makala zao kwenye Majarida yasiyotambulika ili kuzuia upotezaji wa nguvu na rasilimali za uchapishaji wa Tafiti.

Prof. Mapesa ameyasema hayo wakati akifungua Semina ya Uwasilishaji wa Makala Mijadala za a Kitaaluma iliyoandaliwa na Idara ya Lugha na Fasihii Chuoni hapo hafla iliyofanyika katika Kampasi ya Kivukoni jijini Dar es salaam.

Mkuu huyo wa Chuo amesema kuwa sasa Tasisi ipo katika hatua za ukuaji ikiwemo kuidhinishwa kwa Kitivo cha Uchumi na Biashara, ambapo chuo kimetenga kiasi cha shilingi milioni 120 kwa ajili ya tafiti na kuna mpango wa kuongeza fedha hizo ili kuwekeza zaidi kwa wahadhiri watakaofanya tafiti mbalimbali.

Naibu Mkuu wa Chuo anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaaluma Prof. Richard Kangalawe amekipongeza Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii kupitia Idara ya Lugha na Fasihi kwa kuandaa semina hiyo na kuwahimiza washiriki kutumia fursa hiyo kuimarisha mawazo ya kitafiti, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha tafiti zote zinasajiliwa rasmi na machapisho yawe yenye ubora wa hali. 

Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala Prof. Evaristo Haulle amewataka Wanataaluma kubadilika na kuanza kufikiria namna ya kuchangia asilimia 30 ya mapato ya ndani kupitia Tafiti na Miradi wanayoifanya badala ya kutegemea rasilimali na fedha za ndani za chuo pekee.

Akiwasilisha taarifa ya Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii, Mtiva wa Kitivo hicho Dkt. Luzabeth Kitali ameishukuru Menejimenti ya Chuo kwa Maelekezo na Ushauri na kuahidi kuwa idara yake imejipanga kikamilifu kusimamia ubora wa Tafiti, kuendeleza Uandishi ikiwa ni pamoja na kushiriki katika makongamano ya kitaaluma.


 

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano na Masoko

CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE

21.05.2026