Wanafunzi wanaotaka kujiunga na Chuo Kikuu cha Johannesburg (UJ) nchini Afrika Kusini kupitia ufadhili wa Samia Scholarship sasa wanatakiwa kuwa na ufaulu wa Daraja A,katika somo la Kiingereza kwenye mtihani wa Kidato cha Nne.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ambaye amesema licha ya mwanafunzi kuwa na ufaulu mkubwa katika masomo ya Sayansi kama Fizikia, Kemia na Hisabati, kigezo cha lugha ya Kiingereza ni lazima ili kukidhi masharti ya udahili ya vyuo vya kimataifa.

"Vyuo Vikuu vya Kimataifa vina masharti maalumu ya lugha, hivyo lazima wanafunzi lazima wajidhatiti, waimarishe Sayansi na pia Kiingereza ili waweze kuhimili ushindani wa masomo nje ya nchi," amesema Prof. Mkenda.

Amesema Serikali inaendelea kuwaandaa wanafunzi kujiunga na vyuo mbalimbali vya kimataifa, vikiwemo Chuo Kikuu cha Johannesburg na vyuo vikuu vya Ireland, na wanapaswa kuzingatia taratibu zote za udahili na ufadhili.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Samia Scholarship, Profesa Emeritus Yunus Daudi Mgaya, amesema Wizara imeingia makubaliano na Chuo Kikuu cha Johannesburg kusomesha vijana wa Kitanzania katika fani za Sayansi ya Data (Data Science), Akili Mnemba (Artificial Intelligence) na fani zinazohusiana.

Alisema mwaka huu Serikali imepeleka wanafunzi 16 katika chuo hicho na inatarajia kupeleka kundi lingine la wanafunzi 16 au zaidi kulingana na maendeleo ya majadiliano.

Prof. Mgaya amefafanua kuwa walengwa wakuu wa programu hiyo ni wanafunzi wa mchepuo wa Fizikia, Kemia na Hisabati (PCM) au Fizikia, Kemia na Kompyuta (PGM/PNC) wenye ufaulu wa juu, lakini lazima pia watimize kigezo cha Kiingereza kwa kufanya mitihani ya kimataifa ya lugha na kufaulu kwa viwango vinavyotakiwa.

"Kuna wanafunzi wana uwezo mkubwa sana wa Sayansi lakini changamoto ya lugha inawanyima nafasi. Ndio maana tunawasihi walimu wa shule za msingi na sekondari kuimarisha ufundishaji wa Kiingereza tangu ngazi za chini," alisema.

Ameongeza kuwa wanafunzi wanaolenga vyuo vya Ireland kama vile Chuo Kikuu cha Limerick, Galway na University College Dublin nao wanapaswa kujiandaa kwa kuzingatia vigezo hivyo vya lugha.

Lengo la Serikali amesema, ni kuhakikisha wanufaika wa Samia Scholarship wanakuwa na uwezo wa kutosha kitaaluma na ki-lugha ili waweze kuhimili mazingira ya masomo ya nje na hatimaye kurejea kutumia maarifa yao kuchangia maendeleo ya Tanzania.

















Share To:

Post A Comment: