NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) zimesaini Hati ya Makubaliano ya ushirikiano wa miaka mitano, unaolenga kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa kutumia teknolojia ya kidijitali.
Katika hatua ya awali, UCSAF imetenga Sh milioni 500 kwa ajili ya mradi wa majaribio wa siku 30, kuanzia Oktoba 28 hadi Novemba 25, 2026, utakaohusisha kubadilisha vitabu vinne vya kiada vya Kidato cha Tatu kuwa maudhui ya kidijitali.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Bw. Mulembwa Denis Munaku, alisema ushirikiano huo utasaidia kuongeza upatikanaji wa maarifa, kuboresha ubora wa elimu na kupunguza tofauti za fursa za kujifunza kati ya wanafunzi wa mijini na vijijini.
Alisema UCSAF imewezesha shule za Serikali zaidi ya 1,121 kupata vifaa vya TEHAMA, huku walimu 4,410 wa sekondari wakipatiwa mafunzo ya matumizi ya teknolojia katika ufundishaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba, alisema ushirikiano huo utaimarisha matumizi ya teknolojia katika elimu na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Alisema vitabu vitakavyowekwa katika mfumo wa kidijitali ni Business Studies, Historia ya Tanzania na Maadili, English na Mathematics, ambavyo vitakuwa na video, sauti, vielelezo shirikishi na mazoezi ya kidijitali.
Dkt. Komba aliongeza kuwa makubaliano hayo yatahusisha pia uboreshaji wa miundombinu ya TEHAMA, majukwaa ya usambazaji wa maudhui na maandalizi ya miongozo ya mafunzo ya kidijitali kwa walimu na jamii.
Alisema programu hiyo itazingatia mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu na kupanua fursa za elimu kwa wanafunzi wa mijini na vijijini.
Viongozi hao walisema ushirikiano huo unatarajiwa kuimarisha ujuzi wa kidijitali na kuwaandaa wanafunzi kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.

Post A Comment: