SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetoa tahadhari kwa wananchi kuhusu matumizi ya bidhaa zisizosajiliwa na zisizokidhi viwango vya ubora, likieleza kuwa baadhi ya bidhaa hizo zina viambato vinavyoweza kusababisha madhara makubwa kiafya, ikiwemo saratani na kuvuruga mfumo wa homoni mwilini.

TBS imetoa tahadhari hiyo kupitia maonesho ya Wiki ya Mwanakatavi yanayofanyika mkoani Katavi, ambapo imeonesha sampuli za bidhaa zisizokidhi viwango ili kuwawezesha wananchi kuzitambua na kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi yake.

Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa TBS Kanda ya Magharibi, Hamisi Seleleko, amesema baadhi ya bidhaa hizo huingia sokoni kwa njia za magendo na kuuzwa kwa kificho, huku nyingine zikitumia picha na maelezo ya kupotosha kuhusu ubora na sifa zake.

Amesema matumizi ya bidhaa hizo kwa muda mrefu yanaweza kusababisha madhara mbalimbali mwilini, yakiwemo kupata saratani na mabadiliko katika mfumo wa homoni, ambayo yanaweza kuleta athari kubwa kwa afya ya mtumiaji.

Seleleko amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo, TBS imekuwa ikifanya ukaguzi katika maduka na viwanda vilivyopo mkoani Katavi na maeneo mengine ya Kanda ya Magharibi kwa lengo la kudhibiti usambazaji na uuzaji wa bidhaa zisizokidhi viwango.

Ameeleza kuwa ukaguzi uliofanyika tangu mwaka 2020, wakati ofisi za TBS Kanda ya Magharibi zilipoanza kazi, umeonesha kupungua kwa bidhaa hizo sokoni, hali inayoashiria mafanikio ya juhudi za udhibiti zinazofanywa na shirika hilo.

Hata hivyo, amesema TBS itaendelea na ukaguzi na doria katika maeneo mbalimbali hadi kuhakikisha bidhaa zisizokidhi viwango zinaondolewa kabisa sokoni.

Aidha, amewataka wananchi kuwa makini wanaponunua bidhaa, kuhakikisha zimesajiliwa na zinakidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa, huku akiwahimiza kutoa taarifa wanapobaini bidhaa zinazotiliwa shaka.

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: