London, Uingereza, Novemba 6, 2026
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi, leo Novemba 6, 2026, ameshiriki Mkutano wa Uwekezaji na Wawekezaji pamoja na wadau wa sekta ya utalii nchini Uingereza, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa ziara yake jijini London.
Mkutano huo uliwakutanisha wawekezaji, wadau wa utalii na waendeshaji wa shughuli za utalii (Tour Operators) kutoka Uingereza kwa lengo la kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania, kuwavutia wawekezaji kuwekeza katika sekta ya utalii, pamoja na kuitangaza Tanzania kama moja ya maeneo bora ya utalii duniani.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Dkt. Kijaji aliwashukuru wadau wote waliojitokeza na kusisitiza dhamira ya Serikali ya kuimarisha ushirikiano na wadau wa Uingereza ili kukuza uwekezaji, kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania na kuimarisha sekta ya utalii.
Aidha, amesema Uingereza ni soko muhimu la utalii kwa Tanzania, akibainisha kuwa kuanza kwa safari za moja kwa moja za Shirika la Ndege la British Airways kuja Tanzania kuanzia mwaka 2027 kutakuwa chachu muhimu katika kukuza utalii kwa kurahisisha usafiri na kuongeza muunganiko kati ya nchi hizo mbili.
Katika mkutano huo, wadau walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali kuhusu fursa za uwekezaji, vivutio vya utalii na mazingira ya kufanya biashara nchini Tanzania, ambapo maswali yao yalijibiwa papo kwa papo na viongozi walioshiriki.
Mkutano huo pia umehudhuriwa na Mwakilishi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Joshua Nassari, Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Bw. Patrick Mwakalobo, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Dkt. Thereza Mugobi.
Mkutano huo umefanyika katika Hoteli ya Hyatt Churchill jijini London.















Post A Comment: