Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema matumizi ya Gesi ya Mitungi (LPG) ni miongoni mwa nyenzo muhimu katika kusukuma mbele Ajenda ya Taifa ya Nishati Safi ya Kupikia, hivyo Serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha nishati hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi.
Moja ya hatua zilizochukuliwa na Serikali ni kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika bidhaa za LPG ili kupunguza gharama za upatikanaji wake.
Amesema hayo leo, Novemba 24, 2026, katika Jukwaa la ARDA lililojikita kujadili Maendeleo ya Sekta ya LPG (ARDA LPG Forum 2026), jijini Dar es Salaam.
Amesema Tanzania imepiga hatua katika kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia kutokana na dhamira ya Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameipa ajenda hiyo kipaumbele katika utekelezaji wa sera na mikakati ya maendeleo ya Taifa.
Ameeleza kuwa mwezi Mei 2024, Serikali ilizindua Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034, unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Amefafanua kuwa LPG ni miongoni mwa teknolojia muhimu za nishati safi ya kupikia zinazochangia kufikiwa kwa malengo ya mkakati huo.
Aidha, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yameongezeka kutoka asilimia sita mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025, hatua inayoonesha mafanikio ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali na kuimarika kwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.
Vilevile, amesema kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Serikali inalenga kusambaza mitungi 52,000 ya gesi ya LPG yenye ujazo wa kilo sita kila mmoja kwa kaya mbalimbali nchini, hususan kaya zenye uwezo mdogo wa kiuchumi, ili kuongeza fursa ya wananchi kupata na kutumia nishati safi ya kupikia.
Amesisitiza kuwa juhudi hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuongeza upatikanaji na matumizi ya nishati safi ya kupikia, kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, pamoja na kuboresha afya, mazingira na ustawi wa wananchi.






Post A Comment: