Articles by "Habari"
Showing posts with label Habari. Show all posts

 


Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kimeandika historia mpya mkoani Manyara kwa kuzindua rasmi utoaji wa programu Shahada (Degree) katika Kampasi ya Babati. 

Hafla hiyo ya uzinduzi wa 'Bachelor of Accountancy with Information Technology' na "Bachelor of Computer Science' imeongozwa leo Agosti 24, 2026 na Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Daniel Sillo.

Mhe. Sillo amesema wahitimu wa programu hizo watakuwa sehemu ya kizazi kipya cha wabunifu watakaosadia kuimarisha matumizi ya Teknolojia katika sekta ya fedha, elimu, afya,biashara, kilimo, utalii, viwanda na utoaji wa huduma za serikali.

Mkuu wa Chuo IAA, Prof. Eliamani Sedoyeka amesema" hatua hii ni mkakati wa IAA kuunga mkono juhudi za Serikali kusogeza elimu bora kwa wananchi na kuhakikisha wanapata elimu inayokidhi mahitaji ya dunia ya sasa na baadaye".

Aidha, Prof. Eliamani Sedoyeka ametangaza kuwa wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza watapatiwa huduma ya hosteli bure  hatua inayolenga kupunguza gharama kwa wazazi na kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira salama na tulivu.

Kampasi ya Babati ilianza mwaka 2014 ikiwa na wanafunzi 272, sasa ina wanafunzi 728 na IAA  inalenga kuongeza idadi ya wanafunzi Babati hadi 6,000 ifikapo mwaka 2031.

Aidha, IAA inaandaa mkakati wa kuanzisha programu za  elimu inayozingatia ujuzi (skills-based curriculum) katika maeneo kama Kilimo biashara, Uchakataji wa chakula,Uchakataji wa ngozi,Uhandisi wa uchomeleaji.Lengo ni kuwaandaa vijana wenye ujuzi wa vitendo, kuongeza fursa za kujiajiri na kuajiriwa, na kuendana na mahitaji ya soko la ajira.

















Na Mwandishi Wetu - Zanzibar


Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga mazingira wezeshi kwa uchumi wa kidijitali Zanzibar kwa kuwezesha huduma ya intaneti katika mradi wa makazi wa Amani Residency, uliopo Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, kupitia huduma yake ya Faiba Mlangoni Kwako.

Mradi huo wa kisasa wa makazi ulizinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ukiwa ni sehemu ya uwekezaji unaolenga kuongeza fursa za makazi bora, biashara na utalii pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi Zanzibar.

Akizungumza kuhusu uwezeshaji huo, Meneja wa TTCL Zanzibar, Bi. Nasra Mugheiry, alisema TTCL imeweka mazingira ya mawasiliano ya kisasa katika Amani Residency ili kuwawezesha wakazi kupata huduma ya intaneti karibu na makazi yao na kutumia fursa mbalimbali zinazotokana na uchumi wa kidijitali.

“TTCL kupitia huduma ya Faiba Mlangoni Kwako imeweka mazingira wezeshi ya mawasiliano katika Amani Residency, kwa lengo la kuwawezesha wakazi kutumia intaneti katika shughuli zao za kila siku, ikiwemo kazi, biashara, elimu, mawasiliano na huduma mbalimbali za kidijitali. Tunataka kuhakikisha kwamba makazi ya kisasa yanaendana na mahitaji ya kisasa ya mawasiliano,” alisema Bi. Mugheiry.

Huduma hiyo inatarajiwa kuongeza thamani ya mradi huo kwa kuwawezesha wakazi kufanya shughuli mbalimbali kwa urahisi wakiwa majumbani. Kwa wakazi wanaofanya kazi kwa njia ya mtandao, wafanyabiashara, wanafunzi na familia, upatikanaji wa intaneti ya nyumbani utarahisisha matumizi ya mikutano ya mtandaoni, kujifunza, kufanya biashara kupitia majukwaa ya kidijitali, mawasiliano pamoja na huduma za Serikali mtandao.

Amani Residency, unaojengwa katika eneo la ekari 11, una jumla ya nyumba 82, zikiwemo villa 18 na apartment 64, pamoja na huduma mbalimbali za burudani na mapumziko. Uwepo wa huduma ya Faiba Mlangoni Kwako unaifanya miundombinu ya mawasiliano kuwa sehemu muhimu ya mazingira ya makazi hayo, sambamba na mahitaji ya maisha ya kisasa.

Kwa upande wa biashara, intaneti inayopatikana katika makazi inaweza kuwapa wakazi fursa ya kuendesha shughuli zao za kiuchumi kwa kutumia teknolojia, ikiwemo biashara za mtandaoni, masoko ya kidijitali, huduma za kifedha na mawasiliano ya kibiashara. Hali hiyo inaendana na juhudi za TTCL za kuchochea matumizi ya teknolojia na kuunganisha wananchi na fursa za uchumi wa kidijitali.

Aidha, uwezeshaji huo unaimarisha dhamira ya TTCL ya kusogeza huduma za mawasiliano kwa wananchi katika maeneo wanayoishi na kufanya shughuli zao, kwa kuzingatia kwamba intaneti imekuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku na kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kwa TTCL, kuwezesha Amani Residency kwa huduma ya Faiba Mlangoni Kwako ni zaidi ya kuunganisha makazi na intaneti; ni hatua ya kujenga mazingira ambayo yanawawezesha wananchi kuishi, kufanya kazi, kujifunza, kuwasiliana na kufanya biashara kwa kutumia teknolojia, sambamba na juhudi za taifa za kujenga uchumi unaotegemea zaidi huduma na fursa za kidijitali.





Wananchi wa Mkoa wa Tanga na mikoa jirani wanahamasishwa kushiriki katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ubunifu na Ujuzi, itakayofanyika kuanzia tarehe 15 - 24 Agosti 2026 katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga, ili kujifunza, kubadilishana maarifa na kutumia fursa mbalimbali za elimu, ujuzi na ubunifu.

Akizungumza Agosti 14, 2026, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Rashid Kassim Mchata, amesema maonyesho hayo yatashirikisha taasisi zaidi ya 300 pamoja na wadau wa sekta ya elimu, sayansi na teknolojia. Aidha, kutakuwa na mashindano ya ubunifu na ujuzi katika fani mbalimbali ikiwemo ushonaji, ususi, umeme na mengineyo, ambapo washindi wa kitaifa watapata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa.

Mchata ameongeza kuwa wadhamini mbalimbali wakiwemo mabenki wamejitokeza kudhamini miradi ya ubunifu na kuunga mkono wajasiriamali chipukizi.

Kwa upande wake, Prof. Ladislaus Mnyone, Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, alisema lengo kuu la wiki hiyo ni kuwaleta pamoja wadau kujadili na kuweka mikakati ya pamoja kuhusu elimu, ujuzi na ubunifu.

Amebainisha kuwa matukio makuu yatakuwa ni maonesho ya teknolojia yanayoonyesha mchango wa sayansi katika sekta mbalimbali, pamoja na kongamano la elimu na ubunifu litakalojadili utekelezaji wa Dira 2050.

Prof. Mnyone amefafanua kuwa kongamano hilo litaangazia nyenzo tano kuu: utafiti na maendeleo, sayansi na ubunifu, teknolojia za kidijitali, nishati, na usafirishaji funganishi.

Kupitia mijadala na maonesho hayo, Wizara inalenga kufanikisha malengo ya taifa ikiwemo kufikia uchumi wa dola trilioni 1 ifikapo mwaka 2050, kipato cha wastani cha mtu mmoja kati ya Dola za Marekani 7,000 - 12,000, na ajira zenye staha kwa angalau asilimia 50 ya Watanzania.

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe.Salome Makamba,akipata maelezo mara baada ya kutembelea  banda la Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (EWURA) katika Maonesho ya Kizimkazi yanayoendelea katika Viwanja vya Dimbani, Kizimkazi, Zanzibar.

Na Mwandishi Wetu

Naibu Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Salome Makamba, amehimiza umma kupata taarifa sahihi kuhusu hali ya sekta ndogo ya umeme nchini, huku akitoa wito kwa Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuendelea kutoa elimu na taarifa kwa wananchi kuhusu jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuboresha huduma za umeme.

Mhe. Makamba ametoa wito huo leo, tarehe 13 Agosti 2026, alipotembelea banda la EWURA katika Maonesho ya Kizimkazi yanayoendelea katika Viwanja vya Dimbani, Kizimkazi, Zanzibar.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, amesema ni muhimu wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu kuongezeka kwa uzalishaji na upatikanaji wa umeme nchini na hivyo kukidhi mahitaji tuliyonayo.

“Gharama ya umeme nchini Tanzania ni nafuu ikilinganishwa na nchi jirani, na Serikali inaendelea na juhudi za kuboresha na kuimarisha miundombinu ya umeme ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa uhakika, hatua itakayochochea maendeleo ya kiuchumi nchini,” aliongeza.

Katika banda la EWURA, Mhe. Makamba alifahamishwa Mamlaka imetumia fursa ya Maonesho hayo kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya udhibiti ikiwemo mikataba ya huduma kwa wateja, matumizi sahihi na salama ya huduma za bidhaa za gesi ya mitungi, gesi asilia, umeme na maji, fursa za uwekezaji katika sekta na mengineyo.

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe.Salome Makamba,akisaini kitabu  mara baada ya kutembelea  banda la Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (EWURA) katika Maonesho ya Kizimkazi yanayoendelea katika Viwanja vya Dimbani, Kizimkazi, Zanzibar.

 

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe.Salome Makamba,akipata maelezo mara baada ya kutembelea  banda la Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (EWURA) katika Maonesho ya Kizimkazi yanayoendelea katika Viwanja vya Dimbani, Kizimkazi, Zanzibar.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Siuluhu Hassan, akizungumza alipotembelea banda la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwenye Maonesho ya Tamasha la Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar Agosti 12, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (kulia), akimsikiliza Meneja wa Ofisi ya Zanzibar ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Bi. Mariam Saleh, alipotembelea banda la Mfuko huo kwenye Maonesho ya Tamasha la Kizimkazi 2026 (Kizimkazi Festival 2026) Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar Agosti 12, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (kushoto), akimsikiliza Meneja wa Ofisi ya Zanzibar ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Bi. Mariam Saleh, alipotembelea banda la Mfuko huo kwenye Maonesho ya Tamasha la Kizimkazi 2026 (Kizimkazi Festival 2026) Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar Agosti 12, 2026.


Zanzibar, Agosti 12, 2026


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametembelea banda la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) katika Maonesho yanayoambatana na Tamasha la 10 la Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.


Katika ziara hiyo, Mhe. Rais Samia amepongeza PSSSF kwa kushiriki katika maonesho hayo na kutoa huduma pamoja na elimu kwa wanachama na wananchi wanaotembelea banda la Mfuko.


Mhe. Rais Samia alipokelewa na Meneja wa PSSSF Ofisi ya Zanzibar, Bi. Mariam Saleh, ambaye alimueleza kuhusu huduma zinazotolewa na Mfuko, pamoja na namna wanachama na wananchi wanavyonufaika na huduma hizo kupitia banda hilo.


Mhe. Rais Samia ameupongeza Mfuko kwa utoaji wa huduma na kusisitiza umuhimu wa kusikiliza na kushughulikia kwa wakati changamoto zinazowasilishwa na wananchi na wanachama.


“Nawapongeza sana kwa huduma nzuri. Kama kuna malalamiko, yakusanyeni na muyafanyie kazi,” ameagiza Mhe. Rais Samia.


Ushiriki wa PSSSF katika Tamasha la Kizimkazi unalenga kuendelea kuwafikia wanachama na wananchi kwa kuwapatia elimu kuhusu hifadhi ya jamii, huduma zinazotolewa na Mfuko pamoja na kuwawezesha kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu mafao na huduma za PSSSF.

Mwisho

 

Na Mwandishi Wetu

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Bi. Khadija Ngasongwa, ameanza ziara ya kikazi mkoani Mwanza kwa lengo la kuimarisha udhibiti wa bidhaa bandia na kukuza ushindani wa haki katika soko.

Katika ziara hiyo, iliyofanyika leo Agosti 12, 2026, Bi. Ngasongwa amekutana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Ndugu Balandya Elikana, ambapo wamejadili umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika kudhibiti uingizaji, uzalishaji na usambazaji wa bidhaa bandia.

Akizungumza katika kikao hicho, Balandya amesema udhibiti wa bidhaa bandia ni muhimu katika kuhakikisha bidhaa halali zinapata fursa sawa ya kushindana katika soko, hatua ambayo itasaidia kuchochea shughuli za kiuchumi na kuongeza kasi ya maendeleo ya Taifa.

"Kuimarisha udhibiti wa bidhaa bandia kutasaidia kuwalinda wafanyabiashara wanaofuata sheria, kuongeza imani ya wananchi kwa bidhaa zinazouzwa sokoni na kuchochea ukuaji wa uchumi."amesema Balandya

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, amesema Tume itaendelea kuchukua hatua dhidi ya uingizaji, uzalishaji na usambazaji wa bidhaa bandia ili kuhakikisha bidhaa halali zinapata mazingira bora ya ushindani katika soko.

Bi.Ngasongwa amesema kuwa  hatua hizo ni sehemu ya jitihada za FCC za kulinda ushindani wa haki, kuwalinda wafanyabiashara wanaozingatia sheria na kuhakikisha shughuli za kibiashara zinafanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

  




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akimkabidhi Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Zanzibar, Bi. Mariam Saleh Tuzo ya shukran kutokana na mchango wa Mfuko huo kuwa miongoni mwa Taasisi zilizofanikisha kufanyika kwa Kongamano hilo ambalo ni sehemu ya Tamasha la 10 la Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar usiku wa kuamkia leo Agosti 12, 2026.

Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na Wawakilishi wa Taasisi zilizopatiwa tuzo

Rais wa Zaznibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi (Kushoto) na mkewe Mama Mariam Mwinyi (mwenye raba nyekundu), wakitembelea mabanda ya Maonesho baada ya kuzindua Tamasha la Kizimkazi Agosti 12, 2026



Meneja wa PSSSF Zanzibar, Bi. Mariam Saleh, akiwa na Tuzo ya shukrani baada ya kukabidhiwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya kukabidhiwa



Zanzibar, Agosti 12, 2026


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameutunuku Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) tuzo ya kutambua mchango wake katika kuwezesha kufanyika kwa Mdahalo wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, uliofanyika Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, usiku wa kuamkia leo, Agosti 12, 2026.


Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa Meneja wa PSSSF Zanzibar, Bi. Mariam Saleh, kwa niaba ya Mfuko, ikiwa ni sehemu ya utambuzi kwa taasisi na wadau walioshiriki katika kuwezesha mdahalo huo, uliofuatiwa na Maonesho ya Picha za Tamasha la Kizimkazi.


Mdahalo huo umefanyika sambamba na Tamasha la 10 la Kizimkazi (Kizimkazi Festival 2026), linalofanyika Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, ambapo tamasha hilo limeanza rasmi leo kwa matembezi pamoja na uzinduzi uliofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.


Ushiriki wa PSSSF katika mdahalo huo unaakisi dhamira ya Mfuko ya kushirikiana na Serikali, taasisi na wadau mbalimbali katika kuunga mkono mijadala yenye umuhimu kwa jamii, mazingira na maendeleo endelevu.


Aidha, PSSSF inawakaribisha wanachama na wananchi kutembelea banda la Mfuko katika Maonesho ya Tamasha la Kizimkazi yanayoanza leo, Agosti 12, 2026, kwa ajili ya kupata elimu na huduma mbalimbali zinazotolewa na Mfuko, amesema Afisa Uhusiano Mkuu wa PSSSF, Bi. Fatma Elhady.

Mwisho