MGOMBEA Urais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama Cha National League for Democracy 'NLD' Mheshimiwa Doyo Hassan Doyo ameahidi kununua mashine za kisasa kwaajili ya kuchakata zao la Mkonge pamoja na kujenga kiwanda ambacho kitawezesha kuzalisha mkonge wenye viwango vya kimataifa na hatimaye kupandisha thamani ya zao hilo.
Mheshimiwa. Doyo ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza na wakazi wa Korogwe ikiwa ni mwendelezo wa kampeni zake mkoani Tanga ambapo amesema kuwa endapo atapata ridhaa ya kuchaguliwa kuwa Raisi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania atahakikisha zao hilo linakuwa moja wapo ya mazoa yatakayoitangaza Tanzania kimataifa sambamba na kuwasaidia wananchi kujiletea maendeleo.
Amesema asilimia kubwa ya wananchi wa wilaya hiyo ambao ni wa kulima hususani zao la Mkonge kwa muda mrefu wameshindwa kupata maendeleo kutokana na pembejeo wanazozitumia ambapo ameahidi kujenga kiwanda cha kuchakata Mkonge pamoja na kuwaletea pembejeo za kisasa bure.
"Haiwezekani tuendelee kuteseka wakati zao la Mkonge linaweza kutuletea maendeleo sisi na vizazi vyetu kilichopo sasa hivyi ni kwamba bado Serikali iliyopo madarakani imeshindwa kuwasaidia wananchi wa Korogwe kupitia zao hili ambalo lina thamani kubwa sana kimataifa, ndugu zangu tarehe 29 October nendeni mkakichague chama cha NLD nendeni mkanichague Doyo Hassan Doyo"
"Endapo kama mtanichagua nitakwenda kuhakikisha tunajenga kiwanda cha kisasa pamoja na kuwaletea pembejeo za kisasa ambazo mtazipata bure kwaajili ya kulimia Mkonge, zao hili linashindwa kupewa thamani kutokana na uchakataji sa kizamani unaotumika nipeni kura mimi niende kuhakikisha mnaondokana na umasikini wa zao hili" Amesema Doyo.
Aidha Mh.Doyo ameongeza kuwa endapo atachaguliwa atahakikisha anapiga marufuku taasisisi zinazotoa mikopo ya riba ambayo imekuwa ni maumivu kwa wananchi hususani wakina mama badala yake kuitumia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ambapo wananchi wataipata bila ya kurejesha.
"Tuna asilimia 10 zinazotolewa na Halmashauri kwaajili ya wakina mama ,vijana na walemavu lakini wananchi wamekuwa wakidhalilishwa na mikopo umiza endapo mtanichagua kuwa Raisi wenu wa jamhuri ya muungano nitakwenda kuifuta mikopo umiza ambayo imekuwa ni kero kwa wananchi mikopo inayotolewa na Halmashauri itatolewa bure kabisa bila marejesho" amesema Doyo.
Awali akizungumza Mkurugenzi wa habari na mawasiliano kwa umma kutoka National League for Democracy 'NLD' Ibrahimu Pogora amesema ilani ya chama hicho imeangazia kwa asilimia kubwa changamoto zinazowakabili wananchi hususani wa hali ya chini.
Ameongeza kuwa chama tawala kwa muda wa miaka 64 ya uhuru kimeshindwa kutatua baadhi ya kero zinazowagusa wananchi moja kwa moja ikiwemo katika sekta za kilimo , afya ,ardhi na elimu hivyo kuwaomba watanzania ifikapo October 29 kukichagua chama hicho kupitia madiwani , wabunge wake pamoja na nafasi ya Rais.
" Ndugu zangu watanzania niwaombe sana msije mkafanya makosa October 29 kwenye chumba cha kupigia kura tuna miaka 64 ya uhuru lakini bado tuliowaamini wameshindwa kutuletea maendeleo , tusije tukaendelea kuteseka na kuumia wakati nchi yetu ina rasilimali za kutosha tupeni nafasi chama cha NLD tukawaletee maendeleo, acheni mzaha na maisha yenu tutaendelea kuumia kama tukiendelea kuiamini Serikali iliyoshindwa kutuletea maendeleo tangu miaka 64 iliyopita" amesema Pogora.,
Post A Comment: