Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Sekta ya Fedha na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba ameitaka kamati hiyo kuendelea kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha ulioleta mafanikio katika kukuza upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha, matumizi ya teknolojia na kuimarisha uthabiti wa sekta kwa ujumla.
Hayo yalibainishwa jijini Dodoma, katika Kikao cha Kamati ya Uongozi wa Sekta ya Fedha kilichowakutanisha wajumbe kutoka Wizara zinazohusika na masuala ya Sekta ya Fedha pamoja na Taasisi simamizi kama Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA), Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) na Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU)
Dkt. Mwamba alisema kuwa Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha, inaonesha mwelekeo chanya wa kufanikisha utekelezaji wa viashiria vya Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha ifikapo 2029/30, hivyo wadau wa sekta ya Fedha wanahamasishwa kuendelea na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha ili kufikia malengo hayo.
Alisema kuwa katika kuhakikisha Sekta ya Fedha inaendelea kuimarika, Wizara itaendelea kuimarisha sekta ya fedha kwa kuongeza juhudi katika uhamasishaji wa matumizi ya mifumo ya malipo ya kidigiti (cashless economy).
Pia itaendelea kuandaa kanzidata ya Sekta ya Fedha ili kurahisisha upatikanaji wa takwimu za sekta ya fedha na kuimarisha ulinzi wa mifumo ya malipo kwa watumiaji na kudhibiti wizi wa kimtandao kupitia wasimamizi wa sekta.
Aidha alisema kuwa Wizara ya Fedha itaendeleza ubunifu wa bidhaa na huduma endelevu katika sekta ya fedha na kuendelea na utekelezaji wa Programu ya Elimu ya Fedha na kuimarisha uratibu wa masuala ya fedha kwenye jumuiya za Kikanda na Kimataifa.
Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya Uongozi wa Sekta ya Fedha na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema alisema kuwa Serikali imetekeleza Mpango Mkuu katika Sekta ya Huduma Ndogo za Fedha kwa kuongeza watoa huduma ndogo za fedha ambapo hadi desemba, 2024 jumla ya taasisi za huduma ndogo zisizopokea amana zilikuwa 2,342, na SACCOS 964 zilipata leseni na vikundi 58,926 vimesajiliwa.
Alisema utoaji wa Elimu ya Fedha katika maeneo ya mijini na vijijini katika mikoa 17 nchini, kuandaa SME Financing Strategy 2023/24 hadi 2028/29, kuandaa mkakati wa ugharamiaji wa miradi ya Maendeleo kwa njia mbadala (APF Strategy).
Mafanikio ya Utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha ni pamoja na ukuaji wa shughuli za sekta ya fedha umeongezeka kwa asilimia 13.8 mwaka 2024, kuongezeka upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha kutoka asimilia 65 mwaka 2017 hadi asilimia 76 mwaka 2023.
Mafanikio mengine ni pamoja na kiwango cha mikopo chechefu kimepungua kufikia asilimia 3.3 mwaka 2024 kutoka asilimia 9.4 mwaka 2020, mchango wa sekta ya fedha kwenye pato la Taifa umeongezeka kufikia asilimia 3.1 mwaka 2024 na kuongezeka kwa mchango wa mikopo kwa sekta binafsi katika pato la Taifa kutoka asilimia 10 mwaka 2021 hadi asilimia 17.2 Juni, 2024.
Wajumbe wa Kamati hiyo kutoka Wizara ni pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Viwanda.
Post A Comment: