Articles by "MATUKIO"
Showing posts with label MATUKIO. Show all posts

 


Ripoti ya Tume iliyoongozwa na Jaji Mohamed Chande Othman ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 imeendelea kuzua mjadala mkubwa nchini, huku mchambuzi wa masuala ya uongozi, uchumi na siasa Tanzania, Dk Netho Ndilito (PhD), akiitaja kama nyaraka muhimu iliyofichua mambo makubwa matano yenye maslahi kwa taifa.

Akizungumza kuhusu ripoti hiyo, Dk Ndilito amesema baada ya kupitia maoni ya Watanzania, wanamitandao na wachambuzi mbalimbali, amebaini kuwa taarifa hiyo imeleta mwanga mpya kuhusu hali halisi ya taifa na changamoto zilizokuwa zikijadiliwa kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Dk Ndilito, jambo la kwanza ni kwamba ripoti hiyo imeliponya taifa kwa kueleza ukweli ambao kwa muda mrefu haukupata nafasi ya kujadiliwa waziwazi, ikifichuliwa pia kwa nia na dhamira ovu za baadhi ya watu waliotamani vurugu kabla, wakati na baada ya uchaguzi, jambo ambalo sasa limewekwa wazi kupitia uchunguzi huo.

Aidha, ameeleza kuwa ripoti hiyo imeweka bayana upotoshaji na taarifa zisizo sahihi zilizokuwa zikisambazwa na baadhi ya watu wasiolitakia mema taifa, huku wakitamani kuona nchi ikiingia kwenye machafuko.

Katika hoja ya nne, Dk Ndilito amesema ripoti hiyo imeonesha namna Watanzania wengi wanavyoipenda nchi yao, kuiamini serikali yao na kutokuwa tayari kushawishika kuivuruga amani, umoja na mshikamano wa taifa, huku pia ripoti hiyo ikionesha uimara wa serikali pamoja na ukomavu wa vyombo vya ulinzi na usalama katika kushughulikia masuala ya ndani kwa weledi na utulivu.

Dk Ndilito alitumia nafasi hiyo kuwapongeza Watanzania kwa kuendelea kudumisha umoja, upendo, mshikamano na amani, akisisitiza kuwa huo ndiyo utamaduni uliojenga heshima ya taifa kwa miaka mingi.

“Watanzania wameendelea kuonesha ukomavu mkubwa wa kisiasa na uzalendo. Hii ndiyo desturi yetu kama taifa,” alisema.


Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs), yametakiwa kuwa wazi na kuwajabika katika utekelezaji wa majukumu yao hasa kuwahudumia wananchi kupitia miradi mbalimbali wanayotekeleza kwa maendeleo ya jamii. 

Hayo yamesemwa leo Agosti 11, 2025 na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis wakati akifungua Kongamano la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa mwaka 2025 linalofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma kuanzia Agosti 11-13.

Naibu Waziri Mwanaidi ameeleza kwamba uwazi na uwajibikaji wa Mashirika hayo ndiyo msingi wa kutambuliwa kwa mchango wao katika maendelo ya Taifa. 

“Viongozi na wasimamizi wa miradi ya kimaendeleo ya uchumi katika mashirika yenu nawaomba kuzingatia uwajibikaji, pamoja na kuwa tayari kubadilishana uzoefu miongoni mwa Mashirika ili kuwa na maendeleo endelevu kwa nchi yetu” amesema Naibu Waziri Mwanaidi.

Aidha amesisitiza kwamba kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanapaswa kutoa elimu ya kiraia kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu ili kutimiza haki yao ya kidemokrasia. 

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amesema Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni nyenzo muhimu katika kutoa huduma kwa wananchi, hivyo ameyaasa Mashirika hayo kuendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine wa maendeleo kuhakikisha wananchi wananufaika na utekelezaji wa miradi mbalimbali. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mwantum Mahiza amesema Bodi hiyo inaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha NGOs zinafuata kanuni na taratibu zilizopo ili kufanikisha maono yao katika kuwahudumia wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Gasper Makala asema Baraza hilo limeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha Mashirika hayo yanashirikiana na Serikali na wadau wengine katika kuwahudumia wananchi kupitia utekelezaji wa miradi.

Kongamano la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa mwaka 2025 linaongozwa na kaulimbiu isemayo: Tathmini ya Miaka Mitano kuhusu Mchango wa NGOs katika Maendeleo ya Taifa 2020/2021-2024/2025: Mafanikio, Changamoto, Fursa na Matarajio.

 


Na John Mapepele

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe.Mohamed Mchengerwa   amezindua soko la kisasa la nyama choma la Kumbilamoto vingunguti, Ilala jijini Dar es Salaam na kushuhudia utiaji wa mikataba ya  miradi 6 ya maendeleo  yenye  thamani ya  shilingi bilioni 7.7

Mara baada ya kuzindua soko hilo ambalo limegharimu takribani shilingi milioni 727 amepongeza uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kufanikisha mradi huo ambapo amezitaka Halmashauri nyingine kuiga  mfano huo.

Aidha, amefafanua kuwa soko hilo litakwenda kuwapatia ajira  wananchi wengi huku akisisitiza  kuendelea kulitunza  ili lisiharibike kwenye kipindi kifupi.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa kukamilika kwa soko hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na  kufafanua kuwa Serikali ya awamu ya sita tayari imekamilisha  miradi  mingi kama iilivyoahidi.

Wakati  huo huo Waziri Mchengerwa amezitaka Halmashauri zote nchini kutimiza malengo  zilizojiwekea ya ukusanyaji  mapato ili  ziweze kutekeleza  miradi ya  maendeleo huku akizitaka  kuendelea kubuni miradi  mbalimbali ya maendeleo yenye tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Akizungumzia kuhusu wakandarasi wazawa, Mhe Mchengerwa  amezitaka Halmashauri na mikoa  yote nchini kuwapa kipaumbele  wakandarasi wazawa huku akitoa wito  kuwachukulia hatua wakandarasi wanaofanya  vibaya  katika  kazi wanazopewa.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogole amemhakikishia Mhe. Mchengerwa kuwa  mikataba yote iliyosainiwa inakwenda kukamilika  kabla ya mwisho wa mwaka na kwamba wananchi watakwenda kunufaika  na miradi hiyo.

Katika uzinduzi wa soko hilo Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Zungu ambaye  pia ni Mbunge wa Ilala amewataka watanzania  kutojihusisha na uvunjaji wa amani   katika kipindi hiki  cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika  Oktoba  mwaka  huu

Bi. Amina Selemani ambaye  ni miongoni mwa mfanyabiashara  katika soko  hilo amemshukuru  Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fedha za kujenga soko  hilo ambalo limetoa ajira  kwa akina mama wengi.

“Kwa kweli tunamshukuru Mheshimiwa Rais  wetu  kwa upendo huu wa kutuletea  mradi huu wa soko ambao  umekuwa ni ukombozi kwa  maisha yetu”. Amefafanua Amina






Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo-Busisi) utakaofanyika Juni 19 mwaka huu. 

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametoa taarifa hiyo katika mkutano wa hadhara wilayani Sengerema mkoani Mwanza wakati akizungumza mbele ya Waziri Mkuu, Kassim  Majaliwa,  ambaye yuko ziarani mkoani Mwanza.

Waziri Ulega amewataka wananchi wa Mwanza kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi huo wa daraja hilo lenye  urefu wa kilometa 3 na barabara zake unganishi zenye urefu wa kilometa 1.66 na linalotarajiwa kuwa refu kuliko yote katika eneo la Afrika Mashariki na Kati. 

Ulega alisema kukamilika kwa daraja hilo ni mafanikio ya maono na jitihada kubwa zilizofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na mtangulizi wake, hayati John Magufuli. 

Namna pekee ya kuonyesha furaha yetu na shukrani zetu kwa mafanikio hayo ni kwenu wananchi wa Sengerema, mkoa wa Mwanza, Geita, mikoa yote ya kanda ya ziwa na wa Tanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kwenye uzinduzi huo. Tunasema siku hiyo asiye mwana basi abebe jiwe.” alisema Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga. 

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi katika tukio hilo. 

"Jitayarisheni kwa wingi kumpokea kiongozi wetu mkuu atakapokuja kulifungua daraja hili Juni 19, 2025 ", alisema Waziri Mkuu. 

Ziara ya Waziri Mkuu mkoani Mwanza ni ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo Ulega alitumia mkutano wa Sengerema kumweleza Waziri Mkuu kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutarahisisha huduma za usafiri na uchukuzi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa ujumla.

“Watu waliokuwa wanasafiri kwa zaidi ya saa mbili watakwenda kusafiri kwa wastani wa dakika tatu hadi tano, Tunamshukuru Mhe Rais kwa maono na maelekezo yake”, amesisitiza Ulega.

Ameongeza kuwa zaidi ya shilingi bilioni 700 zimetumika katika ujenzi wa daraja hilo linalounganisha mji wa Kigongo na Busisi katika Ziwa Victoria ambalo ni la tatu kwa ukubwa duniani.

Aidha, Waziri Ulega amewahakikishia wakazi wa Wilaya ya Sengerema kuhusu ujenzi wa barabara Segerema - Nyehunge (km 54.5) na Kamanga - Sengerema (km 32) kwa kiwango cha lami Serikali ipo katika hatua za mwisho za kumkabidhi Mkandarasi kazi ya ujenzi huo.









 


Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa kupeleka umeme kwenye maeneo ya kimkakati nchini ikiwemo maeneo ya migodi midogo, maeneo ya uvuvi, Viwanda na yanayochagiza shughuli za kiuchumi.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Mei 14, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Mwibara, Mhe. Charles Kaijage aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali kuyapelekea umeme maeneo ya uvuvi ili kukuza uchumi wa wananchi wa maeneo hayo.

"Mheshimiwa Naibu Spika Mradi huu wa kupeleka umeme maeneo ya kimkakati umefikia zaidi ya maeneo 300 ikiwemo vituo vya afya na visima vya maji kwa maeneo ambayo yanatoa huduma za kijamii." Amesema Kapinga

Akijibu swali la Mbunge wa Igunga, Mhe. Nicholas Ngassa aliyeuliza lini Serikali itaanza usambazaji umeme kwenye Vitongoji vya Jimbo la Igunga. Mhe. Kapinga amesema Jimbo la Igunga lina jumla ya Vitongoji 337 ambapo kati ya hivyo, Vitongoji 95 vimepatiwa umeme.

Ameongeza kuwa, katika Vitongoji 15 Wakandarasi wanaendelea na utekelezaji wa miradi kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vitongojini Awamu ya Pili A (HEP IIA) na Vitongoji 69 zabuni imetangazwa kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vitongojini Awamu ya Pili B (HEP IIB).

Amesema kuwa, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) itaendelea kutenga fedha za kuvipelekea umeme vitongoji 158 vilivyosalia.

Amesisitiza kuwa, gharama ya kuunganisha umeme kwa maeneo ya Vijijini ni shilingi 27,000/- na kuongeza kuwa, kuna mradi utakaoanza hivi karibuni unaohusisha Vitongoji ambavyo havina laini kubwa ya umeme na vilivyo na kwenye laini kubwa ya umeme.

 


Na Kassim Nyaki, NCAA.

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) Dkt. Elirehema Doriye leo tarehe 12 Mei, 2025 amevisha vyeo jumla ya watumishi 621 ikijumuisha Maafisa 145 na askari 476 wa jeshi la Uhifadhi. 

Akizungumza na watumishi hao baada ya kuwaapisha na kuwavisha vyeo Dkt. Doriye amewasisitiza maafisa na askari wa jeshi la uhifadhi kuzingatia kiapo walichoapa na kuzingatia maadili ya utendaji kazi, kuzingatia sheria, ushirikiano, upendo na kujiepusha na rushwa katika maeneo ya kazi.

“Leo mmeapa na kuvishwa vyeo vya kijeshi, mnapaswa kuonesha dhamira ya dhati ya kulinda Hifadhi ya Ngorongoro na rasilimali zote za uhifadhi, vyeo mlivyovishwa vinakuja na majukumu makubwa ambayo yanahitaji kujituma na kuwajibika ipasavyo, hakikisheni mnakuwa mfano bora kwa jamii kwa kuzingatia maadili, nidhamu, sheria, uaminifu, uzalendo kwa rasilimali za nchi, kujiepusha na vitendo vya rushwa na kufuata miongozo ya jeshi la Uhifadhi” alisisitiza Dkt. Doriye.

Kamishna Doriye amewakumbusha  watumishi hao kuwa, kupanda cheo ni kuongezewa majukumu ya kiuongozi katika usimamizi wa shughuli za uhifadhi, utalii, ulinzi, maendeleo ya jamii na urithi wa asili na utamaduni uliopo hifadhi ya Ngorongoro na kusisitiza kuwa suala la mafunzo ya kijeshi kwa watumishi wa NCAA litakuwa endelevu ili kuendelea kujenga utimamu wa mwili kwa afisa na askari.

Awali akizungumza katika tukio hilo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi (SACC) anayesimamia Idara ya Rasilimali watu na Utawala Salma Chisonga ameeleza kuwa tukio la kuvishwa vyeo watumishi hao ni utekelezaji wa vibali vya kupandisha vyeo watumishi ambavyo vilitolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2021/2022 hadi mwaka 2024/2025.

SACC Chisonga amebainisha kuwa maafisa 145 waliovishwa vyeo wamegawanyika katika ngazi mbalimbali ambapo Maafisa uhifadhi Wakuu daraja la kwanza ni 5, Maafisa uhifadhi Wakuu daraja la II ni 21, Maafisa uhifadhi waandamizi ni 31, Maafisa uhifadhi daraja la I ni 56 na Mafiasa uhifadhi daraja la II ni 32.

Ameongeza kuwa askari 476 waliovishwa vyeo wamegawanyika katika ngazi mbalimbali ambapo askari wa uhifadhi mkuu daraja la I ni  39, askari wa uhifadhi wakuu daraja la II ni 54, askari wa uhifadhi Waandamizi ni 70, askari wa uhifadhi daraja la kwanza ni 86 na askari wa uhifadhi daraja la II ni 227.











 


Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Haruni Mapesa amewatunuku  vyeti na kuwakabidhi zawadi ya Fedha taslimu watumishi  20  ambao wameshinda nafasi na kuwa Wafanyakazi bora katika mwaka wa fedha 2024/2025, Wafanyakazi hao ni  kutoka  katika  Kurugenzi, Idara na Vitengo kwa kampasi zote za Chuo hicho .

Akizungumza na Menejimenti na Wafanyakazi hao Prof.Mapesa amewapongeza kwa ushindi huo na amewataka Watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidi, nidhamu na Uzalendo ili kufikia Malengo ya Taasisi na Taifa kwa ujumla.

Prof. Mapesa amesema teknolojia inazidi kukua hivyo amewataka  Watumishi kuona namna bora ya kutumia E- Learning,  na kuona ni namna gani vifaa na mifumo ya Kisasa  viitaweza kutumika ili kuwafikie wadau wengi. 

Prof. Mapesa amesema  ni wajibu wa kila Mtumishi  kufanya mahala Pa kazi kuwa mahala Pa furaha,  Amani,  na sehemu salama kwa kuwa muda mwingi  mtumishi anatumia muda wake akiwa kazini.

“ Nawasisitiza sana Kwa upande wa Wanataaluma kuhakikisha tafiti zinafanyika, na Ushauri wa kitaalamu unatolewa, jipangeni kuandika na kuchapisha ikiwa ni pamoja na kuhakikisha tunatoa huduma bora kwa wateja (Customer care), kujali wateja ni jambo la msingi sana,”alisisitiza Profesa Mapesa.

Katika hatua nyingine Prof. Mapesa ameungana na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika kuomboleza kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu Mzee Cleopa David Msuya ambapo amesema Taifa limepoteza mtu muhimu kwa namna moja ama nyingine  kwa kuwa Mzee  Msuya alikuwa ni miongoni mwa Wazee walioshirikiana na baba wa Taifa Mwalimu JK Nyerere katika kukijenga Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Kwa upande wake Naibu Mkuu wa Chuo anaesimamia Mipango, Fedha na Utawala Dkt. Evaristo Haulle alivitaja  vigezo vilivyotumika kumpata Mfanyakazi bora kuwa ni sharti awe Mtumishi wa Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa Zaidi ya mwaka mmoja, awe na mahusiano mazuri na viongozi  na Wafanyakazi wenzake, asiwe mtu wa Majungu na awe tayari kulinda Uchumi na kudumisha Amani.

Katika hafla hiyo fupi ambayo ilishirikisha viongozi wa vyama vya Wafanyakazi, Chama cha Wafanyakazi wa Taaasisi, Elimu ya juu, Sayasni, Teknolojia, Ufundi Stadi, Habari na Utafiti (RAAWU), Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu (THTU) na MNIMASA.

Kwa upande wa Wafanyakazi bora waliowakilisha Chuo Dkt. Willy Maliganya upande wa Wanataaluma,  na Bwana. Atanas Limbu upande wa Waendeshaji wameushukuru Uongozi wa Chuo na kusema kuwa zawadi zilizotolewa zinatoa motisha kwa Wafanyakazi kujituma na kufanya vizuri na kuwa ushindi uliopatikana siyo wa kwao peke yao bali ni wa Chuo kizima.







 


Na. James K. Mwanamyoto OR-TAMISEMI


WANANCHI wa Rufiji mikoani Pwani wameeleza kufurahishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo jimboni humo ikiwemo ujenzi wa barabara, shule, zahanati na vituo vya afya.

WANANCHI hao pia wamempongeza Mbunge wa Rufiji, Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa jitihada zake za kuhakikisha huduma za jamii zinapatikana kwa uhakika na ubora.

Wameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya kikazi ya Mwenyekiti wa UWT taifa Mhe. Mary Chatanda aliyoifanya Wilayani Rufiji kwa siku mbili, kwa lengo la kukagua utetelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020/2025.

Mkazi wa ikwiriri Bw. Abdallah Moba amesema jitihada za Mhe. Mchengerwa za kujenga barabara ya Kituo cha Afya Ikwiriri zimewawezesha wananchi kufika kwa urahisi katika kituo hicho ili kupata huduma za afya msingi.

Bi. Mariam Hamza ambaye ni Mama Lishe amesema kuwa, kabla ya barabara ya Kituo cha Afya Ikwiriri kujengwa wateja wake walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya vumbi pindi bodaboda zinapopita, hali iliyopelekea kuwapoteza wateja lakini hivisasa changamoto hiyo imetatuliwa.

Bw. Sirajidini Hassan ambaye pia ni dereva bodaboda ambaye shughuli zake anazifanya nje ya Kituo cha Afya Ikwiriri, amemshukuru Waziri Mchengerwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuijenga barabara hiyo ya Kituo cha Afya Ikwiriri na kuiwekea taa kwani hapo awali watu hususani wanawake walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya kuporwa mali zao kutokana na kiza kilichokuwepo wakati usiku.

Bw. Ramadhan Hamza ambaye pia ni dereva bodaboda, amemshukuru Waziri Mchengerwa kwa kuhakikisha Barabara ya Kituo cha Afya Ikwiriri inajengwa, na hatimaye kuwawezesha wagonjwa kufika kwenye kituo hicho cha afya kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuwawezesha madereva bodaboda kujiongezea kipato.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema amefanya kazi usiku na mchana ya kuleta mabadiliko wilayani Rufiji kwa kushirikiana na viongozi wa kata zote, lengo likiwa ni kuboresha upatikianaji wa huduma za kijamii ambapo wananchi hivisasa wanafurahia huduma zinazotolewa katika sekta ya elimu, afya na barabara.

Mhe. Mchengerwa amesema: “Tumefanya kazi usiku na mchana kuhakikisha tunaibadilisha Rufiji, tulianza ujenzi wa shule, ujenzi wa zahanati, ujenzi wa vituo vya afya na miundombinu ya barabara na mingineyo,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, walikubaliana kwamba ndoto ya wanarufiji ni kuleta mabadiliko, hivyo ana uhakika mwananchi yeyote akiulizwa hivisasa ataeleza namna ndoto hiyo ilivyotimia katika kipindi hiki cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ikwiriri Dkt. Tegemei Mtambo ameishukuru Serikali kwa kuwapatia milioni 140 zilizowezesha ujenzi wa jengo la huduma za mionzi na huduma tayari imeanza kutolewa, ambapo awali wananchi walilazimika kusafiri zaidi ya kilomita 30 kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Wilaya na Hospitali ya Misheni Mchukwi.

Sanjari na hilo, Dkt. Mtambo ameishukuru Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kuwapatia X-Ray ya kisasa inayowahudumia wananchi, aidha amemshukuru Waziri Mchengerwa kwa kutimiza ahadi yake ya kumleta Mteknolojia wa Mionzi ikiwa ni pamoja usimamizi wa maboresho yote yaliyofanyika kiasi cha watu kuamini kuwa Kituo cha Afya Ikwiriri ndio Hospitali ya Wilaya ya Rufiji.







 


Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza nchini wamezindua Programu ya Mafunzo ya Ujasiriamali na Stadi za Biashara kwa wafungwa wanaokaribia kumaliza vifungo vyao, ili kuwapatia ujuzi utakaowasaidia kujipatia kipato halali na kujikwamua kiuchumi baada ya kumaliza vifungo.

Akifungua programu hiyo leo Mei 06, 2025 katika gereza kuu Arusha, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza CGP Jeremiah Katungu ameipongeza IAA kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha eneo la urekebishaji ambalo ndiyo jukumu kubwa la jeshi la magereza. 

“Kasi ya IAA tumeiona, tangu tuliposaini makubaliano Septemba 2024 matokeo tunayaona, na sisi tunakwenda kwa kasi hiyo hiyo kuhakikisha kwamba tunayafikia tuliyokubaliana kwa maslahi mapana ya taifa letu; programu hii  ni mwanzo mzuri na tutahakikisha tunawafikia wafungwa wengi zaidi,” amesema CGP Jeremiah Katungu.

CGP Jeremiah Katungu ameongeza kuwa pamoja na mafunzo hayo kwa wafungwa, zaidi ya maafisa na askari 100 wa jeshi la magereza wamedahiliwa kwa mwaka wa masomo 2024/2025 kwa ngazi ya shahada ya uzamili, ikiwa ni sehemu ya makubaliano kuwajengea uwezo waweze kutimiza majukumu yao kwa weledi na ufanisi

Mkuu wa Chuo IAA Prof. Eliamani Sedoyeka amesema wajibu wao kama chuo ni kutoa mafunzo kwa ngazi mbalimbali na mafunzo haya kwa wafungwa ni mwanzo tu, huku akibainisha kuwa malengo yao kutoa mafunzo ya muda mrefu kuanzia ngazi ya cheti mpaka shahada ya uzamili kwa wafungwa.

Prof. Sedoyeka ameongeza kuwa katika kozi za muda mfupi IAA imeanza na programu hii ya ujasiriamali na wanatarajia kutanua wigo wa mfunzo kwa kuanzisha kozi nyingine ikiwepo udereva, ili wafungwa wanapomaliza vifungo vyao wawe na ujuzi, maarifa  na kuwa vielelezo bora kwa jamii zao.

Naye Mkuu wa Kitivo Cha Utawala na Usalama IAA Dkt. Adonijah Abayo amesema Programu ya Mafunzo ya Ujasiriamali na Stadi za Biashara kwa wafungwa imeanza na wanafunzi 40 na yatatolewa kwa wiki mbili kwa kuanza na Gereza la Arusha na baadaye maeneo mengine, ambapo itawasaidia wafungwa wanaporudi mtaani kwenda kujiajiri na kukuza uchumi wao na uchumi wa nchi.