Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Makalla, ameipongeza Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) kwa tafiti na bunifu mbalimbali zinazolenga kuongeza tija katika sekta za kilimo na mifugo.

Mhe. Makalla amesema kuwa ametembelea banda la NM-AIST na kujionea teknolojia mbalimbali za kilimo na mifugo, pamoja na bunifu zinazolenga kuongeza thamani ya mazao na bidhaa za mifugo.

Amesisitiza kuwa mapinduzi ya kweli hayawezi kufanyika bila utafiti, teknolojia na ubunifu, akieleza kuwa NM-AIST imekuwa ikifanya vizuri katika kuibua na kuendeleza teknolojia zinazolenga kutatua changamoto za jamii.

“Kilimo bila utafiti, teknolojia na dhana za kisasa hakiwezi kuleta mabadiliko makubwa. Taasisi za utafiti zinatuelekeza na kutupeleka kwenye kilimo na ufugaji wenye tija,” amesema Mhe. Makalla.

Aidha, Mhe. Makalla amesema maendeleo ya sekta za kilimo, mifugo na uvuvi hayapaswi kupimwa kwa kuongezeka kwa uzalishaji pekee, bali pia kwa uwezo wa kuzalisha kwa tija, ubora na kuzingatia mahitaji ya soko, kama inavyosisitizwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Ameeleza kuwa Dira hiyo inalenga kujenga uchumi shindani unaoongozwa na maarifa, teknolojia, ubunifu na uongezaji wa thamani, hivyo taasisi za utafiti kama NM-AIST zina nafasi muhimu katika kufanikisha azma hiyo.

Mhe. Makalla ameyasema hayo wakati akihitimisha Maonesho ya 32 ya Kilimo, Mifugo na Sherehe za Nanenane Kanda ya Kaskazini, yaliyofanyika katika Viwanja vya Themi Njiro, Arusha.

Share To:

Alex Sonna

Post A Comment: