Na: OWM – KAM, Morogoro.
Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano kupitia kitengo cha Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waaajiri imetoa Mafunzo kwa Viongozi na Wafanyakazi wa Vyama vya Wafanyakazi, Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kwa lengo la kuwajengea uwezo, utawala bora na kuongeza tija miongoni mwa viongozi hao.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo yanayofanyika katika Ukumbi wa Kings Way, leo Agosti 12, 2026, mkoani Morogoro, Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri, Vallensi Wambali, alipomuwakilisha Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Bi. Mary Maganga, amesema mafunzo hayo yana mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga Taifa lenye rasilimali watu wenye ujuzi, taasisi zinazowajibika na mazingira bora ya kazi yanayochochea tija na maendeleo ya Nchi.
“Hatuwezi kufikia Dira 2050 bila kuwa na vyama vya wafanyakazi na waajiri vyenye nguvu, vinavyoendeshwa kwa uwazi na vinavyojenga ushirikiano badala ya migogoro,” amesema Wambali.
Vilevile, Msajili Wambali amesema mafunzo hayo yamewakutanisha viongozi na watendaji kutoka Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Vyama mbalimbali vya Wafanyakazi, Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) pamoja na Maafisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano.
Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo washiriki katika maeneo mbalimbali, ikiwemo usimamizi bora wa taasisi, kufanya maamuzi kwa kuzingatia sheria na taratibu, kuimarisha mazungumzo ya kijamii, kuzuia migogoro kabla haijatokea pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wanachama.
“Kiongozi wa leo hapimwi kwa uwezo wa kuzungumza pekee, bali kwa uwezo wa kusikiliza, kujenga maridhiano na kuleta matokeo,” amesema Wambali.
Sambamba na hilo, Msajili Wambali amesema Serikali itaendelea kulinda na kuimarisha mfumo wa mazungumzo ya kijamii, mfumo huo ni msingi muhimu wa kujenga amani na utulivu mahali pa kazi.
Amesema pale Serikali, Waajiri na Vyama vya Wafanyakazi wanaposhirikiana kwa kuheshimiana na kutatua changamoto kupitia mazungumzo, uzalishaji huongezeka, migogoro hupungua na hatimaye uchumi wa Taifa huimarika.






Post A Comment: