Shirika la Hifadhi ya Taifa TANAPA wameanza mpango wa kudhibiti wanyamapori, wakiwemo tembo wasivamie maeneo ambayo ni makazi ya watu kwa kwa kuwavalisha mikanda ya  kielektroniki yenye kutoa ishara ya utambuzi walipo hasa kama wameondoka katika hifadhi.

Taarifa ya kutekelezwa kwa mpango huo imetolewa na Mkuu wa Uhifadhi kanda ya Mashariki Kamishna msaidizi mwandamizi John  Nyamuhanga wakati mwa utekelezaji wa zoezi la kuwaweka mikanda ya mawasiliano makundi mbalimbali ya wanyama waharibifu.

Nyamuhanga amesema zoezi hilo ni mikakati ya makusudi inayofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori, TAWIRI, katika kupunguza muingiliano baina ya wanyamapori na wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi za Taifa.

Alisema matumizi ya teknolojia za kisayansi ya kuwavalisha Wanyamapori wakali na waharibifu mikanda yenye mfumo wa mawasiliano ili kutambua na kudhibiti mienendo yao itasaidia kupata taarifa za mienendo ya wanyama hao  mapema  na hivyo kuwazuia au kuwarejesha hifadhinikabla ya kusababisha madhara kwa jamii.
 
Awali akizungumzia teknolojia hiyo, Mtafiti kutoka TAWIRI, Dk Justin Shamanche amesema kifaa hicho kinauwezo wa kutoa ishara pindi mnyama akitoka nje ya mipaka hifadhi hivyo kutoa fursa kwa wananchi kujipanga kwa njia nyingine kuweza kurudisha ndani ya hifadhi.

Naye Ofisa Uhifadhi mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa Saadani, Prisca Elisia amesema pamoja na kusaidia wanyama hao wasilete vurugu katika maeneo jirani na hifadhi pia inasaidia sekta ya utalii kwa kutambulisha wanyama wapo wapi hivyo kuwa rahisi kwa watalii kufika walipo na kuwaona.

" Teknologia hiyo itasaidia sekta ya utalii kwa wageni kuweza kumuona mnyama wanaemtaka kwa wakati badala ya kumtafuta mnyama kiholela" alisema Prisca.

Naye mwakilishi kutoka kiwanda cha sukari cha Bagamoyo, Jeremia Mponji alielezea kufurahishwa na kuingizwa kwa teknolojia hiyo kwani wamekuwa wakipata hasara sana katika shamba lao la miwa.

Alisema mashamba yao yamekuwa yakivamiwa sana na tembo hivyo kuja kwa teknolojia hiyo anaamini itawasaidia maofisa uhifadhi kuwaswaga kuwarejesha  hifadhini kirahisi.Share To:

Post A Comment: