Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii imewasili katika Wilaya Mbarali, Mkoani Mbeya kuratibu zoezi maalumu la kuwaondoa tembo kwenye makazi ya watu katika kata tano za Igava, Mawindi, Miyobweni, Imalilosongwe na Rujewa ambapo zoezi litaanza katika vijiji vya Kata ya Igava ambavyo vimeathiriwa zaidi na uvamizi wa tembo.
Akizungumzia zoezi hilo , Mwakilishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii Antonia Raphael amesema zoezi hilo litafanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia tarehe 08 hadi 09 Mei, 2024 ambapo teknolojia ya helikopta itatumika kuwaswaga tembo hifadhini sambamba na kuwafunga mikanda maalum ya mawasiliano (GPS satellite Collars) tembo viongozi wa makundi ili kufuatilia mienendo yao.
Vilevile, Anthonia amesema kuwa zoezi hilo litaongozwa na Mheshimiwa waziri wa Maliasili na Utalii.
Naye, Dkt. Emmanuel Masenga ambaye ni Mtafiti Mkuu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) amebainisha kuwa maandalizi ya zoezi hilo yamekamilika ambapo timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake za TAWIRI, TANAPA, TAWA pamoja na timu kutoka Wilaya ya Mbarali zipo uwandani kuhakikisha zoezi la kuwaondoa tembo kwenye makazi ya watu linaanza kesho kwa ufanisi.
Dkt.Masenga amesema teknolojia ya helikopta imekuwa na manufaa katika kuwaondoa tembo kwenye makazi ya watu kwa haraka zaidi.
Naye, mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Donald Mwigombe ambaye pia ni Afisa Tarafa ya Rujewa, ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari wakati wa zoezi la kuwaswaga tembo kutoka kwenye makazi ya watu ambapo amewataka wananchi kutokusogea karibu na tembo, wakati zoezi linaendelea ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na tembo pindi wanaposwagwa kwa helikopta.
Post A Comment: