Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii leo Agosti 18, 2026 Bungeni Jijini Dodoma, imeipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi yake ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania(TAWIRI)
Kwa namna inavyofanya jitihada za kugundua mbinu mbalimbali za kupambana na kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu.
Pongezi hizo zimetolewa wakati kamati hiyo ikipokea na kujadili taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya utendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI).
“ tunaona na kuthamini kazi nzuri ya Wizara kupitia TAWIRI kwa kufanya tafiti zilizosaidia kupata njia bora zinazoonesha matokeo chanya katika kudhibiti wanyama wakali na waharibifu” amesema Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Timotheo Mnzava
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ameihakikishia Kamati kuwa , Wizara hiyo itaendelea kuziwezesha taasisi zake ili ziendelee kufanya kazi kwa ufanisi na kufikia malengo yanayotarajiwa,
“ Wizara na wataalamu wake wapo kazini kila wakati kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuifanya Sekta ya Maliasili na Utalii kuendelea kuwa na mchango mkubwa katika ustawi wa wananchi na taifa kwa ujumla” amebainisha Dkt. Kijaji
Ikumbukwe mbali na jukumu la Kufanya, Kuratibu na Kusimamia tafiti za wanyamapori hapa nchini, TAWIRI inajukumu la kuishauri serikali juu ya masuala yote ya sayansi ya wanyamapori kwa uhifadhi endelevu, ustawi wa jamii na kukuza utalii.






Post A Comment: