OWM-TAMISEMI ,Morogoro


Mkoa wa Morogoro umeanza kushuhudia shamrashamra za michezo baada ya Mashindano ya Michezo ya Wanafunzi wa Shule za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSA Games 2026) kuanza rasmi katika viwanja mbalimbali vya mkoa huo.

Mashindano hayo yameanza leo, Agosti 14, 2026, yakikutanisha maelfu ya wanamichezo chipukizi kutoka Tanzania na nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, huku ushindani ukianza kushika kasi katika michezo mbalimbali.

Mapema asubuhi, viwanja mbalimbali vilianza kujaa wachezaji, makocha, waamuzi na mashabiki, hali iliyoifanya Morogoro kubadilika na kuwa kitovu cha michezo ya shule katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Katika mchezo wa mpira wa miguu wa wasichana uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Amus College ya Uganda ilianza kampeni yake kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Boni Consili Girls Vocational & Secondary School, katika mchezo uliokuwa miongoni mwa vivutio vya siku ya kwanza. 

Kwa upande mwingine, mchezo wa soka la wavulana nao umeanza kwa ushindani mkubwa, huku timu kutoka Tanzania, Uganda, Burundi na nchi nyingine zikianza safari ya kusaka ubingwa wa Afrika Mashariki. Miongoni mwa michezo ya siku ya kwanza, IPTEM Makamba ya Burundi ilitarajiwa kukutana na Nsumba ya Tanzania katika uwanja wa SUA. 

Mashindano ya mwaka huu yana sura ya kipekee kutokana na kuongezeka kwa michezo inayoshirikishwa, ikiwemo baseball, cricket, lacrosse, beach volleyball, chess, softball, beach football na scrabble, ambayo imeongezwa kwenye programu ya mashindano. 

Kwa ujumla, FEASSA Games 2026 imekusanya zaidi ya wanamichezo 6,000 ikifanya toleo hili kuwa miongoni mwa matoleo makubwa zaidi katika historia ya mashindano hayo. 

Mashindano yanaendelea katika maeneo mbalimbali ya Morogoro hadi Agosti 22, 2026, huku kila timu ikipigania heshima ya shule na nchi yake. 

Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: