Na. Veronica Mwafisi-Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imepokea taarifa kuhusu hatua ya mchakato wa maandalizi, matarajio na hatua za utekelezaji wa kipindi cha tatu cha mpango wa kunusuru kaya maskini (PSSN III) na kutoa maelekezo ya kuendeleza misingi ya utekelezaji wenye ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika kufikia walengwa waliokusudiwa na kutimiza malengo ya PSSN III.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amezungumza hayo leo tarehe 14 Agosti, 2026 Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akiongoza kikao cha Kamati yake na Watendaji wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kilicholenga kupokea taarifa kuhusu hatua ya mchakato wa maandalizi, matarajio na hatua za utekelezaji wa kipindi cha tatu cha mpango wa kunusuru kaya maskini (PSSN III).
Vilevile, Mhe. Dkt. Ndumbaro ameipongeza TASAF kwa utekelezaji mzuri wa Miradi ya Maendeleo ikiwemo ujenzi kwenye sekta ya elimu na afya.
Kwa niaba ya Kamati yangu nitoe pongezi nyingi kwa ofisi hii, kwa hakika mnafanya kazi nzuri katika mpango wa kunusuru kaya maskini, lakini pia mnatekeleza vizuri Miradi ya Maendeleo ikiwemo ujenzi kwenye sekta ya elimu na afya, mnamwakilisha vizuri Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa miradi hii Amesema Mhe. Dkt. Ndumbaro
Awali akiwasilisha kwa Kamati hiyo taarifa kuhusu hatua ya mchakato wa maandalizi, matarajio na hatua za utekelezaji wa kipindi cha tatu cha mpango wa kunusuru kaya maskini (PSSN III), Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray amesema, PSSN III iliidhinishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia tarehe 10 Aprili 2026, na kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha maandalizi kabla ya kuanza utekelezaji.
Naibu Waziri Qwaray amesema kuwa, katika maandalizi ya utekelezaji wa PSSN III, hatua muhimu zimekamilika ikiwemo kukamilisha usanifu wa Mpango, kuandaa nyaraka mbalimbali za utekelezaji, miongozo ya kiutendaji na kuimarisha mifumo ya TEHAMA inayosimamia shughuli za Mpango.
Aidha ameongeza kuwa, mchakato wa utambuzi wa Mamlaka za Maeneo ya Utekelezaji yatakayoshiriki kwenye utekelezaji wa Mpango unaendelea na unaojumuisha timu ya wataalamu kutoka TASAF, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), pamoja na wataalamu wa mazingira ambapo uchambuzi na uchakataji huo utazingatia viwango vya umaskini katika ngazi ya Halmashauri pamoja na viashiria vya athari za kimazingira, ikiwemo uwezekano wa maeneo kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na majanga mbalimbali.
Vilevile, Mhe. Qwaray amesema kupitia mpango huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa kaya maskini na zilizo katika mazingira hatarishi kukabiliana na changamoto za kiuchumi, kijamii na kimazingira, kuongeza ujuzi na taaluma kwa vijana kutoka kaya maskini na zinazoishi katika mazingira hatarishi zitakazoweza kujiajiri na kuajiriwa, kuwa na masijala ya kitaifa (kanzi data) yenye taarifa muhimu ya kaya maskini na zilizopo katika mazingira hatarishi pamoja na urasimishwaji wa TASAF kama taasisi ya umma ya kutekeleza na kusimamia utoaji wa huduma za msaada ya kijamii itakayohakikisha uendelevu, ufanisi na uratibu wa utoaji wa huduma hizo nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Bw. Shedrack Mziray ameishukuru Kamati hiyo kwa maoni na ushauri mbalimbali ambao wameutoa na kuahidi kufanyia kazi ili kuimarisha na kuboresha utendaji kazi wa Taasisi hiyo.











Post A Comment: