Na Mwandishi Wetu - Zanzibar


Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga mazingira wezeshi kwa uchumi wa kidijitali Zanzibar kwa kuwezesha huduma ya intaneti katika mradi wa makazi wa Amani Residency, uliopo Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, kupitia huduma yake ya Faiba Mlangoni Kwako.

Mradi huo wa kisasa wa makazi ulizinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ukiwa ni sehemu ya uwekezaji unaolenga kuongeza fursa za makazi bora, biashara na utalii pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi Zanzibar.

Akizungumza kuhusu uwezeshaji huo, Meneja wa TTCL Zanzibar, Bi. Nasra Mugheiry, alisema TTCL imeweka mazingira ya mawasiliano ya kisasa katika Amani Residency ili kuwawezesha wakazi kupata huduma ya intaneti karibu na makazi yao na kutumia fursa mbalimbali zinazotokana na uchumi wa kidijitali.

“TTCL kupitia huduma ya Faiba Mlangoni Kwako imeweka mazingira wezeshi ya mawasiliano katika Amani Residency, kwa lengo la kuwawezesha wakazi kutumia intaneti katika shughuli zao za kila siku, ikiwemo kazi, biashara, elimu, mawasiliano na huduma mbalimbali za kidijitali. Tunataka kuhakikisha kwamba makazi ya kisasa yanaendana na mahitaji ya kisasa ya mawasiliano,” alisema Bi. Mugheiry.

Huduma hiyo inatarajiwa kuongeza thamani ya mradi huo kwa kuwawezesha wakazi kufanya shughuli mbalimbali kwa urahisi wakiwa majumbani. Kwa wakazi wanaofanya kazi kwa njia ya mtandao, wafanyabiashara, wanafunzi na familia, upatikanaji wa intaneti ya nyumbani utarahisisha matumizi ya mikutano ya mtandaoni, kujifunza, kufanya biashara kupitia majukwaa ya kidijitali, mawasiliano pamoja na huduma za Serikali mtandao.

Amani Residency, unaojengwa katika eneo la ekari 11, una jumla ya nyumba 82, zikiwemo villa 18 na apartment 64, pamoja na huduma mbalimbali za burudani na mapumziko. Uwepo wa huduma ya Faiba Mlangoni Kwako unaifanya miundombinu ya mawasiliano kuwa sehemu muhimu ya mazingira ya makazi hayo, sambamba na mahitaji ya maisha ya kisasa.

Kwa upande wa biashara, intaneti inayopatikana katika makazi inaweza kuwapa wakazi fursa ya kuendesha shughuli zao za kiuchumi kwa kutumia teknolojia, ikiwemo biashara za mtandaoni, masoko ya kidijitali, huduma za kifedha na mawasiliano ya kibiashara. Hali hiyo inaendana na juhudi za TTCL za kuchochea matumizi ya teknolojia na kuunganisha wananchi na fursa za uchumi wa kidijitali.

Aidha, uwezeshaji huo unaimarisha dhamira ya TTCL ya kusogeza huduma za mawasiliano kwa wananchi katika maeneo wanayoishi na kufanya shughuli zao, kwa kuzingatia kwamba intaneti imekuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku na kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kwa TTCL, kuwezesha Amani Residency kwa huduma ya Faiba Mlangoni Kwako ni zaidi ya kuunganisha makazi na intaneti; ni hatua ya kujenga mazingira ambayo yanawawezesha wananchi kuishi, kufanya kazi, kujifunza, kuwasiliana na kufanya biashara kwa kutumia teknolojia, sambamba na juhudi za taifa za kujenga uchumi unaotegemea zaidi huduma na fursa za kidijitali.





Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: