Na Denis Chambi Tanga.
WANANCHI Mkoani Tanga wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki Kliniki ya ardhi mkoani humo itakayoanzia katika wilaya ya Muheza ijifanyika kwa siku nne ili kupata elimu na huduma mbalimbali zinazotolewa na ofisi ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuwapatia hati sambamba na kutatua migogoro iliyopo.
Wito huo umetolewa na Kamishina msaidizi wa ardhi mkoa wa Tanga Jabir Singano wakati akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake kuelezea shughuli watakazozifanya katika Kliniki hiyo ambayo inafanyika kitaifa katika Mikoa yote ndani ya siku 10 ambapo kwa mkoa wa Tanga wameanza na wilaya za Muheza na Tanga.
"Kila mwaka kuanzia September 22 mpaka October 3 wizara tunakuwa kwenye siku kumi ya Kliniki ya ardhi na sisi mkoa wa Tanga tutazindua wilaya ya Muheza kwa siku nne kuanzia September 23 kisha tutarudi wilaya ya Tanga na kuendelea na Halmashauri nyingine, huduma zinazotolewa ni zile za ofisini tunajaribu kuzisogeza karibu na wananchi tukishirikiana na Halmashauri pamoja na Mabaraza ya ardhi" amesema Jabir.
Singano amesema kuwa kufuatia elimu waliyokuwa wanaendelea kuitoa kwa jamii migogoro ya ardhi mkoani humo imepungua kwa kiasi kikubwa ambapo mkakati uliopo sasa ni kuhakikisha wanaimaliza.
Aidha kamishna huyo amewataka wananchi kuacha kutumia madalali wakati wanapohitaji umiliki wa ardhi ambao wengi wamekuwa wakiwaingiza katika migogoro mbalimbali na wamiliki halali wa maeneo ambapo amewataka kuzitumia ofisi za ardhi pamoja na Halmashauri husika ili kuweza kupata huduma.
"Ofisi ya ardhi hatuna madalali ambao tunawatambua kisheria mwananchi kama anataka kujiridhidha na kitu chochote cha ardhi ni bora aje katika ofisi zetu rasmi au aende Halmashauri , unapouziwa eneo ni vyema ukajiridhidha na ofisi ya mipango miji kupitia Halmashauri kama ni eneo sahihi au sio sahihi" amesisitiza Kamishna huyo.
Katika hatua nyingine Kamishina Singano amewataka wamiliki wa ardhi mkoani humo ikiwemo wawekezaji kuzingatia mikataba waliyopewa baada ya kumilikishwa ardhi ikiwa ni pamoja na kuendeleza maeneo yao sambamba na kuweka alama za mipaka ili kuondokana na migogoro ya ardhi baina yao na wananchi ambayo inaweza kujitokeza.
Kwa upande wake Msajili wa hati Msaidizi mkoa wa Tanga Mwajuma Kihiyo amesema kuwa kupitia Kliniki hiyo ofisi ya ardhi mkoa wa Tanga imepanga kutoa hati kwa wananchi wote waliokamilisha taratibu zote za kuomba na kumiliki ardhi hivyo kuwaomba kutumia fursa hivyo kikamilifu.
"Tupo tayari kuwahudumia tumejipanga kutoa hati hivyo tunawasihi wale wananchi wote waliokamilisha taratibu zote kuja na nyaraka zao muhimu ambazo zinahusika ili tutakapozikagua kama ziko sawa tuweze kuwapatia hati zao" amesema Kihiyo.
Akizungumzia juu ya Mirathi Msajili huyo amesema kuwa mara nyingi kumekuwa na migogoro ya kifamiliya hasa pale anayepewa dhamana ya kugawa mali kwa wahusika anapochelewa kufanya hivyo ambapo wengi wamekuwa wakifikishana Mahakamani ambapo amewashauri wanaopewa dhamana hiyo kutokuwa kikwazo ambacho kinaweza kuzalisha migogoro baina ya walengwa.

Post A Comment: