Articles by "TANGA"
Showing posts with label TANGA. Show all posts

 


Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Mhandisi Juma Hamsini, ameitaka Kamati ya Lishe ya Jiji la Tanga, kuhakikisha wanaifikia jamii kwa kuipatia elimu ya lishe bora ili kuweza kubadilisha hali ya lishe ya familia, na hivyo kupata matokeo yaliyokusudiwa. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kamati hiyo, Mhandisi Hamsini amesema suala la lishe bora linatakiwa kuanzia nyumbani hadi kwenye maeneo ya kazi, na amemtaka Afisa Lishe wa Jiji kutayarisha na kuweka vipeperushi vya kukumbushia umuhimu wa kuzingatia lishe bora katika mlo, na kuangalia uwezekano wa kutenga fedha kwa ajili ya uanzishaji wa bustani na ufugaji katika shule za bweni kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi. 

Akiwasilisha taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa afua za lishe, Afisa Lishe wa Jiji la Tanga, Bi. Rehema Kirungi, amesema katika kipindi cha Julai 2024 - Juni 2025, shughuli mbalimbali za lishe zimefanyika ikiwemo ukusanyaji wa takwimu na uchambuzi kupitia nyenzo za kukusanyia taarifa za mwezi na kila robo mwaka. 

Kirungi amesema utambuzi wa hali ya lishe umefanyika kwa watoto 34,143 wa umri wa chini ya miaka mitano, ambapo watoto 57 (0.2 %) waligundulika na utapiamlo mkali na kufanyiwa matibabu. Amesema kitengo cha Lishe pia kimefanya usambazaji na ugawaji wa nyongeza ya matone ya Vitamini A, ambapo jumla ya watoto 42,433 (99%) wamefikiwa kati ya 42,660 waliotarajiwa.

Shughuli za lishe zinasimamiwa na kuratibiwa katika Idara ya Afya na utekelezaji wake unahusisha Idara mtambuka, pamoja na wadau mbalimbali wanao jishughulisha na afua za lishe.



SERIKALI ya wilaya ya Tanga imeipongeza Taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania kwa kujitolea kuendesha kambi maalumu ya matibabu ya macho bure  wananchi wa wilaya hiyo ambapo pia wanapatiwa   dawa , Miwani na kufanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho mara baada ya kugundulika kuwa na tatizo hilo.

Akizindua kambi hiyo iliyaonza 5 April 2025 katika  shule ya Sekondari Usagara Mkuu wa wilaya ya Tanga Japhari Kubecha ameipongeza taasisi hiyo ambayo inaendesha kambi hiyo kwa mara ya pili tangu ile ya mwaka 2019 kwa kuwatibu wananchi ambapo wengi wamekuwa na changamoto ya macho baada ya kufanyiwa vipimo.

Aidha Kubecha amesema kuwa Serikali ya wilaya  itaendelea kutoa ushirikiano kwa kwa taasisi hiyo  pamoja na wadau wengine ili kuhakikisha kuwa  wananchi wanapata huduma  mbalimbali ikiwemo za afya.

"Tumeona hamasa ni kubwa , ofisi ya mbunge pamoja na Serikali wametangaza kwa muda mfupi lakini muitikio umekuwa ni mkubwa sana sisi kama Serikali ya wilaya hatuna cha kuwalipa  taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania zaidi ya kuwashukuru wametufanyia hisani kubwa mno wananchi  na sisi kama Serikali ya wilaya tuwahakikishie kwamba tutaendelea kushirikiana nao kwa Kila hali"amesema Kubecha.

Aidha Mkuu huyo wa wilaya  amempongeza mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu kwa kuwaleta Wadau hao kuja kutoa matibabu hayo kwa wananchi ambapo wananchi wameendelea kujitokeza kuitumia fursa hiyo ambayo wengi wangeshindwa kuvipata kwa wakati kutokana na gharama za matibabu.

"Sisi kama Serikali ya wilaya ya Tanga tunampongeza sana mbunge  wa jimbo la Tanga kwa namna ambavyo ameendelea  wote tunafahamu kwamba mbunge hana fedha za kuhudumia watu lakini jinsi anavyotafuta fursa na kuzileta katika eneo lake binafsi nimpongeze na kumshukuru kwa hiki ambacho amekifanya ni sehemu ya  kuzisaidia Serikali yetu chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan " amesema Kubecha.

Mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu amewapongeza wananchi wa Jiji la Tanga wanaoendelea kujitokeza  kupatiwa huduma hiyo ambayo itahitimishwa April 7,2024 huku  akiwaasa kufuata maelekezo  na ushauri wa wataalamu wa afya  ikiwemo kuepuka kuvaa Miwani bila kufanyiwa vipimo ili kuepukana na madhara mbalimbali ya kiafya.

Aidha Ummy ameendelea kuwashukuru taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania Kwa jinsi wanavyohudumia wananchi pamoja na kampuni ya simu ya Yas ambao ndio waliodhamini kambi hiyo huku akiwaahidi wananchi kuendelea kuwaletea huduma mara tu zinapopatikana.

"Niendelee kuwashukuru wadau wetu kutoka Bilal Muslim Mission of Tanzania Kwa kuleta kambi hii hapa Tanga pamoja na wadau wengine better charitable trust na mtandao wa Yas na Mimi niwaahidi watu wa Tanga kuwa wajibu wangu kama mbunge ni kutafuta fursa kwaajili ya wananchi wa wilaya ya Tanga" amesema Ummy.

Daktari bingwa wa macho kutoka taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania   Hussein Abas ambaye pia ni mratibu wa macho  kwa Mkoa wa Tanga amesema kuwa kuwa katika Mkoa wa Tanga zaidi ya asilimia 50 ya wananchi wameathirika na magonjwa ya macho ikiwemo mtoto wa jicho ambapo wengi wanalazimika kufanyiwa upasuaji ili kuondokana na changamoto hiyo.

Mpaka sasa ikiwa ni siku ya pili  zaidi ya watu 1500 waliojitokeza katika kambi hiyo  wametibiwa na kupatiwa dawa pamoja na Miwani huku 84 kati yao waligundulika kuwa na tatizo la mtoto wa jicho kufanyiwa upasuaji katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tanga Bombo.

Kambi hiyo ambayo imeanza kufanyika April 5 ikitarajiwa kuhitimishwa April 6 wananchi wameendelea kujitokeza kwa kupatiwa matibabu ambapo wengi wameeleza kupona akiwemo Mwanarabu Yusuph aliyesumbuliwa na matatizo ya macho tangu mwaka 2005.






Na Denis Chambi, Tanga.

MKUU wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda Buriani amewaagiza wakuu wa wilaya , makatibu tawala na wakurugenzi wa halmashauri zote za mkoa huo kutembelea na kujionea utendaji wa kituo cha sayansi cha stem Park ili elimu teknologia inayotolewa kwa wanafunzi wanqotembelea kituoni hapo iweze kutolewa ngazi zote.

Balozi Dkt Buriani amesema hayo wakati akifunga maadhimisho ya kusherehekea miaka mitano  ya kuanzishwa kwa kituo cha sayansi cha Stem Park tangu  kilipoanzishwa 2020 ambapo amepongeza elimu inayotolewa na wataalamu wa kituo hicho kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari zilizopo ndani ya halmashauri ya Jiji la Tanga  ambayo imeonekana kuwa na tija kulingana na Maendeleo ya teknologia ya sasa.

"Tutaelekeza wakurugenzi, wakuu wa wilaya na makatibu tawala wote wa wilaya ya mkoa wetu waje watembelee ili iende chini kwenye wilaya zetu zote  na hatimaye ikawe ni mkombozi kwa vijana wetu wote, tunatamani hii fursa wanayoipata watu wa Tanga Jiji waipate na maeneo yote ya mkoa wetu"

Aidha amewataka wadau wa elimu mkoani humo Kwa kushirikiana na walimu na wazazi  kuendelea kuwaunga mkono Sterm Park  kwa kazi wanayoifanya  chini ya shirika la Botner Foundation.

"Ni jambo kubwa mnalolifanya hapa na uwekezaji mkubwa mliouweka hapa matunda yake tumeuanza kuyaona , kupitia dira ya 2050 ambayo tunakwenda nayo kwa sasa , hiki kinachofanywa na kituo cha Sterm Park ndio mambo ambayo yako duniani kote maswala ya ubunifu , uhandisi na kupelekea ukuaji wa uchumi Dunia"

Aidha Dkt Buriani ameongeza kuwa  Sera ya elimu inayotekelezwa na  Serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan imebeba maono ya kufanya Mapinduzi katika sekta  ya elimu hapa nchini. 

"Kutokana na maono ya Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan kwamba sasa tuanzishe shule za sayansi hasa kwa watoto wa kike, masomo ya sayansi hasa hisabati yalikuwa yanafelisha sana kipindi cha nyuma lakini kupitia mfumo huu wa kuwepo na shle za sayansi kumebadilisha sana mtazamo wa wanafunzi, masomo haya yamekuwa rafiki zaidi utaalam wa ufundiahaji umeongezeka".alisema.

Mkurugenzi mtendaji wa kituo hicho cha Sterm Park Luidiko Mhamelawa ameeleza kuwa  miaka mitano tangu kuanzishwa kwa kituo hicho imeleta mabadiliko chanya husausan kwa wanafunzi wa shule za msingi ambao wamekuwa wakiongezeka na kuhamasika kujitika tatika masomo ya sayansi.

Amesema mwenendo huo kituo kina kazi ya ziada  ya kufanya kwa miaka mingine ijayo  kuhakikisha mabadiliko ya sera mpya ya elimu iliyojikita kwenye masuala ya  teknologia inawapa nguvu  na matumaini kuwa ushirikiano wao  pamoja na wadau utazidi kuwa na mafanikio.

"Tunaposherejekea  miaka mitano tangu kuanzishwa kwa kituo cha Sayansi cha Sterm Park hapa  Tanga   imekuwa ni miaka ya furaha sana tumefikia watoto wengi zaidi"

"Kwa miaka mitano inayokuja tunapata  hamasa kubwa kupitia sera mpya ya elimu ambayo ina msisitizo kwenye kujivunza kwa vitendo na matumizi ya teknologia katika ufundishaji sasa sera hii inatupa nguvu sisi kuona kuwa tunaweza kuwa washirika wakubwa wa Serikali kwaajili ya utekelezaji wa sera hii mpya" alisema Mhavilawa.

Alisema ili kupanua wigo wa elimu wanayoitoa kituoni hapo  wameanziaha Klabu mbalimbali katika shule za msingi na sekondari ambapo mpaka sasa 22 wakitarajia kufikia mkoa mzima wa Tanga.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa uwepo wa kituo hicho jijini Tanga na matokeo yake ambayo yameanza kuonekana kimewavutia wadau wengine kutoka katika wilaya na mikoa mingine  alisema kuwa ushirikiano mzuri  utakaowekwa baina yao na Serikali utasaidia kuanzishwa vituo vingine hapa nchini.

"Kwa sasa tumeshavuka malengo yetu ya awali tunategemea tufikie Tanga nzima lakini hiki kituo kumekuwa na mvuto kwa mikoa mingine kupitia wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali wote  wanatamani kuwa na kituo kama hiki kwahiyo tunategemea ushirikiano mzuri wa Serikali ili kueneza elimu hii ya kujifunza kwa vitendo " alisema Mkurugenzi huyo.

Akizungumza kwa niaba ya halmashauri ya Jiji la Tanga Naibu Meya wa Baraza la madiwani Rehema Mhina amepongeza uwepo wa kituo hicho ambao umeanza kuzaa matunda  huku akiwaahidi kuendelea ushirikiano baina yao na kituo.

"Niwapongeze sana watekel zaji wa mradi huu ambao umeanza  kuleta matokeo ya kuonekana  tumejitahidi sana kuhamasisha watoto kupenda masomo ya sayansi katika Jiji letu la Tanga"

Amewataka wazazi na walezi kuendelea kuonyesha ushirikiano kwa kuwahimiza watoto wao kupenda masomo ya sayansi sambamba na kupambana na vitendo vya ukatili.


RAIS Dkt Samia Suluhu Hassan,amerudisha matumaini  kwa wananchi  wa kijiji cha Kimbanga Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma,baada ya kutoa  kiasi cha Sh.milioni 60 kwa ajili ya kuchimba kisima cha maji ili kumaliza kero ya huduma ya maji safi na salama iliyokuwepo kwa muda mrefu  katika kijiji hicho.

Kwa sasa,wakazi wa kijiji cha Kimbanga wanatembea umbali wa kilometa 1 hadi 2 kila siku kwenda vijiji vya jirani kutafuta maji,jambo linalowarudisha nyuma kimaendeleo licha ya kuwa wakulima wazuri wa mazao ya chakula na biashara ikiwemo zao maarufu la Kahawa.

Akizungumza na wakazi wa kijiji hicho Kaimu Meneja wa Ruwasa Wilayani Nyasa Athuman Chola alisema,Ruwasa Wilaya ya Nyasa imepokea Sh.milioni 300 zilizoletwa na Rais Samia Suluhu Hassan ili kuchimba visima vya maji katika vijiji vitano ikiwemo kijiji cha Kimbanga.

Alisema,katika kijiji cha Kimbanga kazi ya kuchimba kisima imekamilika na sasa wanaendelea kujenga kioski cha kuchotea maji ambacho ujenzi wake umefikia asilimia zaidi ya 40.

Chalo ametaja kazi ya zilizobaki ni kusambaza  mabomba ya maji kwenda kwenye makazi ya Wananchi,kujenga vituo vya kuchotea,kufunga mashine ya kusukuma maji kutoka kwenye kisima na kupeleka kwenye tenki na kufunga umeme jua.

“mpaka sasa tumefanikiwa kuchimba kisima katika Kijiji cha Kimbanga pekee na kwenye vijiji vinne tumeshindwa kupata maji chini ya ardhi,hata hivyo tutatumia njia mbadala ikiwemo kuboresha chamchem na kujenga miradi ya mserereko  kwa kutoa maji milimani na kupeleka kwa wananchi”alisema Chola.

Aidha alisema,katika kijiji cha Malamala wanaendelea kufanya usanifu upya kwani imeshindikana kupata chanzo cha maji cha uhakika na watashirikiana na mamlaka  ya Bonde la Ziwa Nyasa ili wananchi waweze kupata maji ya uhakika.

Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,kwa kutenga fedha ili kutekeleza miradi ya maji katika vijiji mbalimbali ambayo  inalenga kupunguza na kumaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

Baadhi ya Wakazi wa kijiji cha Kimbanga,wameishukuru Serikali  kupitia Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kwa uamuzi wa kutatua changamoto ya maji safi na salama katika kijiji chao.

Adelius Mwingira alisema,mradi wa kisima utasaidia kuwaondolea kero ya muda mrefu ya kutumia maji  ya visima vya asili ambavyo maji yake siyo safi na salama pamoja na mateso ya kubeba ndoo za maji  kichwani kila siku.

Bonus Kapinga alisema,mradi wa kisima ni ukombozi mkubwa kwao kwa sababu kijiji hicho tangu kilipoanzishwa miaka zaidi ya 50 hakijawahi kupata mradi wa maji ya bomba badala yake wanatumia maji kutoka vyanzo vingine vya asili kama mito na mabonde yanayop kando kando ya kijiji hicho.

Alisema,kero hiyo inasababisha hata  maendeleo ya kitaalum kwa wanafunzi wa shule ya msingi kuwa chini kwa kuwa muda wa masomo wanafunzi wanakutumia kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

William Komba,ameishukuru Serikali kupeleka mradi wa kisima cha maji,lakini ameiomba Serikali kupitia Ruwasa kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa  kisima hiko haraka na kufikisha mtandao wa maji kwenye makazi ya wananchi ili wasiendele kuteseka kwa kutembea umbali mrefu hadi kwenye vituo vya kuchotea maji.

Mafundi wakiendelea na ujenzi wa kioski cha kuchotea maji katika kijiji cha Kimbanga Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma kupitia mradi wa uchimbaji visima 900/5 kwa kila Jimbo ambapo Wilaya ya Nyasa imepata visima vitano vitakavyochimbwa kwa gharama ya Sh.milioni 300.

 Na Oscar Assenga, Handeni.



WATU 11 wamefariki dunia wa Kijiji cha Chang’ombe kilichopo Kata ya Segera wilayani Handeni Mkoani Tanga baada ya kugongwa na lori lililokuwa limebeba saruji baada ya kupoteza uelekeo wakati walipojitokeza barabarani walipokuwa wakishanga ajali ya gari dogo aina ya tata .

Watu hao walijitokeza barabarani ili kuweza kutoa msaada kufuatia ajali ya barabarani ya gari dogo aina ya Tata ndipo walipokumbana na ajali hiyo iliyopelekea kupoteza maisha..

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Batilda Burian lori hilo liliwagonga watu hao usiku wa kuamkia Januari 14,2025 na kusababisha vifo hivyo pamoja na majeruhi.

Lori hilo lenye namba za usajili T.680 BQW likiwa linatokea Tanga lilifeli breki na kuwagonga watu waliokuwepo pembezoni mwa barabara na kusababisha vifo vya watu 11 papo hapo na kujeruhi wengine 11.

Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya wilaya ya Korogwe Magunga na majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo .


Hata hivyo Mkuu wa Mkoa huyo alitoa pole kwa familia za marehemu na kuwatakia nafuu ya haraka majeruhi wote .

Mkuu huyo wa Mkoa alitoa wito kwa madereva na wamiliki wa vyombo vya moto kuhakikisha magari yao yanakuwa katika hali nzuri ya kiufundi ili kuepusha ajali za namna hiyo.


 



Bodaboda nao wachangia milioni  1 kwa ajili ya fomu ya Rais Dkt Samia

Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Ummy Mwalimu amefanya kikao na viongozi na madereva wa Bodaboda zaidi ya mia tano (500) kupitia Umoja wa Madereva wa Pikipiki na Bajaji  Wilaya ya Tanga (UWAPIBATA) kuzungumzia masuala ya maendeleo ya Bodaboda Tanga Mjini ambapo pamoja na mengineyo Bodaboda kupitia Mwenyekiti wao Mohamedi Chande walimuomba Mh Ummy kuwaunga mkono ili kutunisha Mfuko wao wa  kukopeshana pesa za Leseni kwa Bodaboda. 

Mhe Ummy alikubali ombi hilo na kuwachangia kiasi cha shilingi milioni 10 sambamba na kuwataka bodaboda wengi zaidi kujiunga katika Umoja huo ili kuweza kunufaika na fursa mbalimbali ili kufanya shughuli zao katika mazingira mazuri zaidi.

Wakati huo huo, Bodaboda wa Wilaya ya Tanga kupitia UWAPIBATA wamechangia shilingi miloni moja kwa ajili ya Fomu ya Urais wa Dkt Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi nzuri za maendeleo kwa watu wa Tanga ikiwemo maboresho ya Bandari ya Tanga ambao yameongeza fursa za wateja kwa Bodaboda.

Mhe Ummy alimeshukuru Bodaboda kwa kuchangia Fomu ya Rais Dkt Samia Suluhu na amesema kuwa Mh Rais anastahili kutiwa moyo na kuungwa mkono. 

Aidha ameahidi atashirikiana nao bega kwa bega kutafuta kura za Rais Samia na pia kutafuta wadau mbalimbali ili kuboresha shughuli za bodobda. Sambamba na hilo Mhe Ummy alitoa ofa ya mafuta lita mbili kwa bodaboda wote waliohudhuria.

Shughuli hiyo ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tanga Ndg.Meja mst.Hamisi Mkoba, katibu wa UVCCM Wilaya ya Tanga ndugu Salim Dede, viongozi wa bodaboda wakiongozwa na mwenyekiti wake ndg. Mohamed Chande.

Imetolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini.













 Wajiolojia kutoka ndani na nje ya nchi ya Tanzania wamewasili Jijini Tanga kwa ajili ya Mkutano wao wa mwaka (TGS 2024) utakaofanyika Desemba 04 hadi 06, 2024 katika Hoteli ya Tanga Beach Resort Jijini hapo.


Leo, Desemba 01, 2024 wajiolojia hao wameanza kwa kufanya ziara katika maeneo mbalimbali ya kijiolojia kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu jiolojia ya Tanga na kujionea aina ya miamba iliyopo.

Pamoja na kutembelea maeneo ya kijiolojia, washiriki hao watatembelea maeneo ya kitalii na kihistoria kama vile Magoroto, Makumbusho ya Tanga, Mapango ya Amboni, na Forodhani.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wajiolojia wanaoshiriki ziara hiyo wamesema maeneo waliyotembelea na wanayoendelea kutembelea yamewapa kufurahia uwepo wao Tanga, kuongeza uelewa wao juu ya historia ya Tanga na jiolojia yake.

Kwa historia, Jumuiya ya Wajiolojia Tanzania (The Tanzania Geological Society - TGS) ilianzishwa mwaka 1969 kwa lengo la kuwaunganisha watanzania wote waliosomea masuala ya jiolojia na jiosayansi.

Tangu kuanzishwa kwake, Jumuiya hii imefanyika jukwaa adhimu kwa wanajiolojia na wanajiosayansi wakitanzania kupeana taarifa za kitaalamu, kubadilisha uzoefu na kujadili masuala yanayohusu utafutaji na uendelezaji wa rasilimali za madini, mafuta, gesi asilia, maji na joto ardhi.
 Sehemu ya wajiolojia waliowasili Jijini Tanga na kushiriki ziara ya mafunzo iliyofanyika Desemba 01, 2024. Mkutano wa mwaka wa wajiolojia utafanyika Desemba 04 hadi 06, 2024 Jijini Tanga.

Sehemu ya wajiolojia waliowasili Jijini Tanga na kushiriki ziara ya mafunzo iliyofanyika Desemba 01, 2024. Mkutano wa mwaka wa wajiolojia utafanyika Desemba 04 hadi 06, 2024 Jijini Tanga.

Sehemu ya wajiolojia waliowasili Jijini Tanga na kushiriki ziara ya mafunzo iliyofanyika Desemba 01, 2024. Mkutano wa mwaka wa wajiolojia utafanyika Desemba 04 hadi 06, 2024 Jijini Tanga.

Sehemu ya wajiolojia waliowasili Jijini Tanga na kushiriki ziara ya mafunzo iliyofanyika Desemba 01, 2024. Mkutano wa mwaka wa wajiolojia utafanyika Desemba 04 hadi 06, 2024 Jijini Tanga.

 


Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tanga Mjini, Eng. Juma Hamsini, amewataka Wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika Jiji la Tanga, kutumia vikao rasmi katika kufanya maamuzi, badala ya kufanya mambo kienyeji kwa kufahamiana. 

Eng. Hamsini ameyasema hayo wakati akizungumza na viongozi hao mara baada ya kukamilika kwa zoezi la kuapishwa kwao, lililofanyika leo kufuatia ushindi walioupata katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa uliofanyika jana, Jumatano, Novemba 27, 2024, katika mitaa 181 ya Jiji la Tanga.

Hamsini amesema kama jambo linahusu jamii, au serikali, viongozi hao wana wajibu wa kuitisha vikao na kutatua jambo hilo ambalo litaingia kwenye kumbukumbu za vikao. 

Akizungumzia suala la usafi wa mji, Eng. Hamsini ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, amesema tayari Halmashauri ipo kwenye mpango wa kubinafsisha shughuli za uzoaji taka, na tayari wazabuni watano wamepatikana. Na hivyo amewataka viongozi hao kuhamasisha ulipaji wa ada ya uzoaji taka. 

Hamsini pia amesema Jiji lina lengo la kufunga taa za barabarani zipatazo 1500, ambapo tayari taa 300 zimeanza kufungwa na taa 1200, zitapatikana kupitia mradi wa TACTIC.

Aidha ameahidi kuwapatia mafunzo ya juma moja (wiki moja) Wenyeviti hao, ili waweze kujua majukumu yao.


Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Mhandisi Juma Hamsini, amewataka wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi na wasimamizi wa vituo, kuzingatia falsafa ya 4R (Reconciliation- maridhiano, Reforms- mabadiliko, Resilience- ustahimilivu, na Rebuilding- kujenga upya) katika kufanya kazi zao.

Mhandisi Hamsini ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya siku moja ya Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi na wasimamizi wa vituo, yaliyofanyika leo, Jumatatu Septemba 30, 2024, katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Galanos Jijini Tanga.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni mtenda haki, na hivyo amewataka watendaji hao wa uchaguzi kutenda haki kwa kufuata miongozo, kanuni na sheria, ili uchaguzi uweze kufanyika vizuri na kuisha kwa usalama na amani. 

Kufanyika kwa mafunzo haya ni mfululizo wa matukio ya maandalizi kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 27\/11\/2024, ukiwa na kauli mbiu isemayo; "Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki uchaguzi".













Halmashauri ya Jiji la Tanga imefungua dirisha la utoaji mikopo ya asilimia 10% ya mapato ya ndani Kwa kina mama, vijana na watu wenye ulemavu,  kuanzia leo tarehe 29 Septemba 2024, na litakuwa wazi kwa mwezi mmoja, na kufungwa October 29 ambapo Serikali imefanya maboresho ya sheria na kanuni za mikopo hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake,  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga Mhandisi Juma Hamsini, amesema Halmashauri imeidhinisha kiasi cha zaidi ya shilingi Billion 3, ambapo ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanachagua biashara yenye manufaa na si kuiga biashara ambazo hawana elimu nazo, huku akitoa wito Kwa maafisa mikopo kujiepusha na undugu, na kufuata kanuni zilizowekwa na Serikali.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii wa Jiji la Tanga Simon Mndende amesema kuwa matarajio yao kwa Halmashauri nikuhakikisha wanakopesha vikundi visivyo pungua 135 ndani ya kata 27 zilizopo Jijini humo.

Mndende amesema kwa marekebisho ya sheria yaliofanyika   kikundi ndio dhamana ya mkopo, japo kila mwanakikundi ana uhuru wa kufanya biashara tofauti ndani ya kikundi.

Mwezi Aprili, 2023 serikali ilisitisha utoaji wa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani nchi nzima kutokana na changamoto mbalimbali kama vile vikundi kutorejesha mikopo kwa wakati. Baada ya hapo serikali iliunda timu ya kuandaa maboresho ya utoaji na usimamizi wa mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mapendekezo yaliyotolewa na timu iliyoundwa yamepelekea kuandaliwa Kanuni mpya za utoaji na usimamizi wa mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu za mwaka 2024. Pamoja na mambo mengine, kanuni mpya zimeongeza sifa ya umri wa vijana kutoka miaka 18 - 35 ya awali na kuwa miaka 18 - 45.






Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Mhandisi Juma Hamsini, leo Jumatatu, Septemba 23, 2024, amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya sekta ya elimu sekondari, kuangalia hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi, na kuondoa changamoto zinazochelewesha ukamilishaji wa miradi hiyo.

Katika ziara hiyo, Mhandisi Hamsini alianza kwa kutembelea ujenzi wa mabweni mawili katika shule ya Sekondari ya Ufundi Tanga, Tanga Technical Secondary School, ambayo yapo kwenye hatua za umaliziaji, yanayojengwa kwa fedha za  Mradi wa Programu ya Kutekeleza Elimu kwa Matokeo (EP4R) kwa gharama ya shilingi milioni 260, na uwezo wa kulala jumla ya wanafunzi 160. 

Akiwa shuleni hapo, Mhandisi Hamsini alisisitiza kukamilika kwa kazi ndani ya muda na wanafunzi kuhamia kwenye mabweni hayo kama ilivyopangwa, na amepongeza hatua za umaliziaji zilivyofikia.

Mhandisi Hamsini pia ametembelea shule za Sekondari za Msambweni, Galanos na MACECHU, ambapo katika shule zote hizo, ameweza kukagua miradi ya ujenzi wa madarasa, matundu ya vyoo, Bweni na nyumba za watumishi, ambavyo vinajengwa kwa fedha za Serikali Kuu na mapato ya ndani, na kutoa maelekezo kwa Mhandisi na Mchumi wa Jiji kuhakikisha wanapeleka nguvu ya kukamilisha miradi hiyo ili iweze kutoa huduma kwa jamii. 

Ziara hii ya kutembelea miradi ya sekta ya elimu ni ya pili kwa Mkurugenzi Hamsini, tangu ahamie Jiji la Tanga, ambapo ziara yake ya kwanza alianzia kwenye sekta ya afya, aliyoifanya kwa siku mbili, kuanzia Septemba 17, 2024, na alitembelea na kukagua miradi 11.