Articles by "ZIARA TANGA"
Showing posts with label ZIARA TANGA. Show all posts

Na Denis Chambi, Tanga.

MKUU wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda Buriani amewaagiza wakuu wa wilaya , makatibu tawala na wakurugenzi wa halmashauri zote za mkoa huo kutembelea na kujionea utendaji wa kituo cha sayansi cha stem Park ili elimu teknologia inayotolewa kwa wanafunzi wanqotembelea kituoni hapo iweze kutolewa ngazi zote.

Balozi Dkt Buriani amesema hayo wakati akifunga maadhimisho ya kusherehekea miaka mitano  ya kuanzishwa kwa kituo cha sayansi cha Stem Park tangu  kilipoanzishwa 2020 ambapo amepongeza elimu inayotolewa na wataalamu wa kituo hicho kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari zilizopo ndani ya halmashauri ya Jiji la Tanga  ambayo imeonekana kuwa na tija kulingana na Maendeleo ya teknologia ya sasa.

"Tutaelekeza wakurugenzi, wakuu wa wilaya na makatibu tawala wote wa wilaya ya mkoa wetu waje watembelee ili iende chini kwenye wilaya zetu zote  na hatimaye ikawe ni mkombozi kwa vijana wetu wote, tunatamani hii fursa wanayoipata watu wa Tanga Jiji waipate na maeneo yote ya mkoa wetu"

Aidha amewataka wadau wa elimu mkoani humo Kwa kushirikiana na walimu na wazazi  kuendelea kuwaunga mkono Sterm Park  kwa kazi wanayoifanya  chini ya shirika la Botner Foundation.

"Ni jambo kubwa mnalolifanya hapa na uwekezaji mkubwa mliouweka hapa matunda yake tumeuanza kuyaona , kupitia dira ya 2050 ambayo tunakwenda nayo kwa sasa , hiki kinachofanywa na kituo cha Sterm Park ndio mambo ambayo yako duniani kote maswala ya ubunifu , uhandisi na kupelekea ukuaji wa uchumi Dunia"

Aidha Dkt Buriani ameongeza kuwa  Sera ya elimu inayotekelezwa na  Serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan imebeba maono ya kufanya Mapinduzi katika sekta  ya elimu hapa nchini. 

"Kutokana na maono ya Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan kwamba sasa tuanzishe shule za sayansi hasa kwa watoto wa kike, masomo ya sayansi hasa hisabati yalikuwa yanafelisha sana kipindi cha nyuma lakini kupitia mfumo huu wa kuwepo na shle za sayansi kumebadilisha sana mtazamo wa wanafunzi, masomo haya yamekuwa rafiki zaidi utaalam wa ufundiahaji umeongezeka".alisema.

Mkurugenzi mtendaji wa kituo hicho cha Sterm Park Luidiko Mhamelawa ameeleza kuwa  miaka mitano tangu kuanzishwa kwa kituo hicho imeleta mabadiliko chanya husausan kwa wanafunzi wa shule za msingi ambao wamekuwa wakiongezeka na kuhamasika kujitika tatika masomo ya sayansi.

Amesema mwenendo huo kituo kina kazi ya ziada  ya kufanya kwa miaka mingine ijayo  kuhakikisha mabadiliko ya sera mpya ya elimu iliyojikita kwenye masuala ya  teknologia inawapa nguvu  na matumaini kuwa ushirikiano wao  pamoja na wadau utazidi kuwa na mafanikio.

"Tunaposherejekea  miaka mitano tangu kuanzishwa kwa kituo cha Sayansi cha Sterm Park hapa  Tanga   imekuwa ni miaka ya furaha sana tumefikia watoto wengi zaidi"

"Kwa miaka mitano inayokuja tunapata  hamasa kubwa kupitia sera mpya ya elimu ambayo ina msisitizo kwenye kujivunza kwa vitendo na matumizi ya teknologia katika ufundishaji sasa sera hii inatupa nguvu sisi kuona kuwa tunaweza kuwa washirika wakubwa wa Serikali kwaajili ya utekelezaji wa sera hii mpya" alisema Mhavilawa.

Alisema ili kupanua wigo wa elimu wanayoitoa kituoni hapo  wameanziaha Klabu mbalimbali katika shule za msingi na sekondari ambapo mpaka sasa 22 wakitarajia kufikia mkoa mzima wa Tanga.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa uwepo wa kituo hicho jijini Tanga na matokeo yake ambayo yameanza kuonekana kimewavutia wadau wengine kutoka katika wilaya na mikoa mingine  alisema kuwa ushirikiano mzuri  utakaowekwa baina yao na Serikali utasaidia kuanzishwa vituo vingine hapa nchini.

"Kwa sasa tumeshavuka malengo yetu ya awali tunategemea tufikie Tanga nzima lakini hiki kituo kumekuwa na mvuto kwa mikoa mingine kupitia wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali wote  wanatamani kuwa na kituo kama hiki kwahiyo tunategemea ushirikiano mzuri wa Serikali ili kueneza elimu hii ya kujifunza kwa vitendo " alisema Mkurugenzi huyo.

Akizungumza kwa niaba ya halmashauri ya Jiji la Tanga Naibu Meya wa Baraza la madiwani Rehema Mhina amepongeza uwepo wa kituo hicho ambao umeanza kuzaa matunda  huku akiwaahidi kuendelea ushirikiano baina yao na kituo.

"Niwapongeze sana watekel zaji wa mradi huu ambao umeanza  kuleta matokeo ya kuonekana  tumejitahidi sana kuhamasisha watoto kupenda masomo ya sayansi katika Jiji letu la Tanga"

Amewataka wazazi na walezi kuendelea kuonyesha ushirikiano kwa kuwahimiza watoto wao kupenda masomo ya sayansi sambamba na kupambana na vitendo vya ukatili.


Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Nishati kufanya mapitio ya sera ya usafirishaji wa mafuta nchini ili kuyawezesha makampuni yanayosambaza mafuta ukanda wa Kaskazini kutumia Bandari ya Tanga kupitia GBP.

Rais Samia ameyasema hayo leo machi 1, 2025 wakati akiweka jiwe la msingi ujenzi wa ghala la kupokelea gesi ya kupikia ya  LPG katika kampuni ya  BGP ikiwa ni mwendelezo wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo mkakati unasema ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia. 


"Hii kazi wanaifanya vizuri sana wao kama GBP, lakini wale ambao wanachukua mafuta kwa ajili ya usambaza ukanda huu, au kupeleka nje ya nchi kupitia kaskazini bado wanachukulia mafuta Dar es Salaam, nendeni mkafanye mapitio ya Sera". Aliagiza Dkt. Samia. 

Dkt. Samia amesema GBP  Tanga inayo mafuta ya kutosha kusambaza kanda ya Kaskazini pamoja na Nchi zilizo ukanda wa kasikazini hivyo hakuna sababu ya wasambazaji hao wa mafuta kuyachukulia Dar es Salaam. 

Aisha, Rais Samia ameipongeza GBP kwa hatua iliyochukua ya kuanzisha vituo vya kujaza gesi kila Mkoa na kuongeza kuwa Serikali inaunga mkono uwekezaji huo.

Amewahakikisha wawekezaji Serikali kuweka Sera rafiki na endelevu zitakazotabirika na sera zitakazowawezesha wawekezaji wa Tanzania kuwa washindani katika soko la ndani na soko la kimataifa.

Awali Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga kabla ya kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema Jiji la Tanga  ni muhimu ndani ya sekta ya nishati kwani ndio kitovu cha kupokea na kusambazaji wa mafuta Mikoa ya Kaskazini na Nchi za Ukanda wa Kasikazini. 

"Wenzetu wa GBP ni washirika wa kiuchumi wa sekta ya nishati hususani kwenye sekta ndogo ya mafuta kwa sababu maghala yao ndio yanatumika kupokea na kusambaza mafuta kwa upande wa Kaskazini". Amesema Mhe. Kapinga. 

Mhe. Kapinga amempongeza Rais kwa kuweka chachu na msukumo wa Sera nzuri katika uwekezaji ambazo zinawafanya wawekezaji hao waendelee kuwekeza katika sekta ya nishati.

Ameongeza kuwa Serikali kupitia TIC imekuwa iki support wawekezaji kwa kuchukua hatua za kikodi ambazo zimekuwa rafiki ikiwa ni pamoja na uondoaji wa kodi za ongezeko la thamani kwenye vifaa vya LPG.

Mhe. Kapinga amesisitiza kuwa sera nzuri za uwekezaji zilizopo zimewaongezea hari wawekezaji wa ndani wa kuwekeza kitokana na kuweza kudhindana na wawekezaji wanaoleta vifaa kutoka nje ya Nchi

Aidha, kutokana na mfumo wa soko uliopo katika nishati safi ya kupikia viwanda vimekuwa vikiongezeka vya utengenezaji wa gesi za majumbani.

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Jumamosi Machi Mosi, 2025 amefanya ziara katika Bandari ya Tanga kukagua maboresho makubwa yaliyofanyika, yakiwemo ujenzi wa gati mbili mpya. 

Katika ziara hiyo, Rais Samia ameeleza kuridhishwa na kazi iliyofanyika, akisisitiza kuwa Tanga sasa inajipambanua kama lango muhimu la biashara kwa Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla.

"Tulitamani kwa muda mrefu kuona meli kubwa zikitia nanga katika Bandari ya Tanga, shughuli za bandari zikishamiri, na vijana wengi wakipata ajira. Leo hii, hayo yote yamewezekana kwa uwekezaji wa Shilingi bilioni 429 uliofanywa katika maboresho ya bandari hii," alisema Rais Samia.

Maboresho hayo yameongeza kina cha maji bandarini, kuwezesha meli kubwa kufunga moja kwa moja kwenye gati, tofauti na awali ambapo mizigo ilikuwa inashushwa baharini kisha kusafirishwa kwa matishari.

 Maboresho hayo pia yamesaidia kupunguza muda wa kuhudumia meli kutoka siku kadhaa hadi siku mbili pekee.

Kwa sasa, Bandari ya Tanga imeongeza uwezo wake wa kuhudumia mizigo kutoka tani 400,000 mwaka 2019/2020 hadi tani 1,200,000 hivi sasa , ikiwa ni ongezeko la zaidi ya tani 700,000. 

Mapato nayo yameongezeka mara mbili, kutoka Shilingi bilioni 17.27 hadi kufikia rekodi ya Shilingi bilioni 49 kwa miezi saba pekee ya mwaka huu wa fedha.

Rais Samia amebainisha kuwa, maboresho hayo yatanufaisha siyo tu wafanyabiashara bali pia serikali kupitia ongezeko la mapato na ukuaji wa sekta ya viwanda

. "Natamani kurudisha hadhi ya Tanga – iwe Tanga ya viwanda, bandari kubwa na pia Tanga ya uvuvi. Hiki ndicho ninachokifanya," alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ametangaza mpango wa kujenga barabara ya Handeni-Kiberashi-Kijungu-Singida (KM 340) kwa mfumo wa ubia kati ya serikali na sekta binafsi (PPP). 

Amesema barabara hiyo itakuwa muhimu kwa usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Tanga kwenda maeneo mbalimbali nchini na kimataifa. "

Tutaiwekea road tolls (tozo za barabara)ili mwekezaji anayejenga barabara hii aweze kurudisha gharama zake," alisema.

Akihitimisha hotuba yake, Rais Samia amewataka wafanyakazi wa bandari kufanya kazi kwa ufanisi ili kushindana na bandari nyingine za kimataifa, huku akihimiza matumizi ya teknolojia za kisasa. 

"Tunashindana na bandari za mataifa mengine. Tukifanya kazi kwa bidii na kupunguza gharama za uendeshaji, Bandari ya Tanga itakuwa kitovu cha biashara Afrika Mashariki," alihimiza.

Kwa maboresho hayo, Bandari ya Tanga imechukua nafasi yake kama lango muhimu kwa uchumi wa Tanzania, ikiwa na uwezo wa kuhudumia meli kubwa zaidi na kurahisisha biashara kati ya Tanzania na mataifa mengine duniani.





















Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Ummy Mwalimu, amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuleta maendeleo katika Jiji la Tanga na Tanzania kwa ujumla.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa CCM Mkwakwani leo Ijumaa Februari 28, 2025 ambapo Rais Samia ni mgeni rasmi, Ummy Mwalimu amewahakikishia wakazi wa Tanga kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ambayo imeleta mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali.

Katika sekta ya elimu, Rais Samia amewezesha ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari, pamoja na madarasa mapya, ununuzi wa madawati, na kuendeleza sera ya elimu bila malipo.

 Pia, sekta ya afya imeimarishwa kwa kujengwa kwa vituo vya afya, zahanati, na kuboresha hospitali ya Rufaa ya Bombo na hospitali ya Wilaya ya Masiwani.

Mbunge huyo wa Tanga Mjini ameeleza kuwa, kwa upande wa miundombinu, Tanga sasa inapendeza kwa barabara za lami, taa za barabarani, na maboresho ya mifereji. Mradi wa barabara ya Tanga hadi Pangani umepewa kipaumbele, ambapo mkandarasi amelipwa Shilingi bilioni 10 ili kukamilisha ujenzi wake.

Katika sekta ya maji, Ummy amesema, Rais Samia amefanikisha upatikanaji wa maji safi kwa kata mbalimbali za Tanga kupitia mpango wa ‘Kijani Bond,’ ambao umetengewa zaidi ya Shilingi bilioni 54.

"Rais Samia ameleta mageuzi makubwa katika bandari ya Tanga kwa kuwekeza Shilingi bilioni 249.1, hatua ambayo imewezesha kupokea meli kubwa, kuongeza fursa za ajira, na kuchochea biashara. Pia, ujenzi wa masoko mapya kama soko la Makorora, soko la samaki Deep Sea, na soko la Mgandini umeendelea kuimarisha uchumi wa wananchi." alisema Ummy 

Mbunge Ummy amewasilisha maombi ya wakazi wa Tanga kwa Rais Samia, ikiwa ni pamoja na kufufua viwanda vya chuma, mbolea, saruji, na nguo ili kuongeza ajira kwa vijana na wananchi kwa ujumla. 

Pia, ameomba ujenzi wa chuo kikuu katika Jiji la Tanga na kupendekeza kiitwe Chuo Kikuu cha Shaaban Robert ili kuheshimu mchango wa mwanazuoni huyo.

Katika hitimisho lake, Ummy Mwalimu amemhakikishia Rais Samia kuwa wananchi wa Tanga Mjini wana imani naye na wako tayari kumpa kura zote mwezi Oktoba 2025 ili aendelee kuiongoza Tanzania na kuleta maendeleo zaidi.


















Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa Mkoani Tanga kuzungumza na wananchi wa Tanga Mjini kwenye viwanja vya Mkwakwani, amewataka Maafisa masuuli wanaosimamia miradi mbalimbali ya maendeleo Mkoani Tanga kufuatilia kwa karibu na kuhakikisha miradi yote ya maendeleo mkoani humo inakamilika kwa wakati.

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Ijumaa Februari 28, 2025 wakati akizungumzia changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa ziara yake ya siku tano kwenye Wilaya zote za Mkoa huo akisema ipo changamoto ya kusuasua kwa miradi ya maendeleo suala ambalo linachelewesha maendeleo kwa baadhi ya maeneo.

Rais Samia pia amesema amelichukua ombi la wananchi wa Tanga pamoja na viongozi wao mbalimbali kutaka chuo kikuu kujengwa Mkoani humo, akisema serikali tayari imeanza kulifanyia kazi suala hilo kwa kuanzisha kampasi ya Chuo kikuu cha Mzumbe kwenye Mji wa Mkinga na kumuagiza Waziri wa Elimu Prof. Adolf Mkenda kufanyia kazi ombi la ujenzi wa chuo kikuu mkoani humo.

Rais Samia ametumia Mkutano huo pia wakati huu Waumini wa dini ya Kiislamu wakisubiri mwandamo wa mwezi kuwatakia Funga njema na yenye kheri waislamu wote nchini sambamba na Kuwatakia waumini wa dini ya Kikristo kuwa na mfungo mwema wa kwaresma, wakati huu wakijiandaa na Mfungo huo kuelekea sikukuu za Pasaka kwa mwaka 2025.