📍Yazindua vituo vya kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme
📍Wananchi kunufaika na mpango wa ukopeshaji wa majiko ya umeme kupitia LUKU
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limezindua mradi wa vituo vya kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme pamoja na Mpango wa Ukopeshaji wa Majiko ya Umeme kwa Wateja (On-Bill Financing – OBF), hatua inayofungua ukurasa mpya wa matumizi ya umeme nchini na kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya nishati safi.
Akizindua miradi hiyo jijini Dodoma, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb) leo tarehe 11 Juni, 2026 alisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya Tanzania kushiriki kikamilifu katika mageuzi ya matumizi ya nishati safi duniani huku ikilenga kuboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi.
“Hatua hii inapanua matumizi ya umeme kutoka kupikia hadi usafiri, kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi, kupunguza gharama za maisha na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa,” alisema Mhe. Ndejembi.
Alisema Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati, hali iliyowezesha uzalishaji wa umeme nchini kufikia zaidi ya megawati 4,000 na kuweka msingi wa matumizi mapana ya umeme katika sekta mbalimbali za uchumi.
Katika kuimarisha matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme, TANESCO kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) imepokea mashine 50 za kisasa za kuchajia vyombo hivyo kutoka kampuni ya AUTEL ya China. Mashine hizo zitafungwa katika maeneo mbalimbali ya kimkakati nchini ili kurahisisha huduma za uchaji.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, alisema Shirika limejipanga kuongoza mageuzi ya matumizi ya umeme nchini kwa kutumia fursa ya upatikanaji wa umeme wa kutosha.
“Mtazamo wa awali kwamba umeme ni ghali na matumizi yake yanaishia kwenye mwanga pekee umebadilika kwa kiasi kikubwa. Leo, wananchi wengi wanatumia umeme katika kupikia na shughuli mbalimbali za kiuchumi, huku hatua ya kuzindua vituo vya kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme ikifungua ukurasa mpya wa matumizi ya nishati safi nchini,” alisema Bw. Twange.
Kwa upande wa nishati safi ya kupikia, TANESCO imeanza kutekeleza Mpango wa On-Bill Financing (OBF) utakaowezesha wateja kupata majiko ya umeme kwa mkopo na kufanya marejesho kupitia manunuzi yao ya kawaida ya umeme wa LUKU.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ameipongeza TANESCO kwa hatua hiyo na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini.
“Nawapongeza TANESCO kwa hatua hii ya kimkakati inayofungua fursa mpya za matumizi ya nishati safi nchini. Ni muhimu kuendelea kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi katika usafiri na kupikia ili kuharakisha maendeleo na kuhifadhi mazingira,” alisema Senyamule.
Uzinduzi wa miradi hiyo unaashiria hatua mpya ya kupanua matumizi ya umeme nchini kutoka matumizi ya kawaida ya majumbani hadi sekta za usafiri, kupikia na shughuli za uzalishaji mali, sambamba na juhudi za Taifa kuelekea uchumi wa kijani na maendeleo endelevu.

Post A Comment: