Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amesema dhana ya taka sifuri na urejeshaji bidhaa ni fursa muhimu ya kukuza sekta ya viwanda, kuongeza thamani ya malighafi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

Akizungumza katika kikao cha mawaziri kilichofanyika jijini Istanbul nchini Uturuki, Juni 5, 2026, kilichobeba mada ya Mageuzi ya Kijani ya Viwanda: Mtazamo wa taka sifuri na urejeshaji bidhaa, Kapinga amesema Tanzania inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha sekta ya viwanda huku ikisisitiza matumizi bora ya rasilimali na uhifadhi wa mazingira. Ameeleza kuwa dhana ya taka sifuri na urejeshaji bidhaa inatoa fursa kwa nchi zinazoendelea kupitia matumizi endelevu ya malighafi, kupunguza upotevu baada ya mavuno, kupunguza uzalishaji wa taka na kuongeza thamani ya bidhaa zinazotengenezwa viwandani. Kapinga amesema Serikali ya Tanzania imeendelea kuunganisha masuala ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika sera na mipango ya maendeleo ya viwanda kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi, ufanisi wa nishati na teknolojia rafiki kwa mazingira. Aidha, amesisitiza kuwa mafanikio ya mageuzi ya kijani yanategemea uwekezaji wa kutosha, upatikanaji wa teknolojia za kisasa pamoja na ushirikiano madhubuti kati ya serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo. Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa kuendeleza viwanda vinavyoongeza thamani ya rasilimali, kudhibiti taka na kuvutia uwekezaji huku akiwakaribisha wafanyabiashara kuwekeza nchini kwa lengo la kujenga uchumi imara na shindani.

Mkutano huo umeandaliwa na Serikali ya Uturuki kupitia taasisi ya Zero Waste Foundation inayosimamiwa na Mwenza wa Rais wa Uturuki Bibi Emine Erdoğan na umeleta pamoja washiriki zaidi ya 3,000 kutoka nchi zote duniani, pamoja na taasisi za kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia, Umoja wa Mataifa, Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kiarabu na Shirika la Maendeleo na Biashara la Umoja wa Mataifa (UNCTAD).

Share To:

Alex Sonna

Post A Comment: