Bodi ya Nishati Vijijini (REB) imeridhishwa na hatua, ubunifu na kasi ya mageuzi yanayotekelezwa na Gereza la Manyoni, mkoani Singida, katika kuachana na nishati isiyo safi na kuanza kutumia bidhaa na teknolojia za Nishati Safi ya Kupikia.
Hayo yalisemwa Julai 17, 2026 na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, alipotembelea gereza hilo akiwa ameambatana na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Thomas Mmbaga, kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mpango wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
"Tumejionea jinsi Gereza la Manyoni linavyoendelea kutekeleza maelekezo, na ni kweli wamehama kutoka kutumia kuni. Sasa wanatumia gesi ya LPG, kuni-poa zinazotokana na mabaki ya miwa, na Rafiki Briquettes zinazotokana na vumbi la makaa ya mawe kutoka STAMICO," amefafanua Balozi Kingu.
Amesema ziara hiyo imelenga kujionea jinsi REA ilivyowezesha Jeshi la Magereza kuachana na nishati isiyo safi ya kupikia na badala yake kuanza kutumia Nishati Safi ya Kupikia.
Aidha, amewapongeza viongozi wa gereza hilo kwa kufunga mtambo utakaotumika kuzalisha mkaa mbadala kutokana na maranda ya mbao na mabaki ya mazao mbalimbali, ikiwemo mahindi na mpunga.
Amesema hatua hiyo italiwezesha gereza hilo kuzalisha briquettes kwa matumizi yake na baadaye kwa ajili ya biashara.
"Tumeona wanakwenda vizuri. Hata jiko walilonalo ni la kisasa; linahitaji maboresho machache, lakini kwa ujumla wanatekeleza vizuri na wamejenga miundombinu kwa kiwango kizuri," amesema Balozi Kingu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Manyoni, Mrakibu Sikai Lucas, ameshukuru kwa ujio huo na kueleza kuwa walianza kutumia Nishati Safi ya Kupikia Desemba 2024, kufuatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Tulianza kutumia kuni-poa, baadaye Rafiki Briquettes, na sasa tunatumia gesi ya LPG kutoka REA, ambayo imeboresha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa nishati. Tunashukuru sana, na tumefarijika kupata ugeni huu kwani umetupa fursa ya kujifunza mambo mengi kuhusu Nishati Safi ya Kupikia," amesema Mrakibu Lucas.
Aidha, ameishukuru REA kwa kugawa mitungi ya gesi ya LPG kwa maafisa na askari wote wa Gereza la Manyoni, na kueleza kuwa gereza hilo litaanza rasmi uzalishaji wa briquettes Agosti 1, 2026.
Ameiomba REA kuendelea kushirikiana nao ili kutekeleza kikamilifu maelekezo ya Rais kuhusu matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.






Post A Comment: