Na Moreen Rojas,Dodoma.


Jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania(JWTZ) limetangaza siku 7 kwa wananchi wanaovaa sare za jeshi kusalimisha mavazi hayo kuanzia leo.


Hayo yameelezwa na Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda Kaimu Mkurugenzi wa habari na uhusiano makao makuu ya Jeshi(JWTZ) wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa idara ya habari maelezo jijini Dodoma.


Aidha ameongeza kuwa kwa muda sasa kumekuwa na wimbi kubwa la baadhi ya wananchi wanaokamatwa au kuonekana wakiwa wamevaa sare za jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania au mavazi yanayofanana na sare za kijeshi.


"Tumekutana hapa hii leo,ili kupitia kwenu JWTZ liweze kutoa ufafanuzi kwa jamii ya watanzania wananchi kuhusiana na kadhia hiyo inayokinzana na katazo la kisheria la raia kuvaa,kumiliki au kuuza mavazi ya kijeshi au yanayoelekea kufanana na sare za kijeshi" Amesema Luteni Kanali Ilonda


Aidha ameongeza kuwa Jeshi linakataza kuvaa mavazi hayo ambayo ni pamoja na Kombati(Vazi la mabaka mabaka),Makoti,Tisheti,Suruali,Magauni,Kofia,Viatu,Mabegi na Kaptula zenye rangi zinazofanana au kushonwa katika mitindo ya kijeshi,katazo hilo ni kwa mujibu wa kifungu cha sheria ya ulinzi wa Taifa(NDA)sura ya 192 sheria namba 24 ya mwaka 1966 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002,ambapo kifungu cha 178 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16(Penal code) na kifungu cha 6 cha sheria ya usalama wa Taifa,vinakataza raia kuvaa sare na mavazi ya majeshi ya ulinzi au yanayofanana nayo.Aidha amesema kuwa zipo baadhi ya taasisi zinazowashonea watumishi wake sare za aina hiyo,wapo pia wafanyakazi wanaoingiza nchini mavazi ya aina hiyo na kuyauza kwa baadhi ya raia kupitia maduka au maeneo yao ya biashara,aidha wapo baadhi ya wasanii wanaovaa mavazi hayo na kuyatumia wawapo kwenye majukwaa ya kazi zao bila kufuata utaratibu.


"Wapo baadhi ambao kwa kuyatumia mavazi hayo wamekuwa wakitapeliwa wananchi na wengine kufanya vitendo viovu ambao pia wamekuwa wakidhaniwa kuwa ni wanajeshi ambapo vitendo hivyo ni vya uvunjifu wa sheria za nchi,hivyo havipaswi kufumbiwa macho,hali hii ikiachwa kuendelea inaweza kuhatarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu hivyo baada ya siku saba atakayekutwa nayo atachukuliwa hatua" Amesisitiza Luteni Kanali Ilonda.


Sanjari na hayo amesema kuwa JWTZ linaomba kuwafahamisha wananchi kuwa utekelezaji wa majukumu yake ya msingi na mengineyo unategemea sana ushirikiano mzuri na wananchi wote,hivyo mahusiano na jeshi na wananchi ndio mhimili mkubwa ndani na nje ya nchi.


"Sio hekima kwetu kulumbana kwa namna yoyote ile na baadhi ya wananchi wenye mavazi yaliyokatazwa,ndio maana tunatoa siku saba kuyasalimisha bila kuchukuliwa hatua ili kuepuka usumbufu kwake ambaye hatayawasilisha atakuwa na nia ovu na dhamira mbaya,JWTZ itaendelea kudumisha ushirikiano na mshikamano na wananchi ili kuweza kutimiza jukumu lake kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania"


Mwisho amewaomba watanzania wote waendelee kuliunga mkono Jeshi lao la Ulinzi ambalo liko imara na tayari kuilinda nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kulitumikia kwa uaminifu mkubwa serikali yetu,Mungu atusaidie.


Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya habari maelezo Ndg.Gerson Msigwa amewasihi watanzania kuhakikisha wanafuata sheria na kusalimisha mavazi hayo ya jeshi kwa wahusika na kuongeza kuwa hata msaidia mtu yoyote atakayekiuka agizo hilo hivyo Jeshi limeshatangaza siku saba ni wajibu wa kila mwananchi kufuata sheria za nchi.Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: