Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla ameiagiza Wakala wa barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Arusha, Jeshi la Polisi pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kushughulikia kadhia ya foleni kwenye Jiji la Arusha kwa wakati ili kuondoa vikwazo katika shughuli za kila siku za kiuchumi na Kijamii ndani ya Jiji la Arusha.
Katika kutekeleza agizo hilo, leo Jumatano Januari 14, 2026, kimefanyika kikao kilichowahusisha Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa, TARURA, LATRA, TANROAD, Polisi na Idara ya Mipango Miji Jiji la Arusha, ambapo pamoja na mambo mengine wametangaza kufutwa kwa Vituo vya Mabasi katikati ya Jiji ambavyo vimekuwa vikitumika kushusha na kupakia abiria, wamiliki wa mabasi wakiagizwa kutumia Kituo Kikuu cha mabasi Arusha kwaajili ya abiria wao.
Kulingana na Mhandisi Julius Kaaya, Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Arusha akizungumza kwaniaba ya washiriki wa Kikao hicho, agizo hilo linaanza utekelezaji wake mara moja, wakitangaza kuchukua hatua kali za kisheria kwa kampuni ya mabasi itakayokaidi kutekeleza agizo hilo.
Kwa upande wake Afisa Mipango Miji Jiji la Arusha Bi. Doroth Absalom ameeleza kuwa kulingana na sheria, Kampuni za mabasi haziruhusiwi kutumia majengo ya makazi na biashara kama Vituo vyao vya mabasi, akisema ni sheria kwamba kila Basi kuanzia safari zake kwenye Kituo Kikuu cha mabasi Arusha, akionya pia kuhusu uoshaji holela wa mabasi pembezoni mwa barabara.






Post A Comment: