Na Joachim Nyambo,Mbeya.


TAASISI ya Afya ya Ifakara kupitia programu ya Nest 360 Tanzania imetoa msaada wa vifaa   vya kujifunzia masuala ya ukarabati wa vifaatiba kwaajili ya kulinda afya ya watoto wachanga vyenye thamani ya Shilingi milioni 70 kwa chuo kikuu cha Sanyansi na Teknolojia Mbeya(Must).


Kutolewa kwa vifaa hivyo kunalenga kuwezesha upatikanaji wa wataalamu wa matengenezo ya vifaa vinavyotumika kunusuru uhai wa watoto wanaozaliwa ili kuondokana na uhaba wa wataalamu hao uliopo hapa nchini.

Akikabidhi vifaa hivyo,Mratibu kiongozi wa mradi wa Nest 360 wa Taasisi ya Afya ya Ifakara,Donat Shamba alisema taasisi imelenga kutoa msaada wa aina hiyo kwenye vituo sita yaliyopangwa kikanda ambapo kwa kanda ya Nyanda za juu Kusini kituo kinachonufaika ni chuo cha Must kilichopo mkoani Mbeya.

Alivitaja vituo vingine kuwa ni Arusha,Dodoma,Mwanza kupitia hospitali ya Bugando na Dar es salaam kupitia Taasisi ya Teknolojia ya Dar es salaam(DIT) alivyosema vitatumika pia kufundishia wataalamu waliopo katika hospitali za mikoa na wilaya jirani.

Shamba alisema Taasisi hiyo ilichukua uamuzi wa kutoa msaada huo baada ya kubaini kuwepo kwa changamoto kubwa ya uhaba wa wataalamu wa vifaa vya kulinda maisha ya watoto wanaozaliwa hatua iliyosababisha vifaa vilivyoharibika kutokarabatiwa.

Alisema kutokana na kukosekana kwa wataalamu matukio ya vifo vya watoto wachanga yalionekana kuongezeka katika maeneo mengi hatua aliyosema hailingani na utaalamu uliopo hivi sasa unaoweza kuwaokoa kwa kiasi kikubwa watoto hao wachanga na kuwafanya waishi.

Kwa upande wake mhandisi wa vifaa tiba wa program ya Nest 360 Tanzania.Elizabeth Ngowi alivitaja vifaa vilivyotolewa kwa chuo hicho kuwa ni pamoja na mashine ya kutibu watoto wachanga waliozaliwa  na tatizo la manjano ya ngozi na mashine ya joto kwa watoto wachanga.

Nyingine ni mashine ya kusaidia kufungua mapafu ya mtoto mchanga ili aweze kupumua vizuri,mashine ya oksijeni inayomwezesha mgonjwa kupata  hewa ya kutosha,mashine ya kutoa vitu visivyotakiwa katika mwili wa mtoto anapozaliwa na mashine ya kuangalia kiwango cha oksijeni kinachoingia mwilini iwapo kinatosha.

Zipo pia mashine ya kuangalia kiwango cha sukari cha sukari katika mwili wa mtoto na pia zana kutengenezea mashine hizo ambapo vifaa vyote hivyo vitatumika katika kuwafundishia wanafunzi waliopo chuoni hapo wanaosoma masomo yanayohusiana na utaalamu wa vifaa tiba.

Ngowi pia lishauri zana hizo zitumike pia kuwafundishia wataalamu waliopo tayari kazini kupitia program mbalimbali zinazoweza kuandaliwa ili kupunguza kwa haraka changamoto ya wataalamu wa vitendea kazi hivyo alivyosema ni muhimu katika kuokoa maisha ya watoto.

Akipokea vifaa hivyo naibu Makamu mkuu wa Chuo cha Must,Profesa Godliving Mtui alisema msaada huo utakuwa chachu ya kuzalisha wa wingi wataalamu watakaokwenda kusaidia maisha ya watoto wachanga na kuwaepusha na vifo vinavyoweza kuzuilika.

Profesa Mtui pia alisisitiza umuhimu wa wadau wa sekta ya afya kutambua umuhimu wa wataalamu wa matengenezo ya vifaa tiba na kuandaa utaratibu wa utoaji ajira akisema tayari chuo hicho kimeanza kuzalisha wataalamu lakini wanapohitimu upatakanaji wa ajira zao bado ni mgumu.

Alisema hali hiyo inatokana na wadau wengi kutotambua uwepo wa wataalamu hao na hivyo kubaki wakikabiliwa na changamoto ya kushindwa kutoa huduma kutokana na kuwa na vitendea kazi vibovu na kubaki wakisubiri wataalamu watoke nje ya nchi kuja kuwasaidia.


 


M

Share To:

Post A Comment: