MKUU wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mkinga wakati wa ziara yake aliyoambatana na kujitambulisha kwao  ikiwa ni mara ya kwanza kutembelea wilaya hiyo tangu ateuliwe kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga.

MKUU wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba katika akiwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga (RAS) Pili Mnyemaa kulia ni Mkuu wa wilaya ya Mkinga Kanali Maulid Surumbu wakifuatilia jambo kwa umakini



Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa huo kutotegemea mradi wa uuzaji viwanja kama chanzo cha mapato badala yake waangalie biashara nyingine za kuwekeza.

Aidha, amewataka kuwa na utaratibu wa kuwekeza kwenye miradi ya kiuchumi badala ya kupeleka fedha zote kwenye miradi ya huduma za jamii. 

Mgumba amesema hayo leo Jumatano Agosti 10,  wilayani Mkinga alipokuwa akizungumza na Mkuu wa Wilaya na watendaji wa wilaya hiyo alipokwenda kujitambulisha ikiwa ni mara ya kwanza kutembelea wilaya hiyo tangu ateuliwe kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga.

Akizungumzia suala la viwanja, Mgumba aliwataka wakurugenzi hao kuwa waangalifu katika upimaji wa viwanja kutopima ardhi yenye rutuba kwa mustakabali wa usalama wa chakula.

Pamoja na mambo mengine, Mgumba amepokea taarifa ya mapato na matumizi ya wilaya hiyo na miradi mbalimbali ikiwamo kuanzisha shamba la miche ya mkonge, soko la samaki, eneo la maegesho na mengineyo.

“Mradi wa kuuza viwanja naomba mtoe kwenye orodha ya miradi yenu kwa sababu ni ya muda tu si endelevu na pia muwe makini msipime ardhi yenye rutuba halafu kesho tukikosa chakula tumlaumu Mungu.

“Kama tunataka usalama wa chakula kwa kizazi hiki na kijacho lazima tulinde ardhi yetu. Leo tunataka kuzalisha mkonge tani 300,000 lakini hatuwezi kwa sababu maeneo yaliyokuwa mashamba ndiyo yamekuwa makazi,” amesema Mgumba.

Kuhusu miradi ya kuwekeza ikiwamo masoko, alisema haimaanishi wilaya isifanye huduma za kijamii bali waangalie ni namna gani wanaweza kuwekeza na kuendelea kujiingizia mapato ya ndani.

Katika hatua nyingine, Mgumba amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, kutenga maeneo ya ibada (kanisa na msikiti) katika maeneo ya biashara, viwanja vya wazi na viwanja vya michezo wakati wa upimaji viwanja.

Amesema viwanja vya wazi lazima viwepo pia halmashauri isiangalie tu viwanja ilimradi iongeze mapato kwamba kuacha aneo la wazi ni kama unapoteza mapato.

“Kwa hiyo maeneo ya wazi yawepo na maeneo ya ibada yawepo, huwezi kujenga soko kisha usitenge kiwanja cha msikiti au kanisa utaonekana mtu wa mpango miji ambaye haelewi. Yaani mtu atoke pale kwenye biashara yake halafu kanisani au msikitini aende zaidi ya Km 30.

“Kwa hiyo katika mipango yenu mnapopanga miji hizo nyumba za ibada nazo ziwepo ili watu wanapofanya biashara pale tusiwaweke mbali na Mwenyezi Mungu,” alisema Mgumba.

Awali akitoa taarifa ya mikakati ya wilaya hiyo kuongeza mapato ya ndani, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Kanali Maulid Surumbu alisema ili kuboresha mapato yake ya  ndani wamejiweka mikakati ya kujenga soko la samaki katika kijiji cha Jasini, ukamilishaji wa soko la mazao Maramba na machinjio ya kisasa Kasera.

“Aidha, tumeandaa michoro ya mipango miji na upimaji wa viwanja katika Mji wa Horohoro, Kasera na ukanda wa bahari (Beach Plots) ambapo Kampuni ya World Map imeandaa michoro ya mipango miji na upimaji wa viwanja takribani 4,583 vya makazi, biashara na viwanda katika Rasi ya Manza (Manzabay).

“Mikakati mingine ni kujenga maegesho ya magari katika eneo la Horohoro mpakani, stendi ya mabasi na maeneo ya huduma za kijamii, kuanzisha shamba la miche ya mkonge lakini pia tayari tumenzisha mnada katika kijiji cha Sokonoi,” alisema.

Aidha, Kanali surumbu alisema tayari uboreshaji wa stendi ya Manza kama stendi ya Wilaya umeshaanza sanjari na ujenzi wa soko la kisasa la mazao Horohoro mpakani (Mradi Mkakati).
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: