Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amezipa siku 20 Viwanda vya saruji vya Tanga Cement na Twiga Cement kukutana na wanachama wa ushirika wa wachimbaji wa madini ya jasi (gypsum) kutoka Kijiji cha Makanya, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, ili kufikia muafaka wa utaratibu wa biashara ya malighafi inayotumika viwandani humo.

Akizungumza Januari 28, 2026 wakati wa kikao cha pamoja kati ya wawekezaji hao na Serikali kupitia Wizara ya Madini, Dkt. Kiruswa alisema Serikali inalenga kuona biashara ya madini ya jasi inanufaisha pande zote, kuhakikisha viwanda vinapata malighafi kwa uendelevu huku wachimbaji na jamii zinazozunguka migodi zikinufaika kiuchumi na kimazingira. 

Alisisitiza kuwa anatoa siku 20, kufikia tarehe 20 Februari 2026, uongozi wa Kampuni inayomiliki viwanda hivyo na ushirika wa wachimbaji hao kukaa pamoja na kukubaliana namna bora ya uratibu wa biashara hiyo bila kuathiri upande wowote na kwamba kikao hicho kihusishe uongozi wa kijiji hicho na vyama vya wachimbaji ili kuweka misingi ya uwazi, haki, uhusiano na uendelevu.

Katika kuhakikisha shughuli za uchimbaji na usafirishaji wa jasi zinafanyika kwa kuzingatia Sheria na maslahi ya jamii, Naibu Waziri alielekeza kampuni hiyo kutekeleza hatua zafuatazo ambazo ni Utunzaji wa Mazingira: Kupitia upya mikataba yote waliyoingia na wachimbaji, na kuhakikisha utunzaji wa mazingira unazingatiwa ipasavyo wakati wa uchimbaji wa madini ya jasi sambamba na kufukia mashimo yaliyoachwa wazi.

Hatua nyingine ni barabara inazoelekea maeneo ya uchimbaji ambayo kwa sasa ni mbovu inapaswa ifanyiwe ukarabati wa haraka ili kurahisisha usafirishaji na kupunguza athari kwa jamii ikiwemo vumbi kali pamoja  kuagiza mizigo ya madini ya jasi kununuliwa kwa watu wanaotambulika na kuthibitishwa na uongozi wa kijiji husika, ili kudhibiti migogoro na kuongeza uwajibikaji.

Pia, Dkt. Kiruswa alielekeza viwanda hivyo kutekeleza kikamilifu Miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa kuwa vinachukua malighafi kutoka katika kijiji hicho na kwamba wanapaswa kuchangia huduma za jamii kama elimu, afya na maji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ununuzi (Procurement Director) wa Kanda ya Afrika Mashariki anaesimamia Tanzania, DRC, Msumbiji na Afrika Kusini chini ya Heidelberg Materials, ambao ni wamiliki wa viwanda hivyo Ahmed Ali, alisema kuwa uongozi wa viwanda hivyo utaitisha kikao cha pamoja na wachimbaji hao wa jasi sambamba na wadau muhimu kwa ajili ya kushughulikia suala hilo na kwamba Kampuni italeta mrejesho Serikalini kama ilivyoelekezwa kufanyika ndani ya siku 20.

Share To:

Post A Comment: