Articles by "MADINI"
Showing posts with label MADINI. Show all posts

 


▪️Tanzania yajipanga kuwa kitovu cha huduma bora za Maabara ya madini kusini mwa Jangwa la Sahara


■ Waziri Mavunde amshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia kwa uamuzi wa ujenzi wa maabara


■ Amtaka Mkandarasi kukamilisha ujenzi kwa wakati


■ Ujenzi wa Maabara kugharimu zaidi ya Bilioni 14.3


Kufuatia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa maabara ya kisasa ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), hatua hiyo inakwenda kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utoaji wa huduma za maabara ya madini kusini mwa Jangwa la Sahara.

Hayo yamesemwa leo tarehe 15 Julai, 2026 na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa maabara ya GST uliopo Kizota, Jijini Dodoma.

"Tunamshukuru Rais wetu Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huu wa kisasa, unaokwenda kuifanya Nchi yetu kuwa kinara na mahiri katika utoaji wa huduma za maabara za madini", amesema.

"Mradi huu pia unakwenda kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utoaji wa huduma za maabara kwa Nchi za Afrika ya Mashariki na Kati, kutokana na ubora wa huduma hizo kuwa za kimataifa" ameeleza Waziri Mavunde.

Aidha, Waziri Mavunde alibainisha kuwa kwa muda mrefu wachimbaji wadogo wamekuwa wakipata changamoto ya upimaji wa sampuli zao kwenye maabara, hali iliyopelekea kushindwa kufanya shughuli zao kiufanisi.

Mavunde amesitiza kuwa ujio wa maabara hiyo ya kisasa unakwenda kuwa mwarobaini wa changamoto za wachimbaji ikiwa ni pamoja na kuhudumia wachimbaji wengi zaidi kwa ubora wa kimataifa.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Madini Tanzania, Mhandisi Ally Samaje ameeleza kuwa ujenzi wa mradi huo wa maabara unagharimu shilingi bilioni 14.3 na upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ambapo unataraji kukamilika ifikapo Mwezi Septemba, 2027. 

Aidha, ameongeza kuwa maabara hiyo ikikamilika itakuwa ni ya kisasa na inakwenda kuhudumia wateja wengi wa ndani na nje ya Nchi.










 



 Asilimia 10 ya mapato ya sekta ya madini kuelekezwa kwenye utafiti

MBT kuwanufaisha wachimbaji Mundarara


Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amesimamisha kwa muda uchaguzi wa Viongozi wa Mabroka wa Madini katika Wilaya ya Longido, Mkoa wa Arusha, akisisitiza kuwa uchaguzi huo hautafanyika hadi pale wapiga kura watakapopatiwa elimu ya kutosha kuhusu haki, wajibu na taratibu za uchaguzi kwa mujibu wa  Katiba ya Mabroka.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, haki na ushirikishwaji wa wadau wote, huku ukiepusha migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na kutokuelewa taratibu za uchaguzi.

Akizungumza leo Juni 10, 2026 na wachimbaji, wafanyabiashara wa madini na viongozi wa Serikali wakati wa ziara yake wilayani humo, Dkt. Kiruswa amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejidhatiti kujenga sekta ya madini yenye uwazi, uwajibikaji na ushiriki mpana wa Watanzania katika shughuli zote za mnyororo wa thamani wa madini.

"Nataka uchaguzi huu ufanyike kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zote. Kwanza tutoe elimu kwa wapiga kura ili kila mshiriki ajue haki na wajibu wake. Tukifanya hivyo tutapata viongozi wenye uhalali, wanaokubalika na watakaoweza kuwatumikia wadau wa sekta ya madini kwa ufanisi," amesema Dkt. Kiruswa.

Ameelekeza Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (CHAMMATA), Jeremiah Kituyo, kwa kushirikiana na viongozi wa kitaifa wa chama hicho, kuhakikisha elimu hiyo inatolewa kwa wakati na uchaguzi mpya unaratibiwa mara baada ya zoezi hilo kukamilika bila kucheleweshwa.

Naibu Waziri huyo amewakumbusha mabroka wote wa madini kuzingatia matakwa ya Sheria ya Madini kwa kuhakikisha wanakuwa na leseni halali za ubroka pamoja na vitambulisho vinavyoonesha namba za leseni zao wakati wote wanapotekeleza shughuli zao.

Amesema Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayejihusisha na ubroka wa madini bila leseni halali, akibainisha kuwa hatua hiyo inalenga kulinda maslahi ya wafanyabiashara, kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha Serikali inakusanya mapato yote yanayostahili.

Aidha, amewataka viongozi wa vijiji, viongozi wa sekta ya madini na wananchi kushirikiana kwa karibu katika kulinda rasilimali za madini na kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa mujibu wa sheria na zinawanufaisha wananchi wa maeneo husika.

Katika kuimarisha sekta ya madini, Dkt. Kiruswa amesema Serikali imeanza kutekeleza maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kurejesha sehemu ya mapato yanayotokana na sekta ya madini katika maendeleo ya sekta hiyo, ambapo asilimia 10 ya makusanyo ya sekta itaelekezwa kwenye shughuli za utafiti wa madini.

Amesema hatua hiyo itaiwezesha Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kufanya tafiti zaidi za kijiolojia, kuongeza upatikanaji wa taarifa za kisayansi kuhusu maeneo yenye madini na kuwasaidia wachimbaji wadogo kufanya uwekezaji wenye tija.

"Utafiti ni msingi wa mafanikio ya sekta ya madini. Tunataka wachimbaji wetu waondokane na uchimbaji wa kubahatisha na badala yake watumie taarifa sahihi za kijiolojia zitakazoongeza uzalishaji, kupunguza hasara na kuongeza kipato chao," amesema.

Ameongeza kuwa uwekezaji katika tafiti za madini utaongeza ugunduzi wa maeneo mapya yenye rasilimali, kuchochea uwekezaji, kuongeza ajira na kuimarisha mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa.

Dkt. Kiruswa amesema Serikali kupitia Wizara ya Madini inatekeleza Programu ya Mining For A Brighter Tomorrow (MBT), inayowalenga wachimbaji wadogo, wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum ili washiriki kikamilifu katika shughuli za utafiti, uchimbaji, uchakataji, uongezaji thamani na biashara ya madini.

Kutokana na fursa hizo, amewahamasisha wananchi wa Kijiji cha Mundarara kuunda vikundi na kujiandikisha katika programu hiyo ili kunufaika na mafunzo, teknolojia, mitaji na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kukuza shughuli za madini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (CHAMMATA), Jeremiah Kituyo, amesema uchaguzi wa mabroka katika ngazi ya wilaya utasimamiwa na viongozi wa mkoa kwa mujibu wa Katiba na mwongozo wa chama.

Amesema mwanachama atakayeshiriki uchaguzi atalazimika kuwa na kitambulisho hai cha chama pamoja na leseni halali ya biashara ya madini, huku akibainisha kuwa viongozi wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi huchaguliwa kila mwaka ili kuimarisha uwajibikaji, uwazi na uwakilishi wa wadau wa sekta hiyo.

Kituyo amesema chama kitaendelea kushirikiana na Wizara ya Madini kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani, uwazi na kuzingatia sheria, hatua itakayochangia kuimarisha mazingira ya biashara ya madini nchini.














 


● Yaligunduliwa kwa mara ya kwanza duniani mwaka 1959 katika Wilaya ya Kongwa, Mkoa wa Dodoma.

● Yana thamani kubwa katika elimu, utafiti wa kisayansi na utalii wa jiolojia.

● Ni sehemu ya urithi wa asili wa Tanzania.


Imeelezwa kuwa kuna umuhimu wa kuchukua hatua madhubuti za kuhifadhi na kulinda madini adimu aina ya Yoderite yanayopatikana katika eneo la Mlima wa Mautia, Wilaya ya Kongwa, Mkoa wa Dodoma, ili kuhakikisha urithi huo wa kipekee wa kijiolojia unabaki salama kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Hayo yalisemwa Juni 30, 2026 na Meneja wa Jiolojia kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Solomon Maswi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea eneo hilo kwa ziara maalumu.

Maswi alisema kuwa uhifadhi wa Yoderite unaweza kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha kimataifa cha tafiti kuhusu madini adimu, sambamba na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea maeneo yenye urithi wa jiolojia.

Aliongeza kuwa Yoderite ni miongoni mwa madini adimu yanayoifanya Tanzania kutambulika duniani kutokana na historia yake ya kugunduliwa kwa mara ya kwanza katika Mlima wa Mautia.

Aidha, alifafanua kuwa madini hayo yana mchango mkubwa katika tafiti za kisayansi kwa kusaidia kuelewa mchakato wa uundaji wa miamba na mazingira yenye shinikizo na joto la juu ndani ya ganda la dunia. Pia yana umuhimu mkubwa katika elimu ya jiolojia, maendeleo ya utalii wa jiolojia na uhifadhi wa urithi wa asili duniani.

Maswi alibainisha kuwa, kutokana na uchache wake na kupatikana katika maeneo machache sana duniani, madini ya Yoderite hayachimbwi kwa matumizi ya viwandani wala biashara. Badala yake, yanahifadhiwa kama urithi wa kipekee wa kijiolojia unaovutia watafiti, wanafunzi, wataalamu wa sayansi na watalii kutoka ndani na nje ya nchi. Hali hiyo inaipa Tanzania fursa ya kujijengea hadhi kama kitovu cha tafiti za kimataifa na utalii wa jiolojia unaotegemea urithi wa asili.

Taasisi za utafiti wa madini na vyuo vya Madini vimeshauriwa kutumia eneo hilo kwa mafunzo endelevu ya utafiti wa madini.

Madini ya Yoderite yaligunduliwa kwa mara ya kwanza duniani mwaka 1959 katika Milima ya Mautia, Wilaya ya Kongwa, Mkoa wa Dodoma.

Kutokana na kuendelea kwa tafiti baada ya miaka 35 watafiti wa miamba na madini walifanikiwa kugundua aina hiyo ya madini nchini Zimbambwe.

Jina la Yoderite lilipewa kwa heshima ya mwanajiolojia mashuhuri wa Marekani, Hatten Yoder Jr., kutokana na mchango wake mkubwa katika tafiti za miamba na madini.







 


Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde leo Juni 30, 2026 amekutana na Mkurugenzi Mkuu na Mmiliki wa Kiwanda cha Kuzalisha Goroli za Chuma “Steel balls” Bw. Hou Songcun kujadiliana juu ya uwekezaji wa Kampuni hiyo nchini ili kuzalisha bidhaa za migodini.

Waziri Mavunde amewakaribisha wawekezaji wao kwenye eneo lililotengwa na serikali la Buzwagi Special Economic Zone lililopo wilayani Kahama,Shinyanga kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kuzalisha bidhaa za migodini ili kuwahudumia wachimbaji wakubwa na wadogo nchini.

Waziri Mavunde amesema serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu imejipanga kuhakikisha inavutia uwekezaji mkubwa kwenye uzalishaji wa bidhaa za migodini ili Tanzania kuwa kitovu za usambazaji wa bidhaa hiyo barani Afrika.

“Lengo letu ni kuona wachimbaji wakubwa na wadogo hapa nchini wanapata bidhaa nyingi za kuzalisha madini pasipo kutegemea uagizwaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi," amesema Mavunde.

Naye, Mmiliki na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oriental Casting and Forging Ltd Bw. Hou Songcun amesema Kampuni yake ipo tayari kufanya uwekezaji mkubwa wa bidhaa za migodini nchini kwa kuwa Tanzania ni nchi ambayo ina mazingira mazuri ya uwekezaji na kwamba sekta ya madini inakua kwa kasi kubwa sana hivyo ni sehemu salama na rafiki ya kufanya uwekezaji ambao utakuwa suluhisho la upatikanaji wa bidhaa za migodini kwa urahisi zaidi.









 


✅️ Sawa na Asilimia 105.8, Zikiwa Zimebaki siku 26 Kufunga Mwaka wa Fedha 2025/26

✅️ Watumishi Watakiwa Kuongeza Weledi Kufikia Sh Trilioni 1.4 Mwaka 2026/27

✅️ Watumishi  Watakiwa kuhudumia wananchi bila ubaguzi

WIZARA ya Madini imevuka lengo la ukusanyaji wa Maduhuli ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 baada ya kukusanya Sh trilioni 1.27 hadi Juni 5, 2026, dhidi ya lengo la Sh trilioni 1.2, huku ikitarajia kufikia Sh trilioni 1.3 ifikapo  Juni 30, 2026.

Kutokana na mafanikio hayo, watumishi wa Wizara hiyo na taasisi zake wametakiwa kuondokana na uzembe, kuongeza bidii na kufanya kazi kwa weledi ili kufikia lengo jipya la ukusanyaji wa Sh trilioni 1.4 lililowekwa kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Akizungumza katika kikao cha watumishi wote wa Wizara ya Madini na taasisi zake ambazo ni GST, TEITI, Tume ya Madini, STAMICO na TGC, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Eng. Yahya Samamba, amesema mafanikio yaliyopatikana yanapaswa kuwa chachu ya kuongeza juhudi katika usimamizi wa Sekta ya Madini kwa kuzingatia Sera, miongozo, kanuni na Sheria zilizowekwa.

Amesema watumishi wanapaswa kutambua kuwa wanapowahudumia wananchi wanatekeleza wajibu wenye thamani kubwa kwa taifa, hivyo wanapaswa kuwahudumia watu wote kwa usawa bila kujali itikadi, dini wala uraia wao.

“Wachache tuliokabidhiwa jukumu la kuhudumia sekta ya madini tunapaswa kuhakikisha watu wote wanahudumiwa kwa haki na uzalendo mkubwa ili kuendelea kujenga taifa letu,” amesema.

Amesema watumishi ndiyo injini ya Serikali katika sekta ya madini na kwamba mchango wao una nafasi muhimu katika kukuza uchumi wa nchi kupitia usimamizi bora wa rasilimali madini.

“Wito wangu ni kufanya kazi kwa bidii, weledi na kusimamia sera, miongozo, kanuni na sheria zilizowekwa ili sekta hii iendelee kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa,” amesema.

Katibu Mkuu huyo amesema watumishi wanapaswa kujiepusha na vitendo vya rushwa, uvivu na uzembe ambavyo vinaweza kuharibu imani ya wananchi kwa wizara, taasisi zake na Serikali kwa ujumla.

“Tusiharibu imani ya wananchi kwa rushwa, uvivu na uzembe. Mtu mmoja anayepokea rushwa anaweza kuchafua kazi za watumishi wengi waadilifu. Tufanye kazi kwa uzalendo mkubwa ili kuhakikisha hakuna mtu au wachache miongoni mwetu wanaochafua taswira ya wizara, taasisi zetu na Serikali kwa ujumla,” amesema.

Amesema watumishi wanapaswa kuchagua kuwa mwangaza badala ya kuwa kivuli na kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya wizara na taasisi zake kwa kuwa wote ni timu moja yenye malengo yanayofanana.

“Kazi ya mwenzako ikichelewa, mafanikio yako pia yanachelewa. GST ikichelewa kutekeleza majukumu yake, Tume ya Madini nayo itaathirika. Tusaidiane kwa pamoja kufikia malengo yetu,” amesema.

Katika salamu za Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, watumishi wamepongezwa kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Aidha, imeelezwa kuwa kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imepangiwa kukusanya Sh trilioni 1.4, lengo ambalo linahitaji watumishi kuongeza uwajibikaji, uadilifu na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.

 



Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde ameielekeza Timu ya Majadiliano ya Serikali kwenye Sekta ya Madini (GNT) kuwaita na kufanya nao majadiliano wamiliki wote wa leseni za uchimbaji madini kinywe nchini Tanzania kujadiliana kuhusu ubia wa serikali katika Kampuni hizo na kuwataka kuanza utekelezaji wa uchimbaji kwa mujibu wa masharti ya leseni na Sheria ya Madini Sura ya 123.

Ameyasema hayo leo tarehe 30 Mei, 2026 Wilayani Ruangwa aliposhiriki zoezi la utiaji saini na Kampuni za Grafica Resources na Eminent Minerals Limited zenye ubia wa uwekezaji wa hisa asilimia 83 na Serikali asilimia 17 kwa kila kampuni. 

"Sisi sekta ya madini tunamshukuru kwa dhati Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyotupa maelekezo na kutuwezesha kusimamia sekta kikamilifu kwa maendeleo ya Taifa letu"

"Na ndiyo maana Kampuni zote ambazo hazijaanza uzalishaji kwa mujibu wa masharti ya leseni zao tumeziandikia hati ya makosa (Default Notice) kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura ya 123. Kusaini kwetu mikataba siku ya leo, hakutoi unafuu kwa wawekezaji hawa kutotekeleza uwekezaji wao kwa mujibu wa Sheria yetu ya madini" amesisitiza Mhe. Mavunde.

Waziri Mavunde amesema hatua ya Timu ya GNT kuwaita na kuwataka wamiliki wa leseni za uchimbaji madini kinywe kufuata masharti ya Sheria na kuanza uzalishaji kutapelekea ufikiaji wa lengo la kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji wa kwanza duniani wa madini kinywe ifikapo mwaka 2030.

Vilevile, Waziri Mavunde ametoa wito kwa wawekezaji wa miradi hiyo kutoa fursa ya kipaumbele cha ajira kwa watanzania hususan wanaozunguka miradi hiyo. Kwa kufanya hivyo kutachochea uchumi wa Vijiji, Wilaya ya Ruangwa hususan kupitia wajibu wa uwekezaji kwa jamii (CSR) na kupelekea maendeleo ya uchumi wa Nchi yetu.

Aidha, Waziri Mavunde amebainisha kuwa miradi hiyo itakapoanza kuzalisha kikamilifu, itakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 101,048 za kinywe kila mwaka kwa upande wa mradi wa Grafica na tani 15,930 za kinywe kila mwaka kwa upande wa mradi wa Eminent mtawalia, hali inayoifanya Ruangwa sasa kuwa sehemu ya mnyororo wa thamani wa teknolojia za kisasa duniani.

Waziri Mavunde pia ameeleza kuwa bado Tanzania ina nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika uzalishaji wa madini mbalimbali duniani, na ndiyo maana tunaendelea kuweka mkazo kwenye ufanyaji wa utafiti wa kina ili kubaini mashapo zaidi yatakayoongeza uchimbaji hususan kupitia wachimbaji wadogo wenye mchango mkubwa katika uchumi wetu.

Awali, akieleza mchakato wa kufikia makubaliano hayo, Mwenyekiti wa Timu ya Majadiliano ya Serikali kwenye sekta ya Madini, Prof. Sifuni Mchome amebainisha kuwa, majadiliano hayo yalifanyika kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi yetu na hayakuwa na lengo la kutafuta mshindi, hali iliyopelekea Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata hisa zisizofifishwa za asilimia 17 kwenye kila mradi wa ubia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Grafica Resources, Bw. Vikas Bardiya ameeleza kuwa kampuni yao inaishukuru Serikali kwa ushirikiano iliyowapa mpaka kufikia makubaliano ya kuwekeza na kuahidi kwamba watahakikisha wanatekeleza uwekezaji huo kwa mujibu wa mkataba ili uweze kuleta manufaa kwa wananchi wa Ruangwa na Taifa kwa ujumla.

Pia, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Eminent Minerals Limited, Bw. Shafiqali Khaki ameeleza kufarijika kwao kuwa kampuni ya kizawa kuingia ubia na Serikali katika uwekezaji kwenye mradi huo wa uchimbaji madini kinywe na kwamba wao kama wazawa watahakikisha sehemu kubwa ya zaidi ya ajira 250 zitakazozalishwa katika uwekezaji huo zinachukuliwa na watanzania ili kuinua uchumi wa Taifa letu. 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mheshimiwa Zainab Telack alimshukuru Mhe. Rais kwa kuwa kiongozi mahiri katika kusimamia uchumi na kuhakikisha rasilimali zetu zinanufaisha watanzania.

 Aidha, alisisitiza kuwa Serikali ya Mkoa wa Lindi itaendelea kuwapa ushirikiano wawekezaji hao ili waweze kuendesha shughuli zao kwa kasi na kunufaisha wananchi wa Lindi na Taifa kwa ujumla.

 


Na Mwandishi Wetu Ruangwa, Lindi


Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kwamba Tanzania inajipanga kuwa mmoja ya wazalishaji wakubwa Duniani wa madini kinywe(𝙂𝙧𝙖π™₯π™π™žπ™©π™š) kupitia Kampuni 30 zinazomiliki Leseni za kati na kubwa za uchimbaji wa madini hayo na hivyo kutoa ushindani wa kiuzalishaji kwa nchi ya China ambayo ndio inaongoza kwa uzalishaji wa madini hayo duniani kwa kuzalisha tani milioni 1.2 kwa mwaka.

Mhe Mavunde ameyasema hayo leo Mei 28, 2026 Wilayani Ruangwa, Lindi aliposhiriki katika hafla ya utiaji saini wa mikataba wa ubia baina ya Serikali na Kampuni ya Lindi Jumbo Limited kwa ajili ya mradi mkubwa wa uchimbaji madini kinywe na kubainisha kuwa kuanza kwa uchimbaji mkubwa wa madini mkakati ya kinywe (graphite) kunaiweka Tanzania kwenye dira ya duniani kama Nchi ya kimkakati katika uzalishaji wa madini hayo muhimu kwenye utengenezaji wa betri za magari ya umeme.

"Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuijenga na kuifanya nchi yetu ya Tanzania kama Taifa lenye dira wazi ya kiuchumi, mazingira rafiki ya uwekezaji na usimamizi imara wa rasilimali zake," amesema Waziri Mavunde

Amesema tukio la leo ni matokeo ya dira na maono hayo thabiti ya Mhe Rais ambayo yameendelea kuifanya Tanzania kuwa sehemu salama ya wawekezaji ambayo ina sera na Sheria zinazoeleweka na kutabirika.

Pia, Mhe.Mavunde amefafanua kwamba kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya sita Duniani kwa uzalishaji wa madini kinywe ambapo kwa mwaka uzalishaji wa Tanzania ni tani 25,000 kwa kampuni mbili tu zilizoanza uzalishaji mkubwa za Lindi Jumbo na God Mwanga-Tanga huku zingine 28 zikiwa katika hatua mbalimbali za kuanza uzalishaji.

Mhe Mavunde amewataka wamiliki wa Leseni 28 za uchimbaji madini kinywe kuhakikisha wanaanza uzalishaji mapema kama sheria inavyoelekeza ili kuepuka kufutuwa leseni hizo.

Aidha, Waziri Mavunde alibainisha kuwa dunia kwa sasa inapita kwenye mageuzi makubwa ambapo madini kinywe ni msingi wa kesho kwani upatikanaji wake ni kichocheo kikubwa katika uzalishaji wa nishati safi kwa kusaidia utengenezaji betri za magari ya umeme.

Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni 82 unataraji kuzalisha madini kinywe tani 40,000 kwa mwaka katika kipindi cha uhai miaka 24 ya mgodi ambapo zaidi ya ajira 300 zimezalishwa hadi sasa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Timu ya Majadiliano ya Serikali kwenye sekta ya madini, Prof. Sifuni Mchome ameeleza kuwa miongoni mwa faida ambazo Serikali itapata kupitia kusaini mikataba hiyo ya ubia ni pamoja na udhibiti wa fedha na uhakika wa mapato kutokana na uwekezaji huo na fursa za ajira kwa watanzania.

Prof. Mchome amebainisha kuwa kupitia
makubaliano hayo yaliyotiwa saini, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itamiliki asilimia 16 ya hisa huru zisizohafifishwa thamani (non-dilutable free carried interest shares), huku Kampuni ya Lindi Jumbo Limited ikimiliki asilimia 84 ya hisa katika kampuni ya ubia.

Awali, akieleza maendeleo ya mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Lindi Jumbo Limited, Bw. Andrew Cunningham amebainisha kuwa pamoja na upanuzi wa uzalishaji wa mgodi huo, wataendelea kufanya utafiti ili kubaini mashapo zaidi ambayo yatarefusha maisha ya mgodi na kuongeza manufaa zaidi kwenye uchumi wa Tanzania.

Naye mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuvutia wawekezaji ambayo wamekuwa ni chachu ya maendeleo ya Mkoa wa Lindi na kuahidi kwamba Serikali ya Mkoa wa Lindi itaendelea kuwapa ushirikiano wawekezaji wote ili wafikie malengo yao na kuchochea uchumi wa Nchi yetu.