Articles by "MAVUNDE"
Showing posts with label MAVUNDE. Show all posts

 


Serikali imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania kupitia uongezaji thamani ndani ya nchi ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchumi wa kijani (green economy)  hususan katika utengenezaji wa magari ya umeme, betri za magari, nishati safi na vifaa vya kielektroniki.

Hayo yamewekwa wazi leo Agosti 26, 2025 na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony  Mavunde, wakati akiweka jiwe la msingi la Kiwanda cha kusafisha na kusindika Madini ya Nikeli na Shaba kinachojengwa na Kampuni ya Zhongzhou Mining Co. Ltd, eneo la Zamahero, Wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma.

Amesema kuwa, Mradi huo utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba madini yanayochimbwa hapa nchini yaongezewe thamani ndani ya nchi na kuuza bidhaa ya mwishyabadala ya madini ghafi.

“Ujenzi wa kiwanda hiki ni uthibitisho kuwa dhamira ya kuongeza thamani madini nchini, tunataka kuona Tanzania ikibadilika na kuwa taifa linalozalisha bidhaa zenye thamani kubwa kwenye soko la dunia la bidhaa teknolojia.” amesema Mavunde 

Waziri Mavunde ameeleza kuwa mradi huo wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 15 utakapokamilika utazalisha takribani tani 200,000 za nikeli na shaba kwa mwaka, kuajiri zaidi ya Watanzania 200 hadi 230, na kuchangia kodi na mapato mengine ya Serikali.

“Uwekezaji huu ni kielelezo cha mafanikio ya Serikali katika kufanikisha dira ya uchumi wa viwanda na uongezaji thamani madini kama ilivyoelekezwa na Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020–2025," amesisitiza Mavunde. 

Amebainisha kuwa, pia Sera ya Madini ya mwaka 2009 inaelekeza kuyaongezea thamani madini yetu ndani ya nchi na kuongeza kuwa “hivi sasa Tanzania tuna viwanda vinane vya kusafisha madini ya dhahabu (gold refinery) lakini viwanda vya kuongezea thamani Madini ya metali tunavyo 9, mkoa wa Dodoma peke yake tunavyo vitano”  ameongeza Mavunde. 

Kwa upande wake, Kamishna wa Madini, Dkt. AbdulRahman Mwanga amesema kuwa, kwa kuwekeza kwenye miradi ya kuongeza thamani, Tanzania inajenga msingi imara wa ajira, mapato, na uchumi shindani kimataifa na kufikia lengo la ujenzi wa Tanzania ya uchumi.

Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Zhongzhou Mining Lee Zhong LIANG amemuhakikishia Waziri Mavunde kuwa Kampuni itaendeleza uhusiano mwema na Serikali pamoja wananchi wanaozunguka mradi huo.

Pia, Katibu Tawala Wilaya ya Bahi , Mwanamvua Muyongo ameeleza kuwa uwepo wa kiwanda hicho utasaidia kuiweka Wilaya hiyo katika ramani ya wazalishaji wa bidhaa muhimu za kiteknolojia pamoja na kuboresha maisha ya watu wa hapa kupitia ajira rasmi na zisizo za moja kwa moja.











 


Tanzania imeanza ujenzi wa maabara kubwa na ya kisasa ya uchunguzi wa sampuli za madini ambayo itakuwa ni kubwa kuliko zote kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati na ambayo itatoa huduma ya kimaabara kwa ubora na kwa uharaka kwa wadau wa sekta ya madini nchini.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Madini Mh.Anthony Mavunde wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa maabara ya kisasa ya uchunguzi wa sampuli za madini katika eneo la Kizota, jijini Dodoma.

“Tunamshukuru Mhe Rais Dkt. Samia  Suluhu kwa kuwa kinara wa mageuzi makubwa ya sekta ya madini na kwa kuandika historia ya ujenzi wa maabara hii ya kisasa miaka 100 baadaye tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa madini(GST) mwaka 1925," amesema Mavunde.

Ameongeza kwamba Tanzania  imeandika historia kuanza kwa ujenzi wa maabara kubwa  ambayo itafungwa mitambo na vifaa vya kisasa katika kutoa huduma za kimaabara ndani na nje ya nchi.

"Huu ni ukombozi mkubwa kwa wadau wa sekta ya madini katika kupata taarifa sahihi za kimaabara kwa wakati na zenye ubora wa hali ya juu ni imani yangu maabara hii itachochea ukuaji na maendeleo ya sekta ya madini," amesema Mavunde.

Naye,  Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini(GST) Dkt. Notka Huruma Batenze  amesema Maabara hiyo ya kisasa ya uchunguzi wa sampuli za madini utaleta tija kwa wadau wa sekta ya madini na kurahisisha upatikanaji wa huduma hii muhimu kwa maendeleo ya sekta ya madini.

Gharama za ujenzi wa maabara hiyo unatarajiwa kuwa Shilingi Bilioni 14.3 na muda wa ujenzi wa kukamilika maabara ni siku 690.

 

Serikali imetangaza rasmi kuanza kwa mchakato wa ulipaji fidia kwa wananchi wa Mitaa ya Nyakabale na Nyamalembo katika Halmashauri ya Manispaa ya Geita, ili kupisha shughuli za uchimbaji wa dhahabu katika Mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML). Hatua inayoleta suluhu ya mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 26. 

Akizungumza  Agosti 21, 2025 Mkoani Geita, Waziri wa Madini, Mhe.Anthony Mavunde, amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imekuwa ikifuatilia kwa karibu changamoto za wananchi wa Geita na kutoa maelekezo mahsusi kuhakikisha zinatatuliwa kwa ufanisi.

 “Nawashukuru sana wananchi kwa uvumilivu wenu kwa zaidi ya miongo miwili. Leo hii tunatangaza suluhu ya mgogoro huu kwa sababu Serikali yenu inawajali na Rais wetu amekuwa mstari wa mbele kutaka wananchi wapate haki zao bila usumbufu,” amesema Waziri Mavunde.

Mhe. Mavunde amebainisha kuwa GGML wameridhia kuanza mchakato wa kuwalipa fidia wananchi wa eneo la Nyakabale na Nyamalembo kwa mujibu wa utaratibu ili kupisha shughuli za mgodi. Amesema kuanzia kesho Agosti 22, 2005,  timu ya wataalamu wa Serikali itaanza kazi ya uthamini wa mali, na ndani ya siku 40 tathmini hiyo itakamilika ili wananchi waweze kulipwa stahiki zao.

Aidha, Waziri ameeleza kuwa, mgogoro huo ulikuwa na hoja 13 za msingi ambazo zilihitaji kushughulikiwa, ambapo ndani ya mwaka mmoja na miezi mitatu Serikali kwa kushirikiana na wadau imefanikiwa kutatua hoja 10 kati ya hizo na hatimaye leo kutatua hoja nyingine mbili.

Aidha, Waziri Mavunde ameeleza kuwa, katika jitihada hizo, GGML imekubali kurekebisha mipaka yake ya leseni ya uchimbaji lna kuliachia eneo linalobaki kwa ajili ya wakazi wa maeneo hayo.

“Ninawapongeza viongozi wote mlioshiriki, hususan Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella, na timu maalum iliyoundwa kushughulikia jambo hili kwa ufanisi mkubwa wamefanya kazi ya kupitia maoni ya wananchi na kuleta maoni ya wakazi hawa,  bila juhudi zao leo hii tusingefikia hatua hii” amesisitiza Mavunde. 

Pia, Waziri Mavunde ametumia nafasi hiyo kuwaonya na kuwakumbusha wananchi kuepuka tabia ya ‘tegesha’ kwani inaweza kukwamisha zoezi la tathmini na ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaostahili kupata haki zao kwa wakati na kuleta usumbufu kwa mwekezaji na wananchi. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella, amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kufuatilia kwa karibu mgogoro huo wa muda mrefu, na kumpongeza Waziri Mavunde kwa kusimamia utekelezaji kwa umakini.

“Wananchi wa Geita wamevumilia kwa muda mrefu. Tunawashukuru kwa ustahimilivu wao na tunahakikisha maelekezo ya Serikali yanatekelezwa ipasavyo kwa manufaa ya wote,” alisema Shigella.

Wananchi wanaotarajiwa kufanyiwa tathmini na kulipwa fidia ni wa mitaa ya Nyakabale na Nyamalembo ndani ya Manispaa ya Geita.

Hatua hiyo ya Serikali inatazamwa kama historia muhimu ya kumaliza mgogoro wa muda mrefu kwa zaidi ya miaka 26 na uliokuwa unachangia sintofahamu kati ya wananchi na mwekezaji, na sasa inaleta matumaini ya maendeleo na mshikamano endelevu katika Mkoa wa Geita.






 


Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Peter Mavunde, amesema ujenzi wa maabara ya kisasa ya utafiti na uchambuzi wa madini katika mkoa wa Geita ni hatua kubwa itakayosaidia kuwainua wachimbaji wa madini Kanda ya Ziwa na kuimarisha mchango wa Sekta ya Madini katika uchumi wa taifa.

Akizungumza leo Agosti 21, 2025 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa maabara hiyo, Mhe. Mavunde amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kukubali ombi la Wizara la kujenga maabara tatu za kisasa nchini. 

Amesema mbali na maabara hiyo inayojengwa Geita itakayogharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.5, maabara nyingine itajengwa Chunya mkoani Mbeya na maabara kubwa zaidi kimataifa itajengwa jijini Dodoma.

“Maabara hizi zitakuwa nguzo ya utafiti wa kisayansi wa sampuli za madini, kuongeza ufanisi wa wachimbaji wadogo na kupunguza gharama na usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizi, zitakuwa na vifaa vya kisasa zaidi” amesema Mavunde.

Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ndiyo moyo wa shughuli za madini hapa nchini kupitia kazi ya utafiti wa kijiolojia, hivyo kuanzishwa kwa kituo hicho kutasaidia kuchochea shughuli za madini hususan katika Ukanda wa Ziwa ambao unaongoza kwa shughuli za uchimbaji hapa nchini, zikiwemo mikoa ya kimadini ya Geita, Mbogwe, Kagera, Mwanza, Kahama, Mara na Shinyanga.

“Kwa mwaka uliopita pekee, sekta ya madini ilikusanya maduhuli shilingi bilioni 328 kutoka Mkoa wa Kimadini ya Geita, jambo linaloonesha mchango mkubwa wa ukanda huu katika pato la taifa na ndiyo maana uwekezaji huo umefanywa na Serikali hapa” amesisitiza Mavunde.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella, amesisitiza kuwa maabara hiyo itapunguza muda na gharama kwa wananchi waliokuwa wakilazimika kusafiri hadi Dodoma kufuata huduma hizo.

“Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia kwa kuona umuhimu wa kutuletea kituo hiki muhimu. Ni msaada mkubwa kwa wachimbaji na wananchi wetu wa Kanda ya Ziwa,” amesema RC Shigella.

Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Maabara wa GST, Notika Bandeze, amesema maabara hiyo1 mpya itakuwa na vifaa na mitambo ya kisasa zaidi, ikiwemo ya utambuzi wa madini, uchunguzi wa sampuli, pamoja na utoaji wa taarifa za kina za kijiolojia zinazohitajika na wachimbaji na wawekezaji.

Ujenzi wa maabara ya madini Mkoani Geita unatarajiwa kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali, kuokoa muda na mitaji kwa wachimbaji, na kuimarisha mchango wa sekta ya madini katika maendeleo ya taifa.











▪️Waziri Mavunde azindua Kiwanda cha kuongeza thamani madini Chumvi-Kigoma

▪️Ni cha uzalishaji Chumvi Lishe(๐ถ๐‘Ž๐‘ก๐‘ก๐‘™๐‘’ ๐ฟ๐‘–๐‘๐‘˜) kwa ajili ya Mifugo

▪️Lengo ni kupunguza uagizaji wa Chumvi Lishe kutoka nje ya Nchi

▪️Tanzania kuongeza uzalishaji wa Chumvi ghafi kwa matumizi ya viwandani


Uvinza,Kigoma

Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Nyanza Salt kwa kuitikia wito wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan wa uongezaji thamani madini nchini kwa kuanza rasmi uzalishaji wa chumvi lishe itokanayo na madini ya Chumvi mahususi kwa ajili ya kuongeza virutubisho vya mifugo.

Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Wilayani Uvinza-Kigoma wakati akizindua shughuli za  Kiwanda cha kuzalisha chumvi lishe(๐˜พ๐™–๐™ฉ๐™ฉ๐™ก๐™š ๐™‡๐™ž๐™˜๐™ ) kwa ajili ya mifugo kinachomilikiwa na Kampuni ya Nyanza Salt.

“Ni wito wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan na matakwa ya sheria juu ya uongezaji thamani madini yetu hapa nchini.

Nawapongeza Kampuni ya Nyanza kwa hatua hii kubwa ya kuitoa chumvi yetu katika matumizi ya kawaida na kuiongezea thamani kuzalisha Chumvi lishe ambayo ni muhimu kwa virutubisho vya mifugo.

Wafugaji wengi huagiza chumvi lishe kutoka nje ya nchi kwakuwa hakukuwa na uzalishaji hapa nchini,hatua hii ya leo ya uzalishaji wa ๐˜พ๐™–๐™ฉ๐™ฉ๐™ก๐™š ๐™‡๐™ž๐™˜๐™  nchini itapunguza uagizwaji wa bidhaa hii kutoka nje ya nchi kwa kiwango kikubwa hivyo natoa rai kwa wafugaji kuiunga mkono bidhaa hii inayozalishwa ndani ya ya nchi.

Tasnia ya chumvi inaendelea kukua kwa kasi siku hadi siku na lengo la serikali ni kuhakikisha tunaboresha mazingira ya uwekezaji kwenye eneo hili ili kuongeza tija na uzalishaji na kuondokana kabisa na uagizaji wa chumvi ghafi kutoka nje ya nchi kama malighafi ya viwanda” Alisema Mavunde

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Nyanza Salt Mines Ndg. Mukesh Mamlani amesema uzalishaji wa bidhaa ya chumvi lishe itokanayo na madini chumvi ni mkombozi kwa wafugaji wa Tanzania na kwamba kampuni itahakikisha inakidhi viwango na ubora wa bidhaa ili wafugaji wa Tanzania wanufaike.

Pia Ndg. Mukeshi ameeleza kwamba mpango wa Kampuni ni uzalishaji wa tani 120,000 za chumvi ifikapo mwaka 2027 ili kuhakikisha chumvi ya kutosha inapatikana nchini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Uvinza,Mh. Dina Mathamani amesema uwepo wa Kampuni ya Nyanza wilayani Uvinza umekuwa ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi na mapato kwa serikali na wananchi ambapo kupitia Ajira za moja  kwa moja na zisizo za moja kwa moja jumla ya wa wananchi 1000 wamekuwa wakipata Ajira kiwandani hapo wakati wa msimu wa uchakataji chumvi.

 



▪️Waziri Mavunde azindua Ghala la Mauzo ya vipuri vya Mitambo na Mashine kubwa za Madini


▪️Ni uwekezaji wa Kampuni kubwa za Mitambo kutoka India na Italia


▪️Vipuri vya mitambo na mashine kubwa za uchimbaji kupatikana nchini


▪️Rais Samia apongezwa kwa mazingira mazuri ya uwekezaji


Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde amesema Tanzania inajipanga kuwa kitovu cha utengenezaji wa bidhaa na huduma migodini kwa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara kwa kuvutia uwekezaji kwenye viwanda vya kutengeneza bidhaa za migodini na utoaji wa huduma kwenye migodi ya ndani na nje ya nchi.


Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati akizindua ghala la mauzo ya vipuri vya mitambo mikubwa  na vifaa  vya uchimbaji madini ambalo linamilikiwa kwa ushirikiano kati ya Kampuni ya Shan Parts Africa ya India na Kampuni ya ITR  ya Italy.


“ Nawapongeza sana Kampuni ya Shan Parts na ITR kwa uamuzi wa kuwekeza nchini Tanzania kwenye vipuri vya mitambo mikubwa na vifaa vya uchimbaji madini.


Uwepo wa huduma hii hapa nchini utapunguza uingizaji wa vipuri kutoka nje ya nchi kwa wingi na kupunguza gharama za uendeshaji.


Sekta ya Madini ni sekta muhimu kwa uchumi wa nchi yetu,kuwa na huduma kama hii itasaidia sana kuchochea ukuaji wa sekta ya madini.


Tumetenga eneo la Buzwagi,Kahama kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani na huduma migodini.


Lengo ni kuhakikisha tunaifanya Tanzania kuwa kitovu cha usambazaji wa bidhaa na huduma migodini ya ndani ya nchi na kwa nchi jirani zinazozunguka nchi ya Tanzania”Alisema Mavunde


Nao Balozi wa India Nchini Mh. Bishwadip Ney na Balozi wa Italia Mh.  Giuseppe Coppola wamepongeza ushirikiano wa kibiashara wa nchi tatu za Tanzania,India na Italia na kuahidi kuendeleza ushirikiano wa kibiashara na kukuza sekta ya madini ambayo ndi sekta muhimu kwenye kuchochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Shan Parts Africa Ltd Ndg. Malhar Dave amesema mazingira mazuri ya uwekezaji chini ya Uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan yamewezesha Kampuni hiyo kuamua kuwekeza hapa Tanzania huku akibainisha Mpango wa Kampuni ni kuhakikisha inasambaza vipuri vyenye ubora wa hali ya juu kuendana na mazingira ya Teknolojia ya Dunia ya leo na hivyo kuchochea katika ukuaji wa sekta ya madini.

 


Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amekabidhi Leseni ya Utafiti na Uchimbaji Mkubwa wa Madini Adimu na Muhimu ambayo ni ya kimkakati ya Rare Earth Elements (REE) kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), ikiwa ni hatua muhimu ya kuliwezesha shirika kuingia kwenye shughuli za uchimbaji mkubwa kwa lengo la kuwanufaisha wananchi wote wa Tanzania.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo Julai 24, 2025 katika viwanja vya Shule ya Msingi Sesenga kijiji cha Sesenga Kata ya Mgazi Wilaya ya Morogoro, kufuatia uamuzi wa Serikali wa kuirejesha leseni hiyo kutoka kwa kampuni ya Wigu Hill Mining Company Limited baada ya kumalizika kwa shauri la madai kwenye Baraza la Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID).

Akizungumza mbele ya mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara kwenye hafla ya makabidhiano ya leseni hiyo, Waziri Mavunde amesema kuwa madini ya Rare Earth Elements ni miongoni mwa madini ya kimkakati ambayo kwa sasa yanahitajika kwa kiwango kikubwa duniani  kutokana na umuhimu wake katika sekta ya teknolojia ya kisasa.

"Madini haya yanatumika katika vifaa vya kivita, kutengeneza simu janja, kompyuta, betri za magari ya umeme, vifaa vya matibabu na mashine mbalimbali. Hii ni fursa adhimu kwa kijiji cha Sesenga, Wilaya ya Morogoro, Mkoa na Taifa kwa ujumla kunufaika na rasilimali hii muhimu," amesisitiza Waziri Mavunde.

Pia, Waziri Mavunde amebainisha kuwa mradi huo utafungua fursa nyingi za ajira kwa wakazi wa maeneo ya jirani na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kupewa kipaumbele kwa wananchi wanaozunguka mgodi kuuza bidhaa zao mgodini (Local content) na kupitia uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR).

Vilevile, ameeleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro itaongeza mapato yake kupita tozo za huduma ambazo hutozwa kwenye shughuli za madini.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde ameitaka STAMICO kuanza mara moja mchakato wa uendelezaji wa leseni hiyo ili shughuli za uzalishaji madini hayo ziweze kuanza  kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mussa Kilakala amempongeza Waziri Mavunde kwa kuisimamia vizuri Sekta ya Madini na kumuahidi Waziri huyo kuendelea kusimamia sekta hiyo kwa karibu kwa ajili ya masilahi ya taifa.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Eng. Yahya Samamba amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira rafiki na salama kwenye maeneo ya uchimbaji madini nchini ambapo kwa sasa wachimbaji wananufaika na rasilimali hiyo.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuendelea kuwaamini na kulikabidhi shirika hilo leseni hiyo muhimu na kumhakikishia Waziri Mavunde kuwa STAMICO iko tayari kuanza kazi kwa wakati na kuhakikisha kuwa mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi, kwa muda uliopangwa na kwa kuzingatia manufaa mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

"Tunatambua wajibu wetu mkubwa kwa taifa, STAMICO iko tayari kusimamia mradi huu kwa weledi wa hali ya juu ili kuleta tija na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa," amesema Dkt. Mwasse.

Uamuzi wa Serikali kukabidhi leseni hiyo kwa STAMICO ni sehemu ya jitihada za kulinda maslahi ya Taifa katika Sekta ya Madini kwa kuhakikisha maeneo yenye rasilimali hayakai bila kuendelezwa na kwamba rasilimali hizo zinachangia moja kwa moja katika ustawi wa wananchi na uchumi wa nchi.

  


▪️Bilioni 33 kukutumika kukamilisha Jengo la ghorofa pacha-TGC Arusha

▪️Biashara ya madini kufanyika kwenye Jengo

▪️Ni mkakati wa uongezaji thamani madini ya vito

▪️Wachimbaji Arusha wamshukuru Rais Samia kwa miundombinu ya jengo

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, leo Julai 22, 2025 ametembelea eneo la ujenzi wa jengo la kisasa la ghorofa nane la Kituo cha Jeomolojia Tanzania (TGC), linaloendelea kujengwa jijini Arusha, kwa lengo la kukagua maendeleo ya mradi huo muhimu kwa Sekta ya Madini nchini.

Katika ziara hiyo, Waziri Mavunde amepata fursa ya kujionea hatua mbalimbali za ujenzi na kupokea taarifa ya maendeleo kutoka kwa Mhandisi Julian Mosha wa Kampuni ya Skywards Lumocons Joint Venture pamoja na msimamizi wa mradi Jumanne Nshimba kutoka TGC ambapo baada ya kukamilika kwake unatarajiwa kuwa kitovu cha huduma za utambuzi wa madini, tafiti na mafunzo kuhusu vito vya thamani na madini mengine nchini, na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia mnyororo wa thamani wa Sekta ya Madini.

Amesema Jengo hilo linatarajiwa kuwa na madarasa ya wanafunzi, karakana, mabweni ya wanafunzi, maabara ya madini pamoja na ofisi mbalimbali kwa ajili ya uongozi wa chuo hicho ambapo zaidi ya bilioni 33 zinategemewa kukamilisha mradi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ukaguzi huo, Mhe. Mavunde ameeleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa lakini amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.

“Mradi huu ni wa kimkakati kwa mustakabali wa Sekta ya Madini nchini ambao utawaleta pamoja wafanyabiashara wa madini (One Stop Centre). Tunahitaji kuona ujenzi ukikamilika haraka ili Kituo hiki kianze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa. Natoa wito kwa mkandarasi kuongeza nguvu kazi, vifaa na ufanisi ili kuendana na muda wa mkataba,” amesema Waziri Mavunde.

Mradi huo unatekelezwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Madini kwa kushirikiana na taasisi ya TGC, ambapo jengo hilo litakapokamilika litaongeza uwezo wa kitaifa wa kuchambua madini, kutoa mafunzo ya kitaalamu, na kukuza ajira kwa vijana wa Kitanzania waliobobea katika masuala ya Jiolojia na Jiomolojia.

Aidha, Waziri Mavunde amesisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuimarisha miundombinu ya kisayansi na kiteknolojia kwa ajili ya matumizi bora ya rasilimali za madini na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na uongezaji thamani madini katika Ukanda wa Afrika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Mwenyekiti wa Wachimbaji Mkoani Arusha (AREMA) Ndg. Alfred Mwaswenya na Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Madini (CHAMATA) Ndg. Jeremia Kituyo wamemshukuru Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa uamuzi wake wa ujenzi wa jengo ambalo litazalisha watanzania wenye ujuzi ya kuchakata madini ya vito lakini pia kurahisisha biashara ya madini kufanyika katika eneo hilo kwa kuwa litawakusanya wadau kwa wakati mmoja.

Akizungumza katika ziara hiyo,Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mh.Kenani Kihongosi  ameipongeza Serikali kupitia wizara ya madini kwa ujenzi wa Jengo la kisasa la ghorofa nane la TGC ambalo litasaidia katika kuchochea biashara ya madini mkoani Arusha na kukuza uchumi wa wananchi wa Arusha.









 -Serikali kupunguza ada ya kodi ya pango kwa mwaka kwa Leseni ya chumvi


-Rais Samia apongezwa kwa kiwanda cha kusafisha chumvi Lindi

-Wazalishaji wa chumvi wafurahia kuanza kwa kodi ya zuio

-Serikali kudhibiti uingizaji wa chumvi kiholela nchini

Dar es Salaam

Katika kuwajengea uwezo wazalishaji wa chimvi nchini,Serikali imekuja na mikakati mbalimbali kufikia azma hiyo ikiwemo upunguzaji wa ada ya pango kwa mwaka ya leseni (Annual Rent) za uchimbaji mdogo wa chumvi nchini ili kusaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kuchochea uzalishaji wa wingi wa chumvi nchini.

Hayo yamesemwa jana tarehe 15 Julai, 2025 na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde (Mb) Jijini Dar es Salaam alipokuwa akifunga Kikao cha wadau wa sekta ndogo ya chumvi chini ya Chama cha Wazalishaji wa Chumvi Tanzania (TASPA).

"Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kutubeba sekta ya madini na wachimbaji kwa ujumla. Ni yeye aliyetuelekeza kusikiliza kilio chenu na kutatua changamoto zinazowakabili ili mnufaike na shughuli mnazofanya"

"Ametuelekeza Wizara ya Madini tuliridhie ombi lenu na kupunguza ada ya pango ya mwaka ya leseni ya uchimbaji mdogo kutoka Shilingi 45,000 mpaka Shilingi 20,000 kwa hekta, hili linakwenda kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ubora wa chumvi ya mzalishaji mdogo" alieleza Mhe. Mavunde.

Aidha, Waziri Mavunde alibainisha kuwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ikiwemo udhibiti wa chumvi inayoingizwa kutoka nje ya nchi, zimepelekea bei ya chumvi ghafi kuongezeka na hivyo kuwanufaisha zaidi wazalishaji wadogo wa chumvi nchini.

Uanzishwaji wa kodi ya zuio ya asilimia mbili (2%) kwenye mauzo ya chumvi ghafi kwa wazalishaji wenye leseni za PML imekuwa ni neema na manufaa kwao badala ya utaratibu wa awali wa kufanyiwa makadirio ya kodi ya mapato, ambao ulikuwa ni kero kubwa kwa wazalishaji wadogo.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde alieleza kuwa Kiwanda cha kuzalisha chumvi cha STAMICO kipo hatua za mwisho, na kuagiza Shirika hilo kuhakikisha kabla ya mwezi wa Agosti kuisha kiwe kimekamilika na kuanza uzalishaji wa chumvi ili kupanua wigo wa soko la chumvi ya wazalishaji wadogo.

Awali, akitoa taarifa ya utendaji wa Taasisi yao, Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji wa Chumvi Tanzania (TASPA), Bi. Hawa Ghasia aliishukuru Serikali kwa kushughulikia changamoto zilizokuwa zinaikabili sekta ndogo ya chumvi nchini ambazo zimepelekea bei ya chumvi kupanda na kuwanufaisha zaidi wazalisha chumvi nchini.



 


▪️Aelekeza mabadiliko ya Kanuni ili kuruhusu uhaulishwaji teknolojia kwa Kampuni za Kigeni

▪️Ataka Watanzania kuchangamkia Trilioni 5.3 za usambazaji bidhaa na utoaji huduma

▪️Rais Samia apongezwa kwa uongozi wa maono

▪️Watanzania 19,371 wanufaika na ajira rasmi

▪️Kamati ya Bunge yaipongeza Wizara kwa ukuaji wa sekta


Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde ameitaka Tume ya Madini kuwapa kipaumbele watanzania kwenye usambazaji wa huduma na bidhaa kwenye migodi ya madini ili kujipatia kipato, kuongeza mzunguko wa fedha nchini hivyo Sekta ya Madini kuendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa.

Mhe. Waziri Mavunde ameyasema hayo mapema leo Juni 17, 2025 jijini Mwanza kwenye ufunguzi wa Jukwaa la Nne la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini linalokutanisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wizara ya Madini na Taasisi zake, Taasisi za Serikali, Taasisi Binafsi, Taasisi za Fedha, Kampuni za Uchimbaji wa Madini na Watoa Huduma kwenye Migodi ya Madini.

Amesema kuwa katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na kuhakikisha watanzania wananufaika na rasilimali madini, Serikali imeendelea kusimamia ipasavyo Sheria ya Madini, Sura 123 Kifungu Na. 102 na Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za Mwaka 2018 ili kuweka usimamizi thabiti katika utekelezaji wa masuala ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini nchini.

Amesisitiza kuwa lengo la uwepo wa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ni kuhakikisha watanzania wanashiriki ipasavyo kupitia usambazaji wa bidhaa na huduma kwenye migodi ya madini badala ya kampuni kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi.

Aidha Mhe. Mavunde ameitaka Tume ya Madini kufanya mabadiliko ya Kanuni ili kuruhusu uhaulishwaji teknolojia kwa Kampuni za Kigeni ambapo itatoa fursa kwa kampuni za kitanzania kushirikiana na kampuni za kigeni kwenye utoaji wa huduma migodini na kujifunza teknolojia mpya kutoka kampuni za kigeni.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa ya kuendeleza Sekta ya Madini hali iliyopelekea mabadiliko makubwa ambapo mpaka sasa mafanikio makubwa yamepatikana.

“Mpaka sasa mafanikio makubwa yamepatikana hasa kwa wachimbaji wadogo ambapo wameanza kukopesheka kutoka kwenye Taasisi za Fedha, ushiriki wa watanzania kwenye shughuli za uchimbaji, uchenjuaji, biashara ya madini na utoaji wa bidhaa na huduma kwenye migodi ya madini umeongezeka na mchango wa wachimbaji wadogo kwenye makusanyo ya maduhuli umeendelea kuimarika,” amesisitiza Mhe. Mavunde.

Akielezea mafanikio ya utekelezaji wa kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini, Waziri Mavunde amesema katika kipindi cha mwaka 2023/2024 jumla ya ajira rasmi 19,874 zilizalishwa katika migodi ya madini ambapo ajira 19,371 sawa na asilimia 97 zilitolewa kwa Watanzania na ajira 503 sawa na asilimia 3 zilitolewa kwa wageni.

Aidha, amewataka watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini hasa kwenye usambazaji wa bidhaa na huduma kwenye migodi ya madini kama vile usambazaji wa vifaa, vyakula na huduma na kuzitaka Taasisi za Kifedha kuendelea kuwakopesha mitaji.

Amesema kuwa kampuni za madini zinatumia kiasi cha shilingi Trilioni 5.3 kila mwaka kwa ajili ya manunuzi ya bidhaa na huduma zinazotumika migodini na kuwataka watanzania kuchangamkia fursa hizo.

Naye Mkuu wa Wilaya Ilemela, Mhe. Hassan Masala akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda amempongeza Waziri Mavunde kwa usimamizi mzuri wa Sekta ya Madini hali iliyopelekea mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na ongezeko la wawekezaji nchini.

Ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika mkoa wa Mwanza hasa katika eneo la uchimbaji wa madini na utoaji wa huduma mbalimbali kwenye migodi ya madini.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amesisitiza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kufungamanisha Sekta ya Madini na sekta nyingine muhimu za kiuchumi ili kuongeza ushiriki wa watanzania kwenye shughuli za madini nchini.

Wakati huohuo akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dkt David Mathayo, Mbunge wa Ilemela, Dkt. Angeline Mabula amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Waziri Mavunde hali iliyochangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa.

“Kupitia uongozi wa Mhe. Mavunde tumeshuhudia mapinduzi makubwa kwenye Sekta ya Madini ambapo Tanzania imepiga hatua kubwa ya kihistoria kwa kufikia mchango wa asilimia 10.1 katika Pato la Taifa kwa Mwaka 2024, ikiwa ni Mwaka mmoja (1) kabla ya lengo la asilimia 10 lililowekwa kwenye Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026),” amesisitiza Dkt. Mabula

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo amesema kuwa Tume imeanza kukusanya takwimu za bidhaa zinazoingizwa nchini ili kushauri Serikali kuhusu uanzishwaji wa viwanda vinavyotoa bidhaa husika na kuongeza mzunguko wa fedha nchini huku wananchi wakijipatia ajira.

Katika hatua nyingine, Kamishna wa Tume ya Madini ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, Dkt. Theresia Numbi ameeleza mikakati iliyowekwa na Tume ya Madini ya kuongeza ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini kuwa ni pamoja na mikutano, majukwaa na vyombo vya habari.

 



Chama Cha Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dodoma (UMAPIDO), kimepongeza jitihada za Jeshi la Polisi Mkoani hapo kwa kuwezesha uzinduzi wa Ofisi ya Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) cha umoja huo.

Akizungumza katika uzundunzi huo Juni 11,2025 kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwamdamizi wa Polisi George Katabazi amesema Jeshi la Polisi la mbali na kuchangia fedha za ukamilishwaji wa chama hicho pia linatambua mchango wa maafisa hao katika kuzuia na kutanzua uhalifu.

Aidha katabazi amewataka wanachama hao kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi katika nyanja mbalimbali hususani kukemea uhalifu kuelimisha umma juu ya matumizi sahihi ya barabara pamoja na kuheshimu sheria za usalama barabarani.

Katibu wa Chama Cha Boda boda na bajaji Mkoa wa Dodoma Yusufu Mwamonje amesema Jeshi la Polisi limekuwa na mahusiano mazuri na chama hicho kwa kuinua uchumi wa chama, upatikanaji wa leseni kwa madereva hao pamoja na kushiriki katika mabonanza ya michezo
yaliyo kuwa yakiandaliwa na jeshi la polisi chini ya Rpc Katabazi ikiwemo
ligi mbalimbali za mpira wa miguu Polisi Family Day, pamoja na kuandaa mikutano ya kuhamasisha vikundi vya ulinzi shirikishi.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika uzinduzi huo Waziri wa Madini Mhe, Athony Mavunde amepongeza chama hicho kwa kufanya mageuzi yatakayo changia maendeleo kwa kila mwana chama

Vilevile, Mavunde ameeleza umuhimu wa kushirikiana na Jeshi la Polisi katika sekta hiyo ya usafirishaji pamoja na kutoa tuzo ya heshima kwa kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma (SACP), Katabazi kwa kuwaongoza askari kutoa huduma bora kwa wananchi wa Dodoma na kuimarisha ulinzi na usalama.