▪️Waziri Mavunde azindua Ghala la Mauzo ya vipuri vya Mitambo na Mashine kubwa za Madini


▪️Ni uwekezaji wa Kampuni kubwa za Mitambo kutoka India na Italia


▪️Vipuri vya mitambo na mashine kubwa za uchimbaji kupatikana nchini


▪️Rais Samia apongezwa kwa mazingira mazuri ya uwekezaji


Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde amesema Tanzania inajipanga kuwa kitovu cha utengenezaji wa bidhaa na huduma migodini kwa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara kwa kuvutia uwekezaji kwenye viwanda vya kutengeneza bidhaa za migodini na utoaji wa huduma kwenye migodi ya ndani na nje ya nchi.


Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati akizindua ghala la mauzo ya vipuri vya mitambo mikubwa  na vifaa  vya uchimbaji madini ambalo linamilikiwa kwa ushirikiano kati ya Kampuni ya Shan Parts Africa ya India na Kampuni ya ITR  ya Italy.


“ Nawapongeza sana Kampuni ya Shan Parts na ITR kwa uamuzi wa kuwekeza nchini Tanzania kwenye vipuri vya mitambo mikubwa na vifaa vya uchimbaji madini.


Uwepo wa huduma hii hapa nchini utapunguza uingizaji wa vipuri kutoka nje ya nchi kwa wingi na kupunguza gharama za uendeshaji.


Sekta ya Madini ni sekta muhimu kwa uchumi wa nchi yetu,kuwa na huduma kama hii itasaidia sana kuchochea ukuaji wa sekta ya madini.


Tumetenga eneo la Buzwagi,Kahama kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani na huduma migodini.


Lengo ni kuhakikisha tunaifanya Tanzania kuwa kitovu cha usambazaji wa bidhaa na huduma migodini ya ndani ya nchi na kwa nchi jirani zinazozunguka nchi ya Tanzania”Alisema Mavunde


Nao Balozi wa India Nchini Mh. Bishwadip Ney na Balozi wa Italia Mh.  Giuseppe Coppola wamepongeza ushirikiano wa kibiashara wa nchi tatu za Tanzania,India na Italia na kuahidi kuendeleza ushirikiano wa kibiashara na kukuza sekta ya madini ambayo ndi sekta muhimu kwenye kuchochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Shan Parts Africa Ltd Ndg. Malhar Dave amesema mazingira mazuri ya uwekezaji chini ya Uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan yamewezesha Kampuni hiyo kuamua kuwekeza hapa Tanzania huku akibainisha Mpango wa Kampuni ni kuhakikisha inasambaza vipuri vyenye ubora wa hali ya juu kuendana na mazingira ya Teknolojia ya Dunia ya leo na hivyo kuchochea katika ukuaji wa sekta ya madini.

Share To:

Post A Comment: