Mbunge wa Jimbo la  Kisarawe, Dkt. Selemani Jafo,akiuliza swali la nyongeza leo Januari 29,2026 bungeni jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna, Dodoma

Mbunge wa Jimbo la  Kisarawe, Dkt. Selemani Jafo, amehoji mpango wa Serikali wa kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Mlandizi–Mzenga–Maneromango kwa kiwango cha lami, akisisitiza kuwa ni barabara muhimu kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.

Akiuliza swali la nyongeza Bungeni, Dkt. Jafo amesema barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 70.2 inaanzia Mlandizi kupitia Mzenga hadi Maneromango, na kwamba tayari upembuzi yakinifu umekamilika.

Ameeleza kuwa kwa sasa mkandarasi ameanza kazi katika kipande cha Mzenga chenye urefu wa mita 300, hali iliyomfanya kuihoji Serikali kuhusu mpango wake wa kuongeza fedha katika bajeti ya mwaka huu ili kufungua kipande cha Mlandizi hadi Mzenga.

“Nini mpango wa Serikali katika bajeti ya mwaka huu kuongeza fedha ili kuhakikisha barabara hii muhimu inaanza kujengwa kuanzia Mlandizi hadi Mzenga?” amehoji Dkt. Jafo.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema Serikali tayari imeonesha nia ya dhati ya kuijenga barabara hiyo, akibainisha kuwa kutokana na ukubwa na umuhimu wake, lazima ijengwe kwa kiwango cha lami.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutenga na kuongeza fedha kadri zinavyopatikana, ili kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unaendelea hadi kukamilika kwa kiwango kilichokusudiwa.

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Alex Sonna

Post A Comment: